[update] Tetemeko la ardhi laripotiwa Dodoma na maeneo ya Arusha

screenshot source: earthquake.usgs.gov  accessed by wavuti.com
Baadhi ya wakazi wa mjini Dodoma walijikuta katika tafakari kubwa asubuhi ya leo baada ya kukumbwa na mtikisiko wa ardhi uliosababishwa na tetemeko lililotokea kiasi cha kilomita 76 kaskazini mwa mji huo.

Tetemeko hilo la kiwango cha Richter 5.1. lilitokea saa 06:01:15.2 kitovu chake ni bonde la Haneti - Itiso Wilayani Chemba na lilikuwa na kina cha kilomita 10. Katika ramani ya dunia inaonesdha kwamba limetokea kiasi cha kiliomita 65 Kusini mwa mji wa Kondoa.

Akizungumza Ofisi kwake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo ni kubwa ukilinganisha na matetemeko ambayo yamezoeleka kutokea ambayo yana ukubwa wa Richter 3.

Alisema mikoa mingine ambayo imeathirika na tetemeko hilo ni Tanga, Dodoma, Singida mashariki na Manyara.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka wakala wa Jiolojia Tanzania mkoani hapa ambaye pia ni mtaalam wa matetemeko Gabriel Mbogoni alisema tetemeko hilo limetokea maeneo ya Haneti kilometa 11 mashariki mwa mji wa Haneti Wilaya ya Chemba ambao upo kilometa 79 kutoka kaskazini mashariki mwa mji wa Dodoma.

“Bado hatujapata taarifa zozote za madhara labda kwa sababu bado ni mapema”alisema. [Lukwangule blog]

Mtu mmoja amechangia maoni katika tovuti inayokusanya taarifa za matetemeko duniani, akisema:
No damage, just strong shaking of the bed for about one or two minutes around 6 am.

UPDATE: Julai 14, 2016...

Na Samwel Mtuwa, GST

Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imetoa taarifa kwa wananchi kuhusu tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 13 Julai, 2016, majira ya saa 12:01:15 alfajiri , likiwa na ukubwa wa kipimo cha Ritcher 5.1.

Kitovu cha tetemeko hilo kilitokea umbali wa kilomita 11 Mashariki mwa mji wa Haneti ambao upo umbali wa kilomita 79 Kaskazini Mashariki mwa mji wa Dodoma.

Akizungumza na MEM Bulletin ofisini kwake, Mtalaam wa Matetemeko katika Idara ya Jiolojia, GST, Gabriel Mbogoni, alisema kuwa eneo hilo lipo katika ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, maeneo hayo hukumbwa na matukio ya matetemeko ya ardhi mara kwa mara.

Akifafanua kuhusu chanzo cha tetemeko, Mbogoni alisema kuwa hiyo ni kutokana na tabaka la miamba katika maeneo hayo kuwa na kina kidogo ikilinganishwa na maeneo ambayo yako nje ya ukanda wa Bonde la Ufa.

“Hali hii husababisha matabaka ya miamba katika ukanda huo kuwa katika hali ya fukuto jingi la joto na kusigana kwa miamba ambapo husababisha miamba hiyo kukatika, hali ambayo hufanya ardhi itikisike,” alisema Mbogoni.

Alisema kuwa kiutalaam hali hiyo husababisha miamba hiyo kukatika na kusababisha mtikisiko wa ardhi ambao ndio huitwa tetemeko la ardhi. Akieleza kuhusu madhara ya tetemeko hilo, Mbogoni alisema kuwa mpaka muda wa mchana wa siku ambayo tetemeko lilitokea, hakukuwa na taarifa yoyote ya madhara kwa wananchi, majengo au miundombinu iliyotolewa kutokana na tetemeko hilo.

Alifafanua kuwa eneo la Haneti kijiografia lipo katika ukanda wa Bonde la Ufa, maeneo ambayo yana mipasuko mingi ya miamba. Alisema kiutalaam mawimbi ya tetemeko la ardhi yana tabia ya kusafiri umbali mrefu katika mwendo wa kasi alitolea mfano mawimbi ya P na S yanaweza kusafiri umbali wa kilomita 8-13 kwa sekunde.

Akizungumzia kuhusu tahadhari, Mbogoni alisema kuwa, wananchi wanaposikia hali ya kutokea kwa Tetemeko la Ardhi wanapaswa kuchukua tahadhari ya kukaa mbali na miti, nguzo za umeme na nyumba ndefu kama vile maghorofa, na pindi wanapokuwa ndani ya nyumba wanashauriwa kukaa katika kona za ukuta wa nyumba ili kujizuia na madhara.

Moja ya majukumu ya GST ni kufanya uchunguzi juu ya matetemeko, maporomoko, mipasuko ya ardhi katika eneo zima la nchi, kwa sasa GST ina vituo tisa ya kurekodi taarifa zote za matetemeko katika mikoa mbalimbali ya nchi kama vile Dodoma, Arusha, Babati, Singida, Geita, Kibaya, Kondoa, Mbeya na Mtwara.