[update] Shukurani ya watoto wa Faraja House kwa wote waliosaidia baada moto kuunguza makazi yetu
SHUKURANI

Kituo/Makao Faraja House ni mahali pa kusaidai na kulea "Watoto wenye kuishi katika mazingira hatarishi". Wapo 72 (saba wasichana): 46 wanaosoma shule ya msingi na 25 wa sekondari. Wapo wakubwa wanaoendelea kusaidiwa kuendelea na masomo ya Chuo Kikuu.

Jumanne saa 11 jioni ya tarehe 7 Julai 2016, tulikumbwa na janga la moto kwenye nyumba za Faraja.Nyumbani walikuwemo vijana wachache wa sekondari. Watoto wengi walikuwa likizoni kwa walezi nyumbani kwao. Watoto 19 waliokuwa wamebaki tulikuwa tumeondona nao saa nane kwenda kutembelea "Magic Site" mjini Iringa.

Tunafikiri kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme ambao ulishika kwenye dari za mbao. Kuwepo kwa upepo mkali huenda kulisambaza moto huo na kusababisha uvume kwa nguvu na haraka. Mitungi 9 ya "zima moto" tuliyokuwa nayo haikusaidia kwani mingine ikishindwa kabisa kufanya kazi.

Tunawashukuru wanakijiji, hasa wakina mama walioonyesha moyo wa kipekee kwa kufika na kuchota maji na kujaribu kuzima moto na kuokoa baadhi ya vifaa.

Hakuna yeyote aliyeumia, iwe ni watoto au watu waliojitokeza kusaidia.

Kwa sasa, watoto wanaishi kwenye bweni na majengo mengine ya Chuo cha Ufundi.

Tunatoa shukurani zetu kwa wote waliotutembelea na kutujali kwa mahitaji mbalimbali, wakiwemo viongozi wengi sana wa mkoa (akiwemo Mkuu wa Mkoa), Mheshimiwa Mbunge, Mkuu wa Wilaya na staff nzima, Ustawi wa Jamii, Polisi, Magereza, Madiwani, Walimu na viongozi wengi sana wa mashirika au taasisi za serikali na binafsi. Watu wengi sana, marafiki na familia nzima, wote walikuja na misaada ya aina mbalimbali kama vile magodoro, mablanketi, nguo, sabuni, vyakula, vifaa vya hsule, fedha n.k.

Tumeonja urafiki, ushirikiano na undugu. Nani ataweza kuwahesabu wote? Mungu anajua na sala za watoto hawa wanaosaidiwa zitamwambia Mwenyezi awarudishie mema mengi.

Katika shirika letu la Consolata imeanzishwa "solidarity fund" na tunajua inaendelea kwa kiasi sana na kudhihirisha Huruma ya Mungu na karama zetu.

Asante ni neno tu lakini likitoka moyoni mwa Watoto hawa lina nguvu na maana ya 'Kimungu'. Sisi sote pamoja na tunaendelea kuwa na ukumbusho na sala kwa ajili yenu.

Asante.
Viongozi wote wa Kituo