Wajawazito walazwa sakafuni katika jengo la CCM lililogeuzwa wodi

Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto akimpa pesa ya matumizi mzazi aliyejifungulia chini katika moja kati ya vyumba vya ofisi ya CCM kijiji cha Kihesa Mgagao jana ,wajawazito hao hulazwa chini kutokana na chumba kilichopo katika zanahati ya kijiji kutokuwa na uwezo wa kuhudumia wajawazito watatu
Na MatukiodaimaBlog 

WAJAWAZITO katika kituo zahanati ya Kihesa Mgagao wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wamekuwa wakilala chini katika godoro chini kwenye ofisi ya CCM kijiji cha Kihesa Mgagao kutokana na zahanati hiyo kukosa chumba kikubwa na vitanda vya kutosha.

Hata hivyo Zahanati hiyo imekuwa ikiwalaza pamoja wajawazito na wagonjwa wa kawaida hasa pindi wagonjwa wanaofika kutibiwa kuzidi wawili kwa siku.

Mwandishi wa mtandao huu wa MatukioDaimaBlog aliyefika zahanati hapo alishuhudia hali hiyo ya wajawazito hao kulazwa sakafuni baada ya chumba kidogo chenye vitanda viwili pekee cha kujifungulia kwenye Zahanati hiyo kuwa na wanawake wagonjwa wengine ambao walikuwa wajifungua.

Uongozi wa Zahanati hiyo umedai kuwa changamoto katika zanahati hiyo zipo nyingine ikiwemo ya ukosefu wa chumba cha kupumzika wagonjwa hali iliyowalazimu kuomba baadhi ya vyumba katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiji cha Kihesa Mgagao ili vitumike kama wodi la kupumzisha wagonjwa na vyumba vya kujifugulia kwa wajawazito wanaofika Zahanati hiyo.

Pia ulisema hata hivyo wagonjwa hao wamekuwa wakilala gizani kutokana na kukosekana na taa za solla ama za kawaida kwa ajili ya matumizi na kuwa shughuli za kuwahudumia wagonjwa hao huwa ni shida kuzifanya gizani hivyo hulazimika kutumia tochi.

Alisema kimsingi zahanati hiyo iliyojengwa mwaka 2008 ndio ambayo inatumika kama kituo cha afya cha kata kutokana na ujenzi wa Kituo cha afya kutokamilika hivyo iwapo wajawazito watafika zaidi ya wawili kwa siku na wagonjwa wengine basi hulazimika wote kuchanganywa katika chumba kimoja kwenye jengo la CCM.

Pia alisema jingo hilo linalotumika kama wodi kiafya si salama kwa wagonjwa kwani halina mazingira mazuri ya kiafya huku suala la chombo cha kuchomea taka (Sterility)zinazotumika Zahanati hapo hakuna hivyo wamekuwa wakichoma kienyeji katika shimo la kawaida jambo ambalo ni hatari zaidi kiafya.

Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto ameahidi kuwasaidia ujenzi wa chumba kikubwa ambacho kitatumika kama wodi la wagonjwa na wajawazito wakati ujenzi wa kituo cha Afya ukiendelea .

Alisema kuwa amesikitishwa na hali hiyo ambayo aliiona katika Zanahati hiyo jana na kuwa ameutaka uongozi wa kijiji kuwasiliana na Halmashauri ili eneo lililopo liweze kutumika kuongeza jengo ambalo litatumika kama wodi

Wakati huo huo mbunge Mwamoto amekabidhi pesa za kununulia taa mbili zinazotumia nishati ya mwanga wa jua (solar) ambazo zitatumika wodini wakati huu ambao zoezi la kusogeza umeme wa Rea likiendelea na kuwa tayari amemuomba meneja wa TANESCO  mkoa kufika leo kutazama eneo hilo ili nguzo za umeme zilizoishia gereza la kihesa Mgagao zifiki kijijini hapo, na kuwa suala la vitanda ataendelea kulifanyia kazi.


Mama aliyejifungua akiwa amejipumzisha katika chumba cha ofisi ya CCM kwa kutandikiwa godoro sakafuni


Ofisi hiyo pia hutumika kama stoo


Zahanati ya Kihesa Mgagao


Jengo la CCM linalotumika kama wodi


Shimo la kuchomea taka


Mzazi akiwa amelala ndani ya jengo la CCM