[update] Pongezi kwa timu ya madaktari waliofanikisha upasuaji mkubwa wa moyo TanzaniaMtoto Happiness John Mkazi wa Seliani Arusha aliyefanyiwa upasuaji kwenye moyo na kupandikiziwa kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker), ameanza mazoezi.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Sulender Kuboja aliyeshiriki upasuaji huyo alisema jana kuwa hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na wameanza kumfanyia mazoezi mepesi.

Dk Kuboja alisema kwa kawaida mgonjwa yeyote aliyefanyiwa upasuaji anapaswa kufanyiwa mazoezi mepesi na kwamba kwa mtoto, mazoezi anayofanyiwa ni ya kukaa, kusimama na kutembea kidogo.
“Hali yake inaonekana kuendelea vizuri sana... nimetoka kumfanyia vipimo muda mfupi uliopita kifaa kile kinafanya kazi vizuri na maendeleo yake yanaridhisha sana,” alisema Dk Kuboja.
Alisema mtoto huyo anaweza kuongea na hata kula chaku- la, hali aliyosema inaonyesha nafuu nzuri kwake.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Elitruda Malley alisema anaridhishwa na maendeleo ya afya ya mwanaye kwa kuwa tangu afanyiwe upasuaji huo juzi, hali yake imeonekana kuimarika kwa haraka.
Mama huyo alisema tangu awekewe kifaa hicho, mwanaye amekuwa mchangamfu, hali aliyosema inamtia moyo na kumpa matumaini makubwa.
“Ingawa yupo kwenye oxygen, lakini namshukuru Mungu kwani anaonekana anapata nafuu nzuri, anatabasamu na kuongea vizuri kabisa na ana furaha sana, shauku yake ni apone ili aende shule kama watoto wengine,” alisema Malley.
Aliongeza kuwa mtoto huyo amekuwa akila vizuri na kumpa moyo kwani mwili wake unaonekana kuwa na nguvu na afya nzuri.
“Madaktari wapo karibu wakifuatilia afya ya mtoto kwa ukaribu, wanampa chakula, wanamfanyia mazoezi ya kukaa na kushuka chini, anaonekana kuwa na nguvu na mwenye maendeleo mazuri. "
Alisema jambo linalompa faraja ni kuona jinsi madaktari wote wanaomuhudumia mtoto huyo wanavyofanya kazi hiyo kwa upendo na bidii.

Juzi, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilifanikiwa kumpandikiza mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitano kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker) kinachoendeshwa kwa betri.

Hayo ni mafanikio ya pili kwa taasisi hiyo ya kisasa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya Mei 24 na 25, mwaka huu kufanikisha operesheni kwa wagonjwa 18 bila kuusimamisha moyo.
Na John Stephen, MNH

Dar es Salaam, Tanzania.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)-Muhimbili Julai 15 mwaka huu ilifanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa mtoto, Happiness John Josephat ambaye amepandikizwa pacemaker (betri ya umeme wa moyo) kwenye mfumo wa moyo wake.

Mmoja wa madaktari wa moyo walioshiriki kwenye upasuaji huo, Dk Godwin Sharau wa taasisi hiyo amesema upasuaji huo umechukua saa moja na kwamba mtoto anaendelea vuzuri.

Dk Sharau amesema mtoto huyo amepandikizwa pacemaker ambayo itasaidia kuunganisha mishipa ya fahamu ya umeme wa moyo ambayo inaunganisha vyumba vya moyo vya juu na chini kwenye moyo wa binadamu.
“Upasuaji huu ni wa kwanza kufanyika Tanzania. Upasuaji kama huu unafanyika kwa watu wazima, lakini watu wazima hawahitaji upasuaji wa moyo wa kupandikiza. Watoto wanahitaji upasuaji wa moyo wa kuipandikiza.
“Tatizo la mtoto huyu ni la kuzaliwa. Na ni nadra kutokea. Inaweza kupita miaka mingi bila watoto kutokea tatizo kama hilo. Upasuaji umefanywa kwa ushirikiano wa madaktari wa moyo na madaktari wa matibabu ya moyo nikiwamo mimi (Dk. Godwin Sharau), Dk Michael Valentine kutoka Marekani, Dk Kisenge na Dk Sulende Kubhoja, daktari wa usingizi, Dk Anjelan Muhozya na madaktari wengine ambao wamesaidia katika upasuaji huu,” amesema Dk Godwin Sharau.
Mama wa mtoto huyo, Elitruda Eligi Malley ambaye ni mkazi wa Sakina-Raskazone mkoani Arusha amewashukuru madaktari wa Taasisi hiyo kwa kufanya upasuaji huo na mtoto wake kutoka salama katika chumba cha upasuaji. Kutoka kushoto ni Dk Michael Valentine kutoka Marekani, Dk Godwin Sharau wa JKCI-Muhimbili, Mama wa mtoto huyo, Elitruda Eligi Malley na Dk Anjelan Muhozya wakifuatilia afya ya mtoto, Happiness John Josephat baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Baadhi ya madaktari wakifuatilia maendeleo ya mtoto, Happiness John Josephat kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo katika taasisi hiyo.


Mama wa mtoto huyo, Elitruda Eligi Malley akimwangalia mtoto wake, Happiness John Josephat baada ya kufanyiwa upasuaji