Ujangili wazidi kutikisha Moshi: Walinzi 2 Ahsante Tours wauawa, Milioni 65/= zaibwa


Watu wasiojulikana wamevamia ofisi za Kampuni ya Ahsante Tours ya mjini Moshi na kuua walinzi wawili na kuiba Sh 65.5 milioni.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya watu wasiojulikana kuvunja duka la kubadilisha fedha la Chase Forex Bureau De Change la mjini Moshi na kuiba zaidi ya Sh120 milioni.

Tukio la mauaji ya walinzi wawili ofisi za Ahsante Tours, lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya watu hao kuwazidi nguvu walinzi na kuwafunga kamba kisha kuwapiga kwa kitu butu kichwani.

Kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara Cathbert Swai na mkewe Stella Shangali, ambao pia wanamiliki hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo Mailisita, nje kidogo ya mji wa Moshi.

Taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya kampuni zinazoongoza kwa kupokea watalii wengi, zinadai huenda tukio hilo ni mpango wa ndani.

“Kuna maswali mengi tunajiuliza. Walijuaje kuna kiasi hicho kikubwa cha fedha kama taarifa hazikutoka miongoni mwetu?” alihoji mmoja wa wafanyakazi aliyeomba jina lake lisitajwe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema kati ya fedha zilizoibwa, kulikuwa na Dola za Marekani (Sh50 milioni) na Sh15 milioni za Tanzania.

Walinzi waliouawa wametajwa kuwa ni Omar Mohamed (48), mkazi wa Matindigani Pasua na Dominick Cheddy (41), mkazi wa Mailisita na wote ni wenyeji wa mkoa wa Tanga.

Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo liligunduliwa saa 1.00 asubuhi na wasamaria wema waliotoa taarifa polisi, na uchunguzi wa awali umebaini watu hao walikata uzio wa ofisi hizo.

“Baada ya kuingia ndani ya jengo hilo la ofisi walivunja ofisi ya meneja mkuu na baadaye ofisi ya mhasibu ndio wakaiba Dola 23,300 na pesa za Tanzania Sh15 milioni,”alisema Kamanda Mutafungwa.

“Tunashuku kuwa huenda hao majambazi waliamua kuwaua hao walinzi baada ya hao walinzi kuwatambua. Bahati mbaya hawakuwa na silaha yoyote hata panga hawakuwa nalo,”alisisitiza.

Kamanda Mutafungwa alisema Polisi inamshikilia mtu mmoja ambaye inaonekana alikuwepo wakati mauaji na uporaji huo ukifanyika lakini, majambazi hao hawakumdhuru sehemu yoyote.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa, aliwataka wafanyabiashara kupeleka pesa benki badala ya kuzihifadhi ndani au ofisini na kuwataka pia kuimarisha ulinzi ikiwamo kuweka CCCTV Camera.

Alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa za waliohusika na tukio hilo, kulisaidia Jeshi la Polisi kama ilivyotokea wiki moja iliyopita ambapo taarifa zao zilisaidia kuwatia mbaroni wahalifu mbalimbali 30.