Vijana wa kiume wenye matiti makubwa kupatiwa upasuaji Agosti 1 -10, Bombo hospitali na mabingwa kutoka Ujerumani

VIJANA wa kiume wenye matiti makubwa wanaweza kuondokana na hali hiyo kama watafika hospitali ya Bombo mkoani Tanga na kujiandikisha kufanyiwa upasuaji na madaktari bingwa kutoka Ujerumani watakaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kazi ya upasuaji wa kurekebisha maumbile.

Pamoja na kufanya upasuaji wa matiti madaktari hao pia watafanya upasuaji wa vipele sugu katika ngozi, kuungua vibaya, uvimbe unaotoa damu pamoja na vidonda sugu.

Aidha madaktari bingwa hao watafanya upasuaji wa uvimbe wa aina mbalimbali uliokaa katika sehemu ya nje ya mwili kama makovu sugu, midomo sungura, uwazi katika kinywa, vidole pacha na madole bonge.

Upasuaji huo utakaofanywa na madaktari 12 kutoka shirika la Intertplast la nchini Ujerumani utafanyika kwa siku 10 kuanzia Agosti Mosi.

Mratibu wa Interplast Tanzania, Dk Walles Karata akizungumza na waan dishi wa habari mjini Tanga leo alisema kwa sasa tayari zoezi la kuandikisha wagonjwa limeanza.

Alisema wanatarajia kukamilisha uandikishaji wa wagonjwa Julai 24 na upasuaji utaanza Agosti Mosi.
“Upasuaji wote utafanywa bila gharama yoyote lakini kwa sasa mgonjwa atalazimika kuchangia kiasi cha sh. 10,000 tu kwa ajili ya usajili wa kadi katika hospitali ya Bombo baada ya hapo shughuli zote zitagharamiwa na shirika la Interplast,”alisema.
via Lukwangule blog