Wafanyabiashara wakubwa wanaokamatwa kwa kukwepa kodi waongezeka

Kikosi kazi maalumu cha vyombo vya dola, kinaendelea na kamatakamata dhidi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa kwenye mtandao wa ukwepaji kodi na utengenezaji wa stakabadhi feki, huku kilio kikitawala kwa wafanyabiashara wa Jiji la Arusha na Dar es Salaam.
Idadi ya wafanyabiashara hao waliokamatwa katika msako huo imeongezeka na kufikia zaidi ya 10 hadi kufika jana jioni.

Chanzo cha kuaminika jijini Arusha kililiambia MTANZANIA kuwa, wafanyabiashara wawili wa jijini humo walikamatwa Jumamosi Julai 2, mwaka huu na kulazwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Wafanyabiashara hao ambao majina yao yamehifadhiwa walikamtwa na kikosi hicho, kisha kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam.

Mmoja wafanyabiashara hao ni mmiliki wa kampuni za ujenzi na huduma za kusambaza mafuta kwenye minara ya kampuni za simu.

“Ni kweli wamekamatwa wafanyabiashara wawili wa hapa Arusha ambao (anawataja majina), huyo mmoja ni mmiliki wa maduka makubwa ‘Super Market’ hapa mjini ambaye pia ndiye aliyekuwa wakala wa usambazaji wa mashine za kufyatulia stakabadhi za kielektroniki (EFD) na alipewa kazi hii kwa mkoa mzima wa Arusha,” alisema mtoa habari wetu kutoka ndani ya vyombo vya dola ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Chanzo hicho kilisema kuwa baada ya kutiwa nguvu kwa wafanyabiashara hao ndugu na jamaa zake walikwenda polisi kwa lengo la kumdhamini, lakini juhudi zao ziligonga mwamba.

Pamoja na hali hiyo ndugu hao walilazimika kukodi mawakili wa kampuni moja maarufu jijini hapa, ambapo nao walishindwa hali iliyowafanya wafanyabiashara hao kulala ndani.

“Taarifa hizo ni za kweli, mzee pamoja na umaarufu na utajiri wake alilala mahabusu kwani tangu alipokamatwa juzi jioni tulijaribu kufanya jitihada za kupata dhamana tukiwa na mawakili lakini ilishindikana hadi pale yeye na wenzake waliposafirishwa chini ya ulinzi mkali,” alisema mtoa habari wetu.

Kutokana na tukio hilo MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusu kukamatwa kwa wafanyabishara hao, ambapo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo.

“Hilo halinihusu, sisi tulitumwa kuwakamata tu na wala usinidadisi zaidi,” alisema RPC Mkumbo huku akisisitiza asiendelee kuulizwa maswali mengine kuhusiana na tukio hilo.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha (TRA), Apili Mbarouk, alipoulizwa kuhusua suala hilo alisema hana taarifa za tukio hilo.

“Kwa hapa Arusha sina hizo taarifa, labda kama vyombo vya vingine vilihusika na suala hilo kwa hapa mkoani kwetu,” alisema Mbaruok.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Arusha, Juventus Baitu, alisema hana taarifa za kukamatwa kwa wafanyabiashara hao.

Kutokana na hali hiyo taarifa kutoka jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa idadi ya watuhumiwa waliotiwa mbaroni imeongezeka kutoka watuhumiwa watatu hadi watano hadi kufikia jana jioni.
Kambi Takukuru

Baada ya taarifa za jana na kuripotiwa na gazeti hili ambapo Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, kumtaka mwandishi wa habari hizo kufika Makao Makuu ya Takukuru jana, alijikuta akigonga mwamba.

Timu hiyo ya waandishi ilipofika Takukuru, wakiulizwa na watumishi wa ofisi hiyo ambao walitaka kujua kama waandishi hao wana ahadi na Mkurugenzi Mkuu, ambapo licha ya kujieleza kuwa ahadi hiyo ilikuwapo, lakini walishindwa kumfikia.

Pamoja na kukaa kwenye eneo hilo kwa zaidi ya saa nne mfululizo bila mafanikio, alipotafutwa kwa njia ya simu Kamishna Mlowola, kuhusu ahadi yake ya kutoa ufafanuzi, alimtaka mwandishi kuwasiliana na Msemaji wa Takukuru kwa ufafanuzi zaidi.

“Hapa tuna utaratibu sasa kwa suala lako pamoja na kuwasiliana na kukutaka uje lakini wasiliana na msemaji wetu yeye ameshapewa maelekezo tayari atakujibu,” alisema Mlowola.

Alipotafuwa Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema hawezi kuzungumzia suala la kukamatwa watu wanaodaiwa kukwepa kodi, huku akimtaka mwandishi kwenda ofisini na aandike maswali kisha atajibiwa baada ya majibu kupatikana.

“Huo ndiyo utaratibu wetu na si vinginevyo siwezi kusema wamekamatwa ama laa tunaogopa ‘kudistort’ nakushukuru sana,” alisema Misalaba.