[update] Ripoti ya Jaji Warioba ya kutisha...


Mwaka huu, Tanzania inaye Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli. Rais Magufuli, ameonyesha nia ya dhati ya kupambana na vitendo vya rushwa nchini, na hasa baada ya kuanzisha rasmi mchakato wa Mahakama ya Mafisadi kwa kuitengea bajeti katika mwaka huu wa fedha. Katika kuunga mkono juhudi zake, Gazeti la JAMHURI, linaloanzia wanapoishia wengine, limeamua kuchapisha Ripoti ya Rushwa ya Jaji Warioba aliyoitoa mwaka 1996.

Kwa hali ya kawaida, Ripoti hii bado iko sahihi kwa asilimia 100, na hivyo inahitaji kufanyiwa kazi. Ripoti hii katika baadhi ya maeneo inataja wala rushwa kwa majina na vyeo vyao. Ripoti hii iliyoandaliwa kwa umakini wa hali ya juu ikifanyiwa kazi, Tanzania yenye neema itawadia haraka. Isome…

SURA YA KWANZA

UTANGULIZI

1. Tarehe 17 Januari, 1996, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Tume ya Kuchunguza Kero ya Rushwa nchini. Tume hii ina wajumbe wafuatao:

1. Mh. J. S. Warioba – Mwenyekiti

2. Bw. I. M. Kaduma – Mjumbe

3. S. Mworia – Mjumbe

4. Bw. L.T. Gama – Mjumbe

5. Bibi H. Kasungu – Mjumbe

6. Bw. Salim J. Othman – Mjumbe

7. Brig. H. I. Mbita – Mjumbe

8. Balozi F. Kazaura – Mjumbe

9. Bw. A. A. Muganda – Katibu

Ilipofika mwezi Machi, 1996, Balozi F. Kazaura aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Afrika Mashariki na Mheshimiwa Rais alimteua Bwana J. Sepeku kuchukua nafasi yake. Tume ilisaidiwa na Sekretarieti iliyoongozwa na Katibu.

2. Kulingana na barua ya Rais ya tarehe 17 Januari, 1996, Tume iliundwa chini ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32, kifungu cha 2(1) na ilipewa hadidu za rejea zifuatazo:

(a) Kutathmini sheria, kanuni na taratibu ili kubainisha mianya ya rushwa kuhusu:-

(i) Ukadiriaji na ukusanyaji kodi

(ii) Utoaji leseni na vibali mbalimbali

(iii) Taratibu za ununuzi, hususani utoaji wa tenda

(iv) Taratibu za kudai na kutoa haki

(v) Taratibu za kutoa huduma za jamii

(b) Kuchunguza ubora wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo zinazosimamia mapambano dhidi ya rushwa na kupokea mapendekezo ya jinsi ya kuziboresha.

(c) Kuchunguza uwezo na uhusiano wa vyombo vinavyosimamia mapambano dhidi ya rushwa na kushauri jinsi ya kuviimarisha.

(d) Kubuni mikakati na mbinu mpya za kupambana na rushwa.

(e) Kuchunguza na kutoa ushauri kuhusu utekelezaji bora wa Sheria ya Maadili ya Uongozi ya 1995, kwa lengo la kujenga imani ya wananchi katika uadilifu wa viongozi.

(f) Kupokea malalamiko, maoni na ushauri kutoka kwa wananchi kama mtu mmoja mmoja au kama vikundi au kama jumuiya.

(g) Kuwasilisha kwenye vyombo vinavyohusika malalamiko au taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vya rushwa ambavyo vinahitaji uchunguzi wa mara moja.

3. Tume ilitakiwa kufanya kazi katika muda usiozidi miezi tisa. Katika kipindi hicho Tume inaweza wakati wowote kukamilisha na kuwasilisha serikalini taarifa juu ya suala lolote inalolifanyia kazi ikiwa itaona linahitaji kuchukuliwa hatua mapema zaidi.

UTARATIBU WA KUFANYA KAZI

4. Tume ilifanya kikao chake cha kwanza tarehe 26 Januari, 1996 ambacho kiliandaa na kuweka mikakati ya utekelezaji wa kazi zake. Tume iliandaa taarifa kwa vyombo vya habari kueleza majukumu yake na kuwaomba wananchi kutoa maoni yao ama kwa maandishi au kufika kwenye Ofisi ya Tume. Pamoja na kupitia sheria mbalimbali zilizotajwa katika hadidu za rejea, Tume ilipitia na kusoma taarifa nyingi ambazo baadhi yake ni:

(i) Muhtasari wa Taarifa ya Uchambuzi wa Mikakati na Mbinu za Kupambana na Rushwa Nchini iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi 1989.

(ii) Taarifa ya Tume ya Shivji kuhusu Sera ya Ardhi na Mfumo wa Kumiliki Ardhi Nchini.

(iii) Taarifa za Crown Agents kuhusu taratibu za ugavi na zabuni za ujenzi serikalini.

(iv) Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya mwaka 1993/94.

(v) Kanuni na Taratibu za Ujenzi Nchini kama zilivyoandaliwa na Baraza la Ujenzi.

(vi) Ripoti mbalimbali za Shirika la Transparency International.

(vii) Taarifa za Shirika la Forum Against Corrupt Elements in Tanzania (FACEIT).

(viii) Taarifa ya Tume ya Rais ya Kupunguza Matumizi ya Serikali – Machi 1994.

(ix) Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu tuhuma dhidi ya Idara ya Wanyamapori – Novemba 1994.

(x) Taarifa ya Tume ya Mtei – 1991.

(xi) Ripoti mbalimbali za SGS na InchCape

5. Tume ilikutana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Jaji Mkuu, majaji wa Mahakama Kuu za Kanda ya Mwanza, Tanga, Arusha na Tabora. Tume pia ilikutana na Kamati ya Uongozi ya Bunge, Kamati ya Fedha ya Bunge, Waziri wa Sheria, Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Meya wa Mji wa Dodoma. Aidha ilikutana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Katibu Mkuu Utumishi.

Tume pia ilikutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato na wasaidizi wake, Kamishna wa Ardhi na Mkurugenzi wa Mipango Miji Wizara ya Ardhi; Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Rasilimali; Wakurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Uvuvi na Misitu, Wizara ya Maliasili na Utalii; Mkurugenzi wa Biashara Wizara ya Viwanda; Maofisa Biashara na Sheria wa Jiji la Dar es Salaam, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na wahandisi kadhaa wa Wizara ya Ujenzi.

6. Tume pia ilikutana na Mkurungenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa

Taifa, Inspekta Jenerali wa Polisi, Kamishna Mkuu wa Magereza na Mkurugenzi

wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Aidha ilikutana na viongozi wastaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa; Polisi; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Idara ya Ushuru wa Forodha ili kupata utaalamu na uzoefu wao katika mapambano dhidi ya rushwa.

7. Tume iliwaalika viongozi wa vyama vya siasa nchini ili waweze kutoa maoni yao kuhusu tatizo la rushwa nchini, lakini wito huo uliitikiwa na viongozi wa CCM, CHADEMA na UDP tu. Uongozi wa NCCR Mageuzi ulikataa wito huo kwa kueleza kwamba Tume imeundwa kwa misingi ya kibaguzi kwa kutoshirikisha vyama vya upinzani na ina sura ya CCM na vyombo vyake.

Aidha Chama cha Wananchi (CUF) kilikataa wito huo kwa kueleza kwamba hawakushirikishwa tangu mwanzo na wanaotakiwa na Tume hiyo ni chama kilichopo madarakani, yaani CCM na wala si vyama vipya vya siasa. Kadhalika Tume ilikutana na viongozi wa baadhi ya mashirika ya umma ya TANESCO, Simu, THA na PPF, wakuu wa makampuni vya TCCIA, Dar es Salaam Chamber of Commerce, Dar es Salaam Merchant Chambers, Dar es Salaam Hunters Association, Tanzania Tour Operators.

Vile vile ilikutana na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya Forum Against Corrupt Elements in Tanzania (FACEIT) na Alcohol and Drug Information Centre (ADIC). Aidha Tume ilikutana na wananchi mbalimbali wapatao 847 ambao walijitolea kutoa maoni yao kuhusu tatizo la rushwa nchini.

8. Tume ilijigawa katika kamati ndogo ndogo ambazo zilitembelea miji mikuu ya

mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Zanzibar ambako ilikutana na wakuu wa idara mbalimbali za Serikali na mahakama, matawi ya wafanyabiashara na kupokea malalamiko na maoni ya wananchi kuhusu tatizo la rushwa mikoani mwao. Maoni haya yamesaidia sana Tume katika kutafakari ukubwa wa tatizo la rushwa nchini na hivyo kuiwezesha kutoa mapendekezo yake.

SHUKRANI

9. Tume inapenda kuwashukuru wananchi wote waliotoa maoni yao ama kwa maandishi au kwa kukutana na Tume, na hivyo kuiwezesha kukamilisha taarifa hii. Aidha shukrani za dhati ziwafike viongozi wote wa Serikali waliojitolea muda wao kutoa maelezo yao kwa Tume, na wote waliosaidia kutayarisha na kufanikisha ziara za Tume mikoani.

10. Tume inapenda kutoa shukrani za pekee kwa maofisa wote wa Sekreterieti, makatibu waendesha ofisi (OMS), mwangalizi wa ofisi, dereva pamoja na wahudumu wote wa Tume ambao wameshirikiana vizuri na Tume katika kufanikisha kazi hii.

SURA YA PILI

HALI YA RUSHWA NCHINI

1. Katika nchi yetu kumekuwepo na onezeko kubwa la woambaji rushwa pamoja na watoaji rushwa. Taifa limeshuhudia pia ongezeko la matumizi ya madaraka kwa manufaa binafsi miongoni mwa watumishi wa umma. Wakati huo huo tabia na vitendo vya kutoheshimu sheria vimeongezeka kwa kasi kubwa.

Aidha, kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya fedha kwa madhumuni ya kupata upendeleo katika huduma ya umma au kupinda na kuvunja sheria au taratibu kwa upande wa raia, hasa wafanyabiashara. Kwa upande wa watumishi wa umma, Tume imeridhika kwamba hali hii imetokana na kuwepo mianya, vishawishi, tamaa, uroho na uduni wa kipato katika utendaji kazi na maisha ya kila siku pamoja na mmomonyoko wa maadili, hususani katika utumishi wa umma na katika jamii kwa ujumla.

2. Hakuna utata kuwa rushwa imeshamiri katika sekta zote za uchumi, huduma na siasa nchini. Kuna ushahidi kuwa hata baadhi ya wafanyakazi wa vyombo vya dola vya Usalama wa Taifa, Polisi, Mahakama na Taasisi ya Kuzuia Rushwa vyenye jukumu la kulinda haki, wametumbukia kwenye vitendo vya rushwa. Hawa badala ya kuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa, wamekuwa sehemu ya tatizo. Matokeo yake raia wa kawaida mpenda haki hana mahali pa kukimbilia. Amebakia kusononeka na kukosa imani na uongozi uliopo.

3. Ongezeko la rushwa katika miaka ya 1990 limechangiwa na mahusiano ya karibu kati ya wanasiasa pamoja na viongozi wengine wakuu serikalini na wafanyabiashara wenye tabia ya kutoa rushwa. Wakati wanasiasa wanafanya maamuzi yaliyozua hisia za rushwa, wafanyabiashara wametumia uhusiano wa karibu uliopo kuendeleza masilahi yao kibiashara. Wakati mwingine maamuzi ya kisiasa yamechukuliwa bila kuzingatia masilahi ya Taifa.

4. Watoaji rushwa wamegawanyika katika makundi mawili. Kwanza, ni kundi la matajiri wanaohonga kushawishi watumishi wa umma wapinde au wavunje sheria, taratibu au kanuni ili kuendeleza masilahi yao. Kundi la pili ni la wale wanaolazimika kutoa hongo kutokana na shinikizo la watoa huduma. Hawa wanajikuta wakilazimika kutoa hongo ili wapate huduma. Hili ni kundi la watu safi, lakini mazingira yanawafanya washawishike kushiriki katika vitendo vya rushwa.

5. Kundi la kwanza la watoaji rushwa ni kundi hatari sana, na vitendo vyao vina athari kubwa katika mfumo wa maamuzi na utendaji kazi katika sekta ya umma. Kutokana na shinikizo lao, mtiririko wa utendaji kazi, haki na malengo ya kitaifa ya kisiasa na kiuchumi hupotoshwa. Kushamiri kwa kundi hili kunaashiria kujengeka kwa tabaka katika jamii na kuzusha mmomonyoko wa mshikamano.

6. Kwa upande wa wapokeaji ambao ni watumishi wa umma wenye mamlaka ya kufanya maamuzi au walio katika nafasi za kuweza kushawishi maamuzi au kutoa huduma, nao pia wamegawanyika katika makundi mawili. Walio katika kundi la kwanza ni wale ambao kupokea kwao rushwa ni matokeo dhahiri ya hali duni kifedha na kimaisha kwa ujumla na wanachopokea husaidia tu kuziba pengo hilo. Aina hii ya rushwa ndiyo inayowakera sana wananchi wa kawaida mijini na vijijini na imeenea katika sekta zote za umma kama ifuatavyo:

ELIMU:

(i) Wazazi kudaiwa rushwa na baadhi ya walimu ili waweze kuwaandikisha watoto wao shuleni na wakati mwingine kwa visingizio kuwa ni michango.

(ii) Walimu hutoa rushwa kwa maofisa elimu wa wilaya, mikoa na wizara ili waweze kupandishwa vyeo.

(iii) Rushwa hutolewa kwa walimu ili kuwawezesha wanafunzi kushinda mitihani ama kwa kuwaongezea maksi, kubadili namba za mitihani au kufanyiwa mitihani na walimu au vijana wa shule za sekondari.

(iv) Rushwa hudaiwa au kutolewa kwa walimu ili kuwawezesha wanafunzi wasiokuwa na uwezo kupata nafasi za masomo ya sekondari na vyuo.

(v) Rushwa hudaiwa na kutolewa kwa maofisa wa Wizara ya Elimu na walimu wakuu ili kuwapatia wanafunzi uhamisho, nafasi ya kurudia darasa.

(vi) Rushwa hutolewa kwa ajili ya upatikanaji wa nafasi ya malazi ya hosteli na mabweni katika shule za sekondari, vyuo na vyuo vikuu.

(vii) Walimu ama kwa ridhaa yao au kwa kudaiwa, hutoa rushwa ili wahamishwe au wasihamishwe sehemu zao za kazi.

(viii) Rushwa hutolewa kwa wale wanaokwenda kusahihisha mitihani ili waongeze maksi za kufaulu mitihani ya watoto waliotahiniwa na hivyo kushinda isivyo halali.

(ix) Wanawake wanaosoma vyuoni na vyuo vikuu hudaiwa na kutoa rushwa ya mapenzi ili waweze kufaulu mitihani yao.

AFYA

(i) Rushwa hudaiwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ambapo wagonjwa au ndugu zao wanalazimishwa kutoa fedha kwa wahudumu, manesi na madaktari ili waweze kupatiwa huduma.

(ii) Rushwa hutolewa ili kukiuka utaratibu uliowekwa makusudi kwa ajili ya kuweza kuwaona madaktari, kupata vitanda katika wodi na wodi za wazazi, kupata madawa, matibabu, huduma za maabara na x-ray, kuwepo katika orodha ya kufanyiwa upasuaji na kupata idhini na fedha za matibabu nje ya nchi.

(iii) Madaktari hutoa rushwa kwa watendaji wakuu ili wahamishwe au wasihamishwe mikoa au hospitali wanazotaka au wasizozitaka.

(iv) Mabwana na mabibi afya wadhibiti wa chanjo ya watu wanaoingia nchini, huomba na kupokea rushwa ili waruhusu au waruhusiwe kukwepa taratibu za afya zinazotawala wanaoingia nchini.

(v) Wahudumu wa vyumba vya maiti hudai na kupokea rushwa kwa kuhifadhi, kuandaa na kutoa maiti.

MAMBO YA NDANI:

Polisi:

(i) Askari wa Usalama Barabarani hulipwa kiasi maalumu kila siku na madereva wa daladala ili wasiwakamate wanapovunja sheria.

(ii) Rushwa hutolewa na madereva kwa polisi wanapopatikana na makosa barabarani.

(iii) Polisi hudai rushwa toka kwa watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu ili wasiwakamate au kuwafungulia mashtaka.

(iv) Polisi huwakamata watu na kuwasingizia makosa ya uongo kama namna ya kushawishi rushwa. Kwa mfano sehemu za mijini watu wanaotoka kutembea usiku husingiziwa makosa ya kuwa na bangi au madawa ya kulevya. Huko vijijini, watu wamekuwa wanafunguliwa makosa ya uongo na mwishowe kudaiwa kutoa kitu chochote kama ng’ombe ili kesi zao zifutwe.

(v) Polisi hupokea rushwa kutoka kwa watu wanaoingia katika viwanja vya michezo, hususan Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwa ajili ya kuona mapambano ya mpira wa miguu badala ya watu hao kulipa viingilio vilivyopangwa na kupewa stakabadhi halali.

(vi) Polisi hupokea rushwa kutoka kwa wahalifu ili wasiwafichue.

(vii) Polisi huwafungulia watu mashtaka mazito ya makosa yenye adhabu kubwa ili watuhumiwa watoe rushwa na hivyo uzito wa mashtaka yao kupunguzwa.

(viii) ‘Public Prosecutors’ wanapokea rushwa ili kuleta mashahidi wa kubabaisha mahakamani.

(ix) Polisi katika vizuizi hupokea rushwa na kuruhusu mazao kutoroshwa kwenda nchi jirani.

(x) Wapelelezi wa Polisi huchelewesha shughuli za upelelezi ili kuwalazimisha wenye kesi kutoa rushwa.

UHAMIAJI:

(i) Maofisa Uhamiaji hudai na kupokea rushwa kutoka kwa raia katika kushughulikia pasi za kusafiria.

(ii) Rushwa hudaiwa na hutolewa kwa maofisa Uhamiaji ili kuwapa uraia, pasi za kusafiria, viza na vibali vya kuishi nchini watu wasiostahili.

MAGEREZA:

(i) Askari Magereza hudai rushwa ili kutoa huduma kwa upendeleo kwa wafungwa na mahabusu. Wenye uwezo wa fedha hupewa chakula kizuri, kazi laini na matandiko mazuri ya kulalia.

FEDHA:

(i) Wahasibu hudai rushwa ili kuidhinisha na kupitisha malipo ya wafanyakazi wenzao.

(ii) Maofisa wa Hazina hudai rushwa ili watoe fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa maofisa wahasibu wa wizara na mikoa.

(iii) Wateja hudaiwa rushwa ili kupata na kurejesha mikopo kutoka mabenki.

(iv) Rushwa hutolewa wakati wa makadirio na malipo ya kodi na ushuru na pengine kusamehewa kodi.

(v) Rushwa hutolewa kwa watendaji wa wizara, idara na mashirika ya umma ili kupata idhini ya malipo baada ya kuwasilisha mali au huduma.

(vi) Wakaguzi wa hesabu hudai rushwa ili kuficha madhambi mbalimbali wanayoyagundua wakati wa ukaguzi.

(vii) Wastaafu na watu walioachishwa kazi hudaiwa rushwa ili waweze kupata malipo yao ya uzeeni.

(viii) Rushwa hutolewa na wateja wasiostahili kulipwa Bima ili hoja zao za ma

(Ripoti tuliyoipata sehemu hii imekatika)

na kupokea rushwa na kuwaachia wavuvi wanaokamatwa wakivua ama waliovua samaki kwa kutumia baruti au madawa kama DDT au nyavu zisizoruhusiwa.

(iv) Rushwa hutolewa kwa maofisa wanyamapori wakati wa kugawa vitalu vya uwindaji.

(v) Maofisa wanyamapori hupokea rushwa ili kutoa Presidential Hunting Licences kwa watu wasiostahili.

Je, unajua ni makundi yapi mengine aliyataja kuwa wala rushwa nchini na mbinu wanazotumia kuchukua rushwa? Wiki ijayo usikose sehemu ya pili ya mfulululizo wa machapisho ya Ripoti ya Rushwa ya Jaji Warioba ya Mwaka 1996 inayochapishwa na Gazeti la JAMHURI pekee, linaloanzia wanapoishia wengine.

VYOMBO VYA HABARI:


(i) Waandishi hupokea rushwa ili kuandika au kutoandika, kutangaza au kutotangaza habari zinazojenga ama kuharibu sifa za mtu au taasisi.

(ii) Baadhi ya maofisa wa vyombo vya habari hupokea rushwa ili kuandika au kutangaza uzuri au ubaya wa vyombo fulani fulani.

NISHATI, MADINI NA MAJI

(i) Wafanyakazi wa Shirika la Ugavi la Umeme (TANESCO), wanadai hongo ili wawaunganishie umeme waombaji wapya.

(ii) Wafanyakazi wa Idara ya Madini hudai hongo kutoa leseni za uchimbaji madini na ugawaji wa maeneo ya kuchimba madini. Wanadai pia hongo ili kutoa thamani ndogo kwa madini yanayosafirishwa nje ya nchi.

(iii) Watumishi wa Idara ya Maji hupokea rushwa ili kutoa upendeleo wa mgawo wa maji mijini.

(iv) Wafanyakazi wa Idara ya Maji mijini wanadai rushwa ili waweze kuunganisha mabomba ya maji ya wateja na bomba la kusambaza maji.

SERIKALI ZA MITAA:


(i) Rushwa hutolewa ili kupata idhini ya maombi ya leseni za biashara kuanzia kwenye ngazi ya kata hadi wilayani.

(ii) Rushwa hutolewa kwa wajumbe wa Baraza la Usuluhishi la Kata ili kutoa upendeleo katika maamuzi kwa upande fulani.

(iii) Watumishi wa halmashauri za miji na wilaya wanadai na kupokea rushwa wakati wa kuajiri, kupandisha vyeo na kutoa madaraka.

(iv) Watumishi wa Serikali za Mitaa hudai na kupokea rushwa ili kutoa huduma mbalimbali kama unyonyaji wa maji machafu, utoaji wa tiba na kadhalika.

(v) Viongozi wa halmashauri za miji na mitaa hudai na hupokea rushwa ili kuidhinisha na kutoa tenda kwa makampuni binafsi.

(vi) Madiwani hupokea hongo ili kuidhinisha ujenzi wa vibanda vya biashara sehemu zisizoruhusiwa na kulinda visibomolewe.

(vii) Mabwana na mabibi afya wa halmashauri za miji hutishia kuwafungia leseni wafanyabiashara na hivyo kupokea rushwa.

1. Kundi la pili la wapokea rushwa ni viongozi na watumishi wa umma wa ngazi za juu ambao kujihusisha kwao katika vitendo vya rushwa ni matokeo ya uroho wa mali na fedha kwa vile hawafanyi hivyo kwa madhumuni ya kukidhi haja za msingi za maisha yao na familia zao (Grand Corruption). Vipato vyao vya kihalali vimetosheleza mahitaji yao na wamekwishajilimbikizia mali na fedha za kutosha.

2. Mbinu ambazo wamekuwa wanatumia kudai na kupokea rushwa ni kama ifuatavyo:

(i) Viongozi wanaopaswa kutoa maamuzi mbalimbali muhimu ya kitaifa, uhongwa na wafanyabiashara ili kufanya maamuzi kulingana na matakwa ya wafanyabiashara hao. Kwa mfano ugawaji wa maeneo ya uwindaji (Hunting Blocks), viwanja katika maeneo nyeti, urejeshaji wa nyumba zilizotaifishwa n.k.

(ii) Viongozi kupeana madaraka ya uenyekiti au ukurugenzi wa bodi za mashirika ya umma kwa upendeleo bila kuzingatia ujuzi, uwezo na masilahi ya taifa.

(iii) Watendaji wakuu hudai na kupokea rushwa ili wakiuke kanuni na taratibu za kutoa zabuni.

(iv) Viongozi wenye mamlaka ya kufanya maamuzi au watendaji wakuu wenye uwezo wa kuathiri maamuzi hutoa misamaha ya kodi mbalimbali kinyume cha sheria baada ya kupokea rushwa.

(v) Watendaji wakuu hudai au hupewa rushwa ili kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kodi.

(vi) Viongozi huingilia shughuli za watendaji wakuu na kufanya maamuzi kama ya kugawa viwanja au maeneo mengine ya ardhi yasiyoruhusiwa kisheria ama kwa upendeleo wa kujuana au baada ya kupokea rushwa.

(vii) Watendaji wakuu huingia katika mikataba na makampuni kwa ajili ya kazi za kitaifa bila kujali masilahi ya taifa.

(viii) Viongozi na watendaji wakuu kugawa maeneo ya uwindaji kutoa vibali vya uvunaji wa misitu, uchimbaji madini pamoja na uvuvi bila ya kuzingatia masilahi ya taifa.

(ix) Wanasiasa hutoa rushwa kwa wajumbe ndani ya vyama vya siasa au katika chaguzi nyingine ama kwa wananchi ili waweze kupigiwa kura ama wananchi waweze kuwapigia kura wagombea wao.

(x) Maofisa watendaji wakuu serikalini na kwenye mashirika ya umma kutojali viwango vya kazi zinazotekelezwa na makampuni walioingia nayo mikataba kutokana na kuwepo kwa vipengele vya rushwa ndani ya mahusiano yao, na hivyo kuwawezesha kupokea kamisheni hasa katika kazi za ujenzi na ununuzi wa vifaa.

(xi) Rushwa katika idara zinazohusika na ugavi wa nafasi za masomo nje ya nchi ambapo mzazi hudaiwa rushwa au mzazi mwenye uwezo hutoa rushwa hata bila kudaiwa ili mwanae apatiwe masomo nje ya nchi.

(xii) Viongozi ndani ya Serikali hupokea rushwa na hutoa siri za Serikali kwa watu wasiostahili ili kuwawezesha kukabiliana na maamuzi na maagizo ya Serikali.

(xiii) Wagombea ubunge kutoa rushwa kwa wapigakura ili wachaguliwe.

(xiv) Wabunge kuwakilisha madai ya uongo kuhusiana na shughuli zao za ubunge.

(xv) Wabunge walio kwenye kamati hukirimiwa, hulipiwa mahali pa kulala na chakula na hupewa fedha na wakuu wa mashirika au idara zinazoshughulikiwa na wabunge hao.

(xvi) Wabunge huwahonga waandishi wa habari ili waandike habari kuwahusu wao.

(xvii) Wabunge hupokea au hudai zawadi wanapotembelea viwanda vya umma na vya binafsi.

3. Tume imeainisha aina nne za vitendo vya rushwa, yaani kuomba na kupokea hongo; kulimbikiza mali kama vile nyumba na magari kwa njia ya rushwa; zawadi zenye sura ya rushwa na upokeaji wa kamisheni baada ya kufanikisha mikataba au ununuzi wa vifaa.

4. Kutokana na picha inayoonekana na kutokana na maelezo ya hapa juu, Tume imetafakari kwa kina namna ya kuandaa mkakati wa kupambana na rushwa. Hata hivyo Tume inaamini kuwa ili kupata ufumbuzi wa kudumu ni muhimu kuangalia sababu zilizolifikisha Taifa kwenye hali hii.

Tume inatambua kuwa Tanzania haikuwa na tatizo la kitaifa la rushwa katika miaka ya 1960. Rushwa imeanza kujitokeza kwa kasi katika miaka ya mwishoni ya 1970 na hatimaye kukithiri katika miaka ya mwishoni ya 1980.

Wakati huo rushwa iliacha kuwa tatizo linalokabili tabaka la wafanyakazi wa umma wa ngazi za chini na kati pekee na kuanza kuwakumba pia wanasiasa na watendaji wakuu serikalini na katika mashirika ya umma.

5. Tume imebaini kuwa sura ya rushwa ya miaka ya 1970 na ile ya miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 ni tofauti, ingawaje sababu zake zinaweza kuwa zile zile.

Ili kukabiliana na rushwa kikamilifu, Tume inaamini kuwa hapana budi kutambua vianzio vya rushwa na kukabiliana navyo kikamilifu. Tume inaamini kuwa ugunduzi wa kiini cha ugonjwa ni hatua kubwa ya kupata dawa ya kuponyesha au kuzuia.

RUSHWA KUANZIA MIAKA YA 1970

6. Matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyolikumba Taifa mwishoni mwa miaka ya 1970 yalisababisha Serikali ichukue hatua mbalimbali za kisiasa, kisheria na kiuchumi katika jitihada ya kukabiliana na hali hiyo.

Kodi zilipanda, sera ya biashara ya ndani ilitoa ukiritimba kwa mashirika ya biashara ya umma katika uuzaji wa bidhaa adimu na muhimu; vizuizi vingi viliwekwa katika maisha ya kila siku ya raia kama vile vizuizi barabarani ili kuratibu usafirishaji wa mazao, uzuiaji kuendesha magari Jumapili mchana na kadhalika.

Mfumo wa vibali uliibuka bila utaratibu wa usimamizi na udhibiti unaoeleweka. Wakati huo huo gharama za maisha zilipanda kwa kasi kuliko ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma. Miiko ya uogozi iliwazuia watumishi wa umma kupata kipato cha ziada kutokana na biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Kwa jumla baadhi ya watumishi wa umma na viongozi walianza kubuni mbinu za kupata mapato ya nyongeza ili kukidhi maisha yao. Mara nyingi baadhi ya mapato hayo ya nyongeza yalikuwa haramu.

7. Tume imefanya tathmini kuhusu tatizo la rushwa nchini na kubaini kuwa rushwa katika miaka ya 1970 ilitokana na mambo yafuatayo:

(i) Matatizo ya utekelezaji wa sheria na kanuni

Kuwepo kwa sheria na kanuni zilizo ngumu kutekelezwa na kusimamiwa. Kwa mfano sheria ya uzuiaji milki ya magari (Motor Vehicles Restriction or Acquisition Act), Road Toll na ile ya kuzuia uendeshaji wa magari Jumapili na vizuizi vya barabarani hazikuwa rahisi kutekelezwa kutokana na ukosefu wa nyenzo za kusimamia. Matokeo yake zilitoa mianya ya rushwa.

(ii) Utovu wa usimamizi na uwajibikaji

Tafsiri potofu ya Ibara ya 15 ya Mwongozo wa TANU wa 1971 ilisababisha viongozi kulegeza usimamizi katika sehemu zao za kazi kwa hofu ya kuitwa wanyapara na kupoteza nafasi zao. Matokeo yake yalikuwa watumishi wabovu kuweza kutumia nafasi zao kazini kwa kujinufaisha binafsi. Wakati huo huo utamaduni wa uwajibikaji ulidorora na kusababisha mambo yaende kiholela. Hali hii ilitoa mianya ya rushwa.

(iii) Taratibu ndefu na ngumu

Ili kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, Serikali iliweka taratibu kadhaa ambazo zilikuwa ni ndefu na ngumu. Kwa mfano, utaratibu wa kumiliki gari ulihitaji kibali ambacho kilipitia kwenye mkondo mrefu.

Vile vile kipindi hiki kilishuhudia uongezekaji wa urasimu katika kutoa mizigo bandarini na kupata leseni za biashara. Binadamu kwa ujumla hapendi usumbufu. Usumbufu huo ulitoa mianya kwa watumishi wa umma kutumia nafasi zao kudai hongo. Pia uliwashawishi raia waliokuwa wakihitaji huduma kutoa hongo.

(iv) Uadimu wa bidhaa muhimu

Mwishoni mwa miaka ya 1970 taifa lilishuhudia upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu (Consumer goods). Wakati huo huo, ukiritimba uliotolewa kwa makampuni ya umma ya biashara uliwapa viongozi wa mashirika hayo mamlaka makubwa ya uamuzi.

Kutokana na upungufu wa bidhaa hizo pamoja na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya raia, mianya mingi ya rushwa ilijitokeza kwa viongozi wa mashirika hayo kupata chochote na upungufu huo uliwachochea raia wenye uwezo kuhonga ili wapate bidhaa hiyo.

(v) Mishahara midogo na upandaji wa kasi wa gharama ya maisha

Kama ilivyokwishaelezwa mwishoni mwa miaka ya 1970, mtumishi wa umma kwa mara ya kwanza alijikuta anashindwa kuishi kwa kutegemea kipato chake cha mshahara kutokana na upandaji wa gharama za maisha.

Hali hii iliwafanya watumishi wengi kutafuta mbinu za kupata kipato cha ziada ili kumudu maisha. Wengine walianzisha miradi halali kama ya ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa. Lakini wapo waliotumia nafasi zao za kazi kupata kipato cha ziada nje ya utaratibu wa haki na sheria.

(vi) Ukosefu wa uhakika wa usalama wa ajira

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Taifa mwaka 1975, Serikali ilipunguza asilimia 10 ya watumishi wake. Kazi hii iliendelea mwaka 1985, 1992/93, 1994/95 na 1995/96. Vigezo vilivyowekwa kutumiwa katika kazi hiyo havikufuatwa kikamilifu.

Matokeo ya kazi hii ni kwa baadhi ya watumishi hodari na wasio na dosari kukumbuwa na zoezi hilo na wengine wabovu kubakia kazini. Hali hii ilizaa wasiwasi wa kutojiamini miongoni mwa watumishi wa serikali. Hofu hii lichangiwa kwa baadhi yao kuamua watumie nafasi zao kudai na kupokea hongo ili kujikinga na hatma isiyotabirika.

(vii) Kukosekana kwa dhamiri ya kisiasa

Moja ya sababu za kushamiri kwa rushwa nchini ilikuwa ni kukosekana kwa dhamiri ya kisiasa. Rushwa ilianza kujadiliwa kwa nguvu sana tangu wakati wa ‘wahujumu uchumi’ na mjadala huo kuhitimishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM cha mwaka 1989, ambacho kilijadili taarifa mbalimbali kutoka taasisi za umma, chama, Serikali na taasisi za dini.

Matokeo ya mjadala huo ni taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya CCM – Dodoma iitwayo ‘Muhtasari wa Taarifa ya Uchambuzi wa Mikakati na Mbinu za Kupambana na Rushwa Nchini.’ Matarajio ya mjadala huo yalikuwa ni kwamba mbali na viongozi wa kisiasa kuendelea kukemea rushwa, maamuzi na maagizo ya CCM yangeliingizwa katika mpango wa Serikali ili iandalie taratibu za kiutawala za kudhibiti rushwa.

Hakuna ushahidi kuwa maamuzi hayo yaliwasilishwa serikalini na Serikali kuyatolea maelekezo ya utekelezaji. Kwa hiyo maamuzi ya chama hayakuwa na nguvu ya kiserikali au ya kisheria kuwashinikiza watendaji wakuu serikalini kuyatekeleza.

Wakati viongozi wa juu wa taifa waliendelea kukemea rushwa, hakuna hatua zilizowekwa sambamba kwa watendaji wakuu wote kuwa viongozi wa kuondoa rushwa katika maeneo yao ya kazi. Vita hivi havikuwa vya wote jambo ambalo lilichochea kasi ya kuenea kwa rushwa nchini.

(viii) Udhaifu wa vyombo vya dola

Vyombo vya dola vimeongeza kushamiri kwa rushwa kutokana na sababu mbili; udhaifu wa ndani ya vyombo hivyo vyenyewe na kujihusisha na rushwa na ubadhirifu.

Mahakama za mwanzo na polisi ambazo ziko karibu na wananchi ndizo zenye tuhuma nyingi za rushwa na utovu wa maadili, hekima na uadilifu. Aidha, iko tabia ya kulindana miongoni mwa baadhi ya mahakimu na polisi wanapokabiliwa na tuhuma za rushwa.

Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Usalama wa Taifa vyote vinakabiliwa na matatizo ya vitendea kazi. Aidha, baadhi ya watumishi wa vyombo hivi wametumbukia katika baa hili na hivyo kufanya zoezi zima la kukabiliana na rushwa kuwa gumu.

8. Ingawa rushwa imeanza kuonekana wazi katika jamii ya Watanzania katika miaka ya 1970, hata hivyo rushwa hiyo iliwahusu wafanyakazi wa tabaka la chini na la kati (Low-level corruption). Hawa walidai na kupokea rushwa kukidhi mahitaji yao. Katika kipindi hicho viongozi wengi wa ngazi za juu walikuwa ni watu safi, wenye tamaa za kawaida na hawakujihusisha katika vitendo vya rushwa.

9. Mwanzoni mwa 1983 Serikali iliendesha msako wa wahujumu uchumi nchi nzima. Miongoni mwa malengo ya kampeni dhidi ya wajuhumu uchumi ilikuwa ni kupambana na watoa na wapokea rushwa. Pamoja na kwamba kampeni hiyo ilifanyika kwa kishindo kikubwa na watuhumiwa wengi kukamatwa na kuzuiliwa, vita hivyo havikufanikiwa.

Hii ilitokana na ukweli kwamba kampeni hiyo ililenga kwenye matukio na si kwenye viini vya tatizo. Hata hivyo, mafunzo yaliyotokana na zoezi hilo yalisababisha Serikali kubadili sera ya biashara ya ndani na kulegeza masharti ya biashara. Watu wenye fedha nje ya nchi waliruhusiwa kuagiza na kuingiza nchini bidhaa na kwa hivyo kupunguza rushwa iliyokuwa imeshamiri katika nyanja ya biashara iliyokuwa imeshikiliwa na mashirika ya umma.

10. Baada ya 1985 sura mpya ya rushwa ilianza kuonekana. Baada ya kulegeza masharti ya biashara ya ndani, misingi muhimu ya kisiasa na kijamii iliyotawala maisha ya raia, hasa watumishi wa umma ilianza pia kulegezwa. Sambamba na mabadiliko haya, rushwa ilianza kunyemelea ngazi za uongozi. Kufikia miaka ya mwanzoni mwa 90 rushwa ilishamiri ndani ya tabaka la uongozi wa juu (High-level corruption). Tatizo hili lilitokana na mambo yafuatayo:

(i) Kuwepo kwa fedha nyingi katika uchumi

Nyongeza kubwa iliyoletwa na ukuaji wa biashara baada ya ulegezaji wa masharti ya biashara, ilisababisha kuwepo kwa wingi wa fedha kwenye mikono ya wachache na ambayo iliwapa matajiri hao tamaa ya kununua haki ambayo hawakustahili. Hii ilikuwa ni pamoja na ukwepaji wa kodi, ulanguzi, ulaghai wa ardhi, biashara haramu kama ya madawa ya kulevya na uingizaji wa bidhaa zenye ubora hafifu. Viongozi wachache walishawishiwa na wenye fedha na kukubali kutimiza tamaa hizi.

(ii) Ukaribu wa wafanyabiashara na viongozi

Mwanzoni mwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Pili, viongozi wa kisiasa walijenga uhusiano wa karibu sana na wafanyabiashara, hasa wenye asili ya Kiasia. Baadhi ya wafanyabiashara hao walishiriki katika tafrija mbalimbali zilizohudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kununua picha, saa au kalamu za viongozi hao na hata mikufu, vidani na hereni za wake zao.

Kwa kufanya hivyo walipiga picha pamoja na viongozi. Hawa walizitundika picha hizo madukani na maofisini mwao na kuonyesha jinsi walivyo karibu na viongozi katika jumuiya zao. Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa karibu na viongozi walikusanya pesa kwa madai kuwa walikuwa wakiwapelekea viongozi.

Ukaribu uliojitokeza baina ya viongozi na wafanyabiashara ulisababisha viongozi waingilie shughuli za watendaji na kufanya maamuzi kuwasaidia baadhi ya wafanyabiashara. Baadhi ya maamuzi hayakufanywa kwa kuzingatia masilahi ya taifa, bali kwa manufaa yao binafsi na wafanyabiashara hao. Hali hii ilidhihirisha wazi ni jinsi gani viongozi walikuwa wamejitumbukiza katika vitendo vya rushwa, jambo ambalo lilichochea zaidi ongezeko la rushwa nchini.
V: WAJIBU WA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI

1. Umma wa Tanzania umekuwa unakerwa sana na kuenea kwa rushwa nchini, hasa ile inayodaiwa na watumishi wa umma katika ngazi za chini kutokana na hali ngumu ya maisha. Rushwa ya aina hii imeufikisha umma pahala pagumu kiasi kwamba umeshawishika kukata tamaa ya kupata haki yoyote ile bila ya kutoa rushwa.

Kwa mfano wazazi huko vijijini wamekwishajenga imani kwamba hawawezi kufanikiwa kuwaandikisha watoto wao shuleni bila ya kuwa na fedha mfukoni, hawawezi kupata haki katika vyombo vya dola na mahakama bila ya kuwa na fedha za kuhonga n.k.

Umma umefikia uamuzi huu potofu kutokana na mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza ni kwamba wananchi wengi hasa wa vijijini bado hawajafahamu haki zao kikatiba. Rushwa inahusu watoaji (wananchi wanaohitaji huduma), na wapokeaji (watu wenye dhamana katika Serikali na mashirikaya umma).

Kama wananchi kwa ujumla wataelewa vizuri haki zao na hivyo kukataa kuzinunua kwa kutoa rushwa ni dhahiri kwamba itatoweka yenyewe. Wananchi wanatakiwa kuelimishwa kuhusu haki zao ili waweze kuzidai pale ambapo wataona kuwa wanadhulumiwa au kucheleweshwa.

Hapa ndipo umuhimu wa vyombo vya habari unachukua nafasi na wajibu wa kipekee kwa umma. Vyombo hivi vina uwezo wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao katika jamii. Aidha, kwa kuwa vinaelewa vizuri maadili ya taifa na vina utaalamu wa kufanya uchunguzi, vitaweza kusaidia kuwafichua wale wote wanaokiuka maadili kwa kudai na kupokea rushwa. Taarifa zao zikiwa za kweli itakuwa rahisi kwa uongozi wa taifa kumuwajibisha kiongozi atakayehusika.

2. Jambo la pili ambalo ni baya zaidi, ni kwamba hata kama umma utapata mwamko kuhusu haki zao na hivyo kukataa kuzinunua na badala yake kuwafichua wale wote wanaoomba rushwa, umeelekea kukata tamaa baada ya kuona kwamba uongozi ambao ulikuwa unaamini kwamba ungelikuwa kimbilio lao umetumbukia katika baa la rushwa.

Umma wa Tanzania unashindwa kuwafichua wale wote wenye kudai na kupokea rushwa kutokana na ukosefu wa uongozi safi na wenye kuwajibika ndani ya vyombo vya dola kama polisi, mahakama, Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Usalama wa Taifa.

Kwa hiyo kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kusafisha safu ya uongozi uliopo katika Serikali yenyewe, mashirika ya umma pamoja na vyama vya siasa. Baada ya hapo itabidi kuchukua hatua za kujenga uongozi wenye nia ya dhati ya kupambana na adui rushwa katika ngazi zote kwa kuwachukulia hatua wale wote watakaofichuliwa. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumerudisha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na hivyo kuchochea kasi ya kufuta rushwa nchini.

VI: WAJIBU WA UONGOZI WA JUU

3. Tumekwisha kuonyesha umuhimu wa kusafisha safu za juu za uongozi. Ili kazi hii ya kupiga vita rushwa iendelee kwa kasi, Rais hana budi kuonyesha njia.

4. Watanzania ni waelewa sana na wamechoshwa na ubadhirifu wa wale wanaowaongoza. Wanangojea kuona hatua madhubuti ili wamsaidie Rais na Serikali yake kuondokana na rushwa.

5. Tume inapendekeza kwamba pamoja na umuhimu wa kusafisha ngazi za juu za uongozi, Rais awaagize viongozi wapya wanaoteuliwa kuongoza vyombo vya dola kusafisha safu za wasaidizi wao. Atakayeshindwa kufanya hivyo na kashfa zikajitokeza mahali pake pa kazi, awajibike bila msamaha na asihamishiwe sehemu nyingine. Pia vyombo hivyo, hususan Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa vijenge mshikamano katika kupambana na rushwa.

SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI YA 1995

6. Ibara ya 132(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunda Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ibara hii pia inaipa sekretarieti hiyo uwezo wa kupeleleza mienendo na tabia za viongozi wa umma kwa madhumuni ya kuona kama inazingatia na masharti ya uongozi yaliyowekwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya 1995, Sheria Na. 13 ya 1995.

VIONGOZI WA UMMA

7. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeorodhesha viongozi wanaohusika na masharti ya sheria katika kifungu cha 4 cha sheria hiyo na imewagawa katika makundi sita kama ifuatavyo:

(a) Wanasiasa.

(b) Watendaji wakuu wa wizara na idara za Serikali na wa Serikali za Mitaa.

(c) Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

(d) Watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

(e) Majaji na mahakimu.

(f) Wajumbe wa kudumu wa tume mbalimbali.

Viongozi wa umma wanatofautiana kuhusu:

(a) Aina ya majukumu au wajibu walionao.

(b) Masharti ya kazi.

(c) Mamlaka na taratibu za kuwapa nyadhifa na kuwaondoa madarakani.

28. Viongozi wa kisiasa wamegawanyika katika makundi mawili. Wale wa kuteuliwa na Rais na wale wanaochaguliwa kwa uchaguzi na kuondoka madarakani pindi kipindi chao kinapomalizika. Hawa hawana masharti au mamlaka yanayosimamia mienendo yao. Wale wa kuteuliwa wanaweza kuondolewa madarakani wakati wowote. Aidha, viongozi wa kisiasa hawana mamlaka au taratibu nyingine zinazosimamia mwenendo wao na nidhamu kazini isipokuwa masharti ya uteuzi na maelekezo ya Rais.

29. Watendaji wakuu wa wizara au idara za Serikali ni watumishi wa Serikali wanaoteuliwa na Rais. Hawa hutawaliwa na kanuni za kudumu za Serikali (Standing Orders) pamoja na sheria ya utumishi serikalini. Sheria na kanuni hizo ndizo zinazoweka masharti ya uteuzi, mwenendo na nidhamu ya watumishi hao.

30. Viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama huteuliwa na Rais na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza shughuli za vyombo hivyo. Jeshi la Ulinzi linatawaliwa na sheria ya Jeshi la Wananchi ya 1966 (Na.32/66).

Sheria hiyo inaweka masharti ya nidhamu ya askari, maofisini na utekelezaji wake. Askari na maofisa wote wa Jeshi la Ulinzi wanapaswa kuheshimu sheria hiyo, vile vile wakuu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza husimamiwa na sheria zinazotawala vyombo vyao. Sheria hizi zimeweka kanuni zinazotawala mienendo na taratibu za viongozi na maofisa wa vyombo hivyo.

31. Viongozi wa mashirika ya umma huteuliwa na Rais. Watendaji wakuu wengine huteuliwa na bodi. Watendaji hao hufanya kazi chini ya usimamizi wa bodi za mashirika yao. Bodi hizo zinayo mamlaka ya kusimamia masuala ya utendaji kazi na nidhamu. Aidha, bodi za mashirika zina uwezo wa kudhibiti ukiukaji wa masharti na miiko ya kazi na kuwaondoa au kupendekeza kuwaondoa katika madaraka yao watendaji hao wanaokiuka masharti na maadili ya kazi.

32. Majaji huteuliwa na Rais kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Majaji na mahakimu hutawaliwa na Sheria ya Utumishi wa Mahakama. Majaji hawawezi kuondolewa kazini isipokuwa kwa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi iliyoteuliwa na kufanya uchaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 110 ya Katiba. Aidha, majaji na mahakimu wamejiwekea wenyewe kanuni za maadili ya maofisa wa mahakama ya 1984.

33. Wajumbe wa tume mbalimbali huteuliwa na Rais na kutenda kazi zao kwa mujibu wa masharti ya uteuzi na sheria zinazoainisha tume hizo au kuweka majukumu yake.

34. Kutokana na mchanganuo wa aina ya viongozi uliofanywa hapa juu kwa kuzingatia aina ya kazi na wajibu, masharti na taratibu za utekelezaji wa kazi zao, watu waliotajwa na sheria kuwa ni “viongozi wa umma” wanatofautiana kwa kila hali isipokuwa tu kwamba kazi wanazozifanya ni za umma (public duties).

35. Tume imetambua umuhimu wa kuwepo maadili kutawala mienendo, tabia na utendaji kazi wa watumishi wa umma. Tume imetambua umuhimu wa kuwepo maadili kutawala mienendo, tabia na utendaji kazi wa watumishi wa umma.

Aidha, Tume inatambua kuwa maadili ni kanuni muhimu zilizowekwa au kukubaliwa na kikundi cha watu, ambazo zinaainisha mambo yanayokubalika au yasiyokubalika katika kikundi hicho au katika mahusiano au shughuli miongoni mwa wanachama au wahusika wa kikundi hicho.

Kanuni hizo huwa ndicho kioo cha watu walio nje ya kikundi cha kukitazama au kukipima kikundi kinachohusika na maadili hayo.

36. Watumishi katika utumishi wa serikali, viongozi wa majeshi ya ulinzi, majaji na mahakimu na watendaji wakuu wa mashirika ya umma wanatawaliwa na kanuni ambazo zipo kudhibiti mienendo, tabia na utendaji wao wa kazi.

Sheria ya maadili inawagusa pia viongozi wote ambao ajira yao inatawaliwa na sheria hizo. Tume inaliona jambo hili la viongozi kutawaliwa na sheria mbili zenye utaratibu tofauti kama linaweza kuleta utata katika utekelezaji na kutosimamia vizuri madhumuni ya sheria ya maadili au hizo sheria na kanuni nyingine.

Tume inapendekeza kwamba viongozi wa umma ambao ajira na mienendo yao inatawaliwa na sheria tofauti na sheria ya maadili, waondolewe kwenye orodha iliyotajwa kwenye sheria ya maadili na waendelee kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotawala ajira yao.

37. Kama viongozi wa umma ambao ajira zao zinatawaliwa na sheria nyingine wataondolewa kwenye sheria ya maadili, viongozi wa umma watakaobaki ni viongozi wa kisiasa. Tume inaridhika kwamba utaratibu huu utarahisisha utekelezaji wa sheria ya maadili kwa viongozi hao.

Tume imebaini kwamba sheria na kanuni zinazotawala ajira za viongozi wa umma wasio wanasiasa, zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili misingi iliyomo kwenye sheria ya maadili iwekwe kwenye sheria na kanuni zinazotawala ajira na nidhamu ya viongozi hao.

38. Orodha ya viongozi wa umma watakaoainishwa kwenye sheria ya maadili iwajumuishe wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Spika wa baraza hilo ambao hawamo kwenye orodha hiyo.

AINA YA MAADILI

39. Kifungu cha 4 cha Sheria kinafafanua neno “Code” kuwa ni kanuni za maadili ya viongozi wa umma yaliyowekwa na au kwa mujibu wa Sheria ya Maadili. Kwa mantiki hiyo kuna maadili ya aina mbili; kwanza ni maadili yaliyowekwa na sheria yenyewe na pili ni maadili yatakayowekwa baadaye kwa mujibu wa sheria hiyo.

Kwa kuwa maadili ni lazima yazingatiwe na wanaohusika na adhabu itolewe kwa ukiukwaji wake, sharti maadili hayo yawe dhahiri na bayana ili wahusika wayafahamu.

40. Ibara ya 132(4) inalipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria itakayoainisha misingi ya maadili ya viongozi wa umma itakayozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za madaraka zitakazotajwa na Bunge. Misingi ya maadili imefafanuliwa katika Ibara ndogo ya (5).

Vile vile Katiba imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria kuweka masharti ya watu kufukuzwa au kuondolewa kazini kwa makosa ya kuvunja maadili ya viongozi. Sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hii ni Sheria ya Maadili tunayoifafanua.

Sheria hii inampa Rais, katika sehemu ya pili, mamlaka ya kuweka maadili kwa shabaha ya kujenga imani ya wananchi kwa uadilifu wa viongozi wao. Tume imeyatafakari mamlaka aliyopewa Rais na inaona kwamba haikuwa, lazima kwa Rais kupewa mamlaka hayo.

Mamlaka hayo ni ya Bunge kama yalivyoelezwa kwenye Katiba. Rais atabaki na mamlaka ya kuhakikisha kwamba Serikali inaongozwa na viongozi wa umma anaowateua yeye na wale ambao ajira yao kwenye utumishi wa Serikali wanakuwa na maadili. Maadili hayo si lazima yatungiwe sheria tofauti na zile zinazotawala ajira hizo.

41. Pamoja na maoni yaliyo hapo juu, sheria kama ilivyotungwa ina kasoro na upungufu unaoifanya isikidhi madhumuni ya kuitunga. Kasoro na upungufu huo ni kama ifuatavyo:

(a) Kifungu cha 5 cha sheria kinampa Rais wajibu wa “to work towards the evolution of ethical standards designed to provide a basis for enhancing public confidence in the integrity of public leaders and in the decision-making process in the government.” Aidha, kifungu hiki kinaorodhesha mambo manne yatakayomuongoza Rais katika kuweka kuweka kanuni za maadili ambayo ni:

(i) Mgongano kati ya masilahi ya umma na ya binafsi katika utekelezaji wa shughuli za kiongozi wa umma;

(ii) Kuvutia na kutoa nafasi kwa watu wote wenye uwezo toka nyanja zote kukubali nafasi za utumishi wa umma;

(iii) Kuweka kanuni za kusimamia mgongano wa masilahi ya umma na ya binafsi, hata baada ya kiongozi wa umma kutoka madarakani;

(iv) Kupunguza fursa za kutokea mgongano wa masilahi ya binafsi na ya umma na kutatua migongano hiyo kwa njia ambayo itazingatia zaidi kuhifadhi masilahi ya umma.

(b) Kifungu cha 6 kinaorodhesha misingi itakayotumika kama vigezo vya utungaji wa kanuni za maadili ya viongozi yatakayowekwa. Kifungu cha 7 kinampa Rais madaraka ya kuweka kanuni za maadili.

Tume inaona kwamba vifungu vya 5, 6 na 7 vya Sheria ya Maadili havieleweki na havina ufasaha unaotakiwa katika sheria. Kifungu cha 5 kinampa Rais jukumu la “to work towards the evolution of ethical standards.”

Sheria haitamki namna Rais atakavyotekeleza hilo na hali hii inasababisha uwepo ugumu wa kupima kama jukumu hilo limetekelezwa au Rais analitekeleza kwa ufanisi na kiwango gani.

Aidha, kipengele cha (2) cha kifungu cha 5 cha sheria kinamtaka Rais aongozwe na “the need to evolve, and foster, sound rules and ethical standards in the public service” wakati anapoyatekeleza majukumu manne yaliyoorodheshwa katika kifungu kidogo hiki.

Kwanza haieleweki kuna tofauti gani au inakusudiwa nini wakati kifungu kidogo (1) cha kifungu cha 5 kinamtaka Rais “to work towards the evolution of ethical standards” na kifungu kidogo cha (2) kinamtaka Rais aongozwe na “the need to evolve and to foster sound rules and ethical standards.”

Pili haieleweki kama mambo yaliyoorodheshwa katika kifungu kidogo cha (2) ndiyo maadili yenyewe au ni mwongozo tu ambao Rais ataufuata katika kuweka maadili, au kama ni vigezo vya maadili yatakayowekwa.

(c ) Mkanganyiko wa aina hii unaonekana pia katika kifungu cha 6 ambacho kinaorodhesha misingi itakayotumika katika maadili (“Principles to be invoked by the code”), wakati ibara ya 135(5) ya Katiba nayo inaweka “Misingi ya Maadili ya Viongozi.”

Aidha, haileweki kama mamlaka ya Rais chini ya kifungu cha 7 ya “declare requirements and rules regarding ethical standards,” ni jambo lile lile au tofauti na “to establish a code of ethics under the Act” ilivyokusudiwa katika ainisho la neno “code.”

42. Kutokana na mkanganyiko unaojitokeza Tume imeridhika kuwa sehemu ya pili ya sheria hii haiweki bayana suala la maadili ya viongozi yanayokusudiwa yawekwe na Rais.

43. Tume inaona kuwa hitilafu hii ni upungufu mkubwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi, upungufu ambao utaathiri utekelezaji wa sheria ya udhibiti wa tabia na mienendo ya viongozi.

44. Kutokana na kasoro zilizojitokeza Tume inapendekeza sheria ifanyiwe marekebisho kuzingatia yafuatayo:

(a) Maadili yote yanayostahili yaorosheshwe kwenye sheria na hali ikihitaji Bunge liweze kuongeza orodha ya maadili hayo kwa kupitisha maazimio;

(b) Adhabu ya ukiukwaji wa maadili iwekwe bayana na mojawapo ya adhabu iwe ni kiongozi kuondolewa madarakani au kupoteza sifa ya kushika uongozi;

(c) Sheria itamke kuwa kiongozi atakayekabiliwa na tuhuma nzito na za wazi atajiuzulu au ataomba kujiuzulu.

MAADILI YA VIONGOZI WOTE

45. Sehemu ya tatu ya sheria inazungumzia maadili ya viongozi wote (Code of Ethics applicable to all public leaders). Aina ya maadili zilizowekwa kwenye sheria ni kama ifuatavyo:

(a) Hatua za kiongozi kuwasilisha kwa Kamishna wa Maadili tamko la mali na madeni yake binafsi, ya mke wake na ya mtoto wake ambaye hajaoa au kuolewa na mwenye umri wa chini ya miaka 18;

(b) Ni kosa kwa kiongozi wa umma, hali akijua, kujipatia masilahi makubwa ya kifedha kwa njia zisizo halali au kumsaidia mtu mwingine kujipatia masilahi kama hayo;

(c) Kiongozi wa umma haruhusiwi kuzungumza kwenye kikao bila kutoa taarifa kwenye kikao hicho, kuhusu masilahi aliyonayo ya kifedha katika jambo linalojadiliwa na kikao hicho;

(d) Kiongozi wa umma anahitajiwa kutoa tamko la masilahi yoyote aliyonayo katika kondrasi ya serikali.

46. Sharti la kiongozi kutangaza mali zake limewekewa vikwazo kiasi kwamba, shabaha ya sharti hilo haieleweki. Vikwazo hivyo vinatokana na mambo yafuatayo:

(a) Kutenganisha mali inayotakiwa kutangazwa (declarable assets) na mali isiyotakiwa kutangazwa (non-declarable assets),

(b) Kujumuisha katika mali isiyotakiwa kutangazwa mali kama nyumba ya kuishi, vyombo vya burudani na mashamba ya familia, vitu vya sanaa na magari na vyombo vingine vya usafiri binafsi, pamoja na fedha itokanayo na mashamba au shughuli binafsi za kiongozi, akiba na mikopo kutoka kwa mwajiri na jamaa zake,

(c) Kuweka sharti katika kifungu cha 10 kuwa mali na masilahi ya viongozi wa umma na familia zao na mali ambayo si ya kibiashara haihitajiki kutangazwa.

47. Tume ina maoni kuwa kigezo cha “mali isiyohitajika kutangazwa” kilichowekwa na sheria kinapingana na misingi ya madhumuni ya maadili. Kitendo cha kutenganisha mali katika mafungu ya mali inayotakiwa na isiyotakiwa kutangazwa inapingana na kudhoofisha madhumuni ya Sheria ya Maadili.

Kifungu cha 6(6) kinamhitaji kiongozi wa umma kutekeleza na kuendesha shughuli iliyowekwa na kifungu hicho kwamba kiongozi wa umma anatakiwa atekeleze kazi zake na kuendesha shughuli zake za binafsi kwa hali ambayo itaruhusu au kuwezesha shughuli hizo kuwa wazi mbele ya macho ya wananchi.

Kama kiongozi ana nyumba ya kuishi au kupangisha, magari na mashamba ni vema wananchi wakajua anavyo na jinsi alivyovipata. Aidha, kama mali ni ya mwenzi wa ndoa au mtoto wa kiongozi ni vema ifahamike wazi ili kiongozi, mwenzi wake wa ndoa au watoto wasituhumiwe kwa kujipatia mali kwa kutumia nafasi za kiongozi.

48. Baada ya kuridhika kwamba vifungu vyote vinavyoweka vikwazo vya kutangaza mali zote na mienendo ya viongozi vinadhoofisha madhumuni ya sheria hii. Tume inapendekeza kwamba vifungu vya 9, 10 na 11 vifutwe ili kuweka sharti la lazima kwa viongozi wa umma kutangaza mali zao bila vipingamizi vilivyomo kwenye sheria ya sasa. Hatua hii itaifanya sheria kuyaweka maadili katika watumishi wa umma wazi.

49. Tume inaliona sharti la kiongozi kutojipatia masilahi makubwa ya kifedha kwa njia zisizofaa katika kifungu cha 12 nalo lina vipingamizi visivyo vya lazima:

Kwanza, maneno “significant percuniary advantage” yaliyomo kwenye sheria hayatoi maana bayana ni kitu gani hasa kinachokusudiwa, jambo ambalo litafanya utekelezaji wa sharti hili kuwa mgumu; Tume inapendekeza neno “significant” liondolewe kwenye sheria;

Pili, kiongozi anaweza kujipatia masilahi mengine ambayo siyo ya kifedha (pecuniary), kwa kufanya mambo yaleyale yaliyotajwa katika kifungu hiki. Kwa mfano anaweza kujipatia nyumba ya kuishi, magari shamba, kazi kwa jamaa zake na kadhalika mambo ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 9 ni “non-declarable assets.”