Taarifa ya TRA ya ufafanuzi kuhusu VAT

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

UFAFANUZI KUHUSU KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWENYE

HUDUMA ZA KIFEDHA (VAT ON FINANCIAL SERVICES)

Bunge la Tanzania limepitisha marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014 kuanzia tarehe 1 Julai 2016 kwenye huduma za kifedha kwa kurekebisha kifungu cha 13 cha Jedwali la Msamaha wa kodi.

Lengo la tamko hili ni kufafanua utozwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za kifedha kwa-

a) Kujulisha umma, Benki, Taasisi za Fedha na wadau wote kuhusu maudhui na utekelezaji wa sheria hii inayolenga kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za kifedha;

b) Kuondoa utata na upotoshaji unaohusu utekelezaji wa sheria hii inayoanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2016; na

c) Kuelezea ukweli kuhusu utekelezaji wa sheria iliyopitishwa na Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao chake cha 3.

Sheria hii inalenga kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia 18 kwenye ada (fees) ambazo benki inatoza wateja wake kwenye huduma mbalimbali zitolewazo na benki au taasisi za fedha.

Kuna taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa VAT itatozwa kwenye amana ya mwenye fedha kwenye benki. Hii siyo kweli. Ukweli ni kuwa kiasi cha VAT kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha.

Mfano: Ada (fees) ya huduma ya benki ambayo mteja ametozwa ni Shilingi 1000/=, Kodi ya Ongezeko la Thamani itakayotozwa kwenye kiasi hiki ni shilingi 152.50 tu na benki kubaki na shilingi 847.50. Kiwango hiki cha shilingi 152.50 ndicho kitakachorejeshwa serikalini na benki au taasisi ya fedha baada ya kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani iliyolipwa kwenye manunuzi ambayo yamefanywa na benki au taasisi ya fedha husika. Kwa mujibu wa sheria hii, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) haitatozwa kwenye riba inayotozwa na benki kwenye mikopo.

Aidha kuna maelekezo yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji wa huduma za kifedha atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala husika haukupitia kwenye akaunti. Taarifa hii si sahihi kwa kuwa ukusanyaji wa VAT husika utafanywa kwa njia ile ile ambayo gharama za huduma za kifedha zinakusanywa sasa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania itatoa maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielekroniki utakavyofanyika ili kuiwezesha benki au taasisi ya kifedha kutimiza matakwa ya kisheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.

Hivyo, kupitia taarifa hii, tunazitaka Benki na Taasisi za Fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa taarifa zisizosahihi kwa umma kuacha mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa. Kimsingi, benki na taasisi za fedha zinazohusika zinaagizwa kurekebisha mara moja taarifa walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi ya marekebisho ya Sheria hii.

“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”

A. J. Kidata
KAMISHNA MKUU
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA.