Ufa mwingine ulioongelewa na Mwalimu...

Julius Kambarage Nyerere
Julius Kambarage Nyerere

Ufa mwingine ulioongelewa ni ule wa suala la katiba na sheria. Mwalimu alitahadharisha suala la kupuuza, kutoijali na kuchezea chezea katiba. Huu ufa aliouona Mwalimu mwaka 1995 wa viongozi kupuuza, kuchezea katiba na kutoijali kwa sasa hali ikoje? Tulipokuwa tunajitafakarisha tukaiangalia hali tuliyo nayo kwa sasa kwenye eneo la katiba.

Bila kuangalia suala la mchakato wa katiba ambao umesimama kimya tena kimya kikuu, tunaangalia hata hii katiba iliyopo kwa sasa. Kwa kiasi gani inaheshimiwa na haipuuzwi au kuchezewa kama Mwalimu alivyoonya.

Nilipata kuangalia kifungu kimoja tu katika katiba yetu na kufanya uchambuzi kidogo sana. Ibara ya 3 ibara ndogo ya 1 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977 inasema kuwa ‘Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa’.

Iwapo tunaweza kusema ufa wa kupuuza katiba umefutwa inabidi tuangalie hii ibara ambayo inatuonyesha Jamhuri yetu ni nini. Je hii Jamhuri ni kweli ni nchi ya Kidemokrasia? Misingi mikuu ya demokrasia nikiitaja kwa uchache tuanze na msingi wa ushiriki wa wananchi, usawa, stahamala za kisiasa kwa uchache. Kwa kuwa demokrasia ni utawala wa watu uliowekwa na watu kwa ajili ya hao watu, sisi raia wa Tanzania ndio hao tulioweka watawala kwa ajili yetu.

Tunajisikia kuwa ndio tuliowaweka na wapo kwa ajili yetu? Huo utawala uliopo ni wetu? Kila mmoja ajibu kwa jinsi anavyojisikia kuwa sehemu ya utawala wa nchi hii. Nchi hii ni ya Kijamaa, ni nini kinachoashiria ujamaa katika nchi yetu hadi katiba kusema nchi ni ya kijamaa? Nilikuwa nakumbuka jinsi ambavyo nchi ilikuwa imejengwa katika hiyo misingi ya kijamaa moja wapo ikiwa ni utu na undugu. Hivi ni nini kilitokea tukaacha kuitana ndugu na uheshimiwa ukaanza tena kwa kasi? Sikatai kabisa watu kuitwa waheshimiwa lakini najiuliza tu swali dogo.

Huu utawala wa watu unawaweka watu kuwa viongozi kwa niaba yao. Ajabu ni kuwa sisi ambao tunampa mtu kazi ya kutuongoza ghafla tunageuka na yule tuliyemtuma anakuwa mheshimiwa sisi tuliempa kazi tunakuwa wakumpigia saluti na tusipofanya hivyo huenda tukanyimwa mshahara.

Hii hali ya watu kuchinjana kwa kasi bila huruma inatokana na nini? Utu uko wapi? Tumeielewa vizuri hii katiba yetu? Ni kweli kuwa hatufahamu kuwa waliompa mtu kura ndio wakuu na si vinginevyo? Ujamaa ndio ulipoanza kuzimika. 
  • Sehemu hii imenukuliwa kutoka kwenye makala iliyochapishwa kwenye gazeti MTANZANIA