Taarifa ya awali ya zoezi la uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu

Picha iliyopigwa hivi karibuni Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) wakati wanafunzi wakihakikiwa na Bodi ya Mikopo nchini.

TAARIFA YA AWALI KUHUSU ZOEZI LA UHAKIKI WA WANAFUNZI WANUFAIKA WA MIKOPO KWENYE TAASISI ZA ELIMU YA JUU NCHINI.


1.0 UTANGULIZI

Mnamo mwezi Mei, 2016, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliagiza kufanyika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi kwenye Taasisi za elimu ya juu nchini ili kubaini kama kuna uwepo wa wanafunzi wasiostahili kupata mikopo. Zoezi hilo lilifanywa na Timu maalum iliypoundwa na Bodi ya Mikopo kuanzia tarehe 30 Mei, 2016 ambapo hadi sasa zoezi hilo linaendelea.

2.0 MATOKEO YA AWALI YA ZOEZI LA UHAKIKI

Katika zoezi la uhakiki wa wanafunzi jumla ya taasisi 26 zimehakikiwa, ambapo uchambuzi wa taasisi 18 umekamilika. Katika taasisi hizo 18 jumla ya wanafunzi 2,739 hawakujitokeza kuhakikiwa. Jedwali lifuatalo linaonyesha idadi ya wanafunzi ambao hawakuhakikiwa kwa kila chuo.

Na. Taasisi ya Elimu ya Juu Idadi ya Wanafunzi
1. Chuo Kikuu cha Dodoma 763
2. Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha 126
3. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino – Mwanza 232
4. Chuo Kikuu cha Mzumbe 66
5. Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji – Mbeya 130
6. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino – Mbeya 21
7. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohane – Dodoma 262
8. Chuo Kikuu cha Mkwawa 103
9. Chuo Kikuu cha Iringa 100
10. Chuo Kikuu cha Tiba – Bugando 43
11. Chuo Kikuu cha Arusha 55
12. Chuo Kikuu cha Jordan 128
13. Chuo Kikuu cha Makumira – Arusha 98
14. Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine 385
15. Chuo cha Ufundi Arusha 22
16. Chuo Kikuu cha Kiislamu – Morogoro 130
17. Chuo cha Uhasibu Arusha 57
18. Chuo Kikuu cha Mount Meru 17

Uchambuzi wa awali wa Vyuo vingine saba (07) unaendelea. Vyuo hivyo ni: Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yosefu, Chuo cha Biashara – Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Chuo Kikuu cha Mwenge, Chuo cha Biashara - Dodoma na Chuo Kikuu cha Ushirika - Moshi. Taarifa zaidi zitatolewa kadri zoezi litakavyokuwa linaendelea.

Orodha za majina ya wanafunzi ambao hawakuhakikiwa wakati zoezi likiendelea vyuoni mwao zinapatikana kwenye tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz). Aidha, orodha hizo pia zimetumwa vyuoni kwa ajili ya taratibu za uhakiki.

Hivyo, wanafunzi wasiohakikiwa wanatakiwa kujitokeza ndani ya siku saba (07) kuanzia tarehe 13 Julai, 2016 ili kuhakikiwa katika sehemu watakazoelekezwa na Vyuo husika. Menejimenti za Vyuo zinatakiwa kuratibu zoezi hilo ili likamilike ndani ya muda uliopangwa. Wanafunzi ambao hawatajitokeza ili kuhakikiwa mikopo yao itafutwa na kutakiwa kurejesha kiasi walichokopeshwa.

3.0 HITIMISHO

Bodi ya Mikopo inapenda kutoa wito kwa wanafunzi wote ambao hawajahakikiwa kujitokeza haraka ili wahakikiwe kabla ya kuhitimisha zoezi hilo. Aidha, ni muhimu kuzingatia wito huu kwani kutokamilika kwa zoezi hili kunaathiri utekelezaji wa majukumu mengine ya Bodi na Vyuo pia.
Mwisho.

Imetolewa na:

KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU