Wakurugenzi 185 waapishwa; WM Majaliwa awafunda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manidpaa na Majiji 185 kabla ya hawajala kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Magufuli awataka Wakurugenzi wa Halmshauri nchini kuondoa kero za wananchi


Na Jonas Kamaleki

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmshauri zote nchini kuondoa kero za wananchi na si kuwaongezea kero.

Hayo ameyasema leo kwenye hafla ya Kiapo cha Uadilifu wa Utumishi wa umma kwa Wakurugenzi Watendaji wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri nchini,iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Anzisheni miradi inayotatua kero za wananchi na si kuwaongezea kero, kila eneo lina kero zake hivyo jitahidini kuziondoa,”alisema Rais Magufuli.
Amewataka Wakurugenzi hao kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya wananchi kwani wamechoshwa na kero hasa kwenye ushuru na kodi zisizo za lazima, akitolea mfano mkulima wa mchicha na mpunga kutozwa kodi wakati amelima kwa ajili ya chakula chake ya kwamba hili jambo halikubaliki.

Rais Magufuli amewaambia Wakurugenzi kuwa anawaamini kwani uteuzi wao ulifanywa kwa umakini na akaonyeshwa kushangazwa na waliokuwa wakibeza uteuzi huo hasa waliosema kuwa amemteua mwenye cheti cha usimamizi wa hoteli.
“Majina kufanana si tatizo, mimi niliyemteu ni Bwana Luhende ambaye ana diploma na masters (shada ya uzamili), Bwana Luhende hebu simama wakuone na vyeti vyako,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa hakubahatisha katika kuteua Wakurugenzi hao na kuongeza kuwa kazi hiyo ameifanya kwa umakini mkubwa.

Rais amewataka Wakurugenzi kuhakikisha wanakusanya na kusimamia kodi za wananchi ili kuwaletea maendeleo na kuwaondolea matatizo ambayo yamewachosha.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan amewataka Wakurugenzi kuwa watumishi wa watu na si watawala.

Amewaasa Watendaji hao kujifunza sheria na kanuni zinazohusiana na kazi zao na kuwataka wawe waadilifu na wachapakazi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majali Majaliwa amewataka Wakurugenzi kuwa wawajibikaji, waadilifu na waaminifu.
“Ninyi ni injini ya maendeleo katika nchi kupitia kwenye Halmashauri zenu na kazi yenu kubwa ni kusimamia watumishi katika kuleta maendeleo katika sehemu zenu,”alisema Majaliwa.
Amewataka Wakurugenzi kukusanya kodi na kuzitumia katika miradi ya maendeleo kwa uaminifu na kuwasisistiza kuzingatia thamani ya fedha katika mradi husika (Value for Money)

Jumla ya Wakurugenzi 185 wamekula kiapo cha uadilifu katika utumishi wa umma na kuhudhuria mafunzo ya maadili yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano ulioitishwa na Rais John Magufuli kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za wilaya na baadhi ya Wakuu wa wilaya ikulu jijini Dar es salaam Julai 12, 2016. (PiCha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya waende wakafanye kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 12, 2016) wakati akizungumza na wateule hao kabla hawajatoa viapo ya maadili katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji utulivu na kujituma. Kila mmoja wenu anatakiwa akafanye kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu,” 
amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Ninyi ndiyo injini ya maendeleo katika Halmashauri zote hapa nchini na pia mna dhamana ya kusimamia fedha za maendeleo katika halmashauri zenu. Mtajikuta mna jukumu la kusimamia fedha za ndani pamoja na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Hakikisheni mnasimamia matumizi ya fedha hizi ili kupata value for money.”
Waziri Mkuu aliwataka wawe makini wasije wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha dhidi ya watendaji wengine, migogoro ya kikazi na pia migogoro na wananchi wanaoenda kuwaongoza.
“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao ni wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara, watumishi wa idara mbalimbali zilizo chini yenu na watendaji wa kata na vijiji”, alisema.
Alisema wanatakiwa wakasome taarifa mbalimbali ili waelewe majukumu yao pamoja na mipaka yao, waelewe maeneo yao ya utawala ni yapi lakini pia wajipange kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani imebeba ahadi zilizotolewa na Rais pamoja na Makamu wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi. 

Aliwaasa pia wasiache kutafuta hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11,aliyoitoa Novemba 20, mwaka jana na kuwataka waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwa vile inatoa dira ya utendaji katika maeneo yao. 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan aliwataka wateule hao watambue dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala.
“Wewe ni mtumishi wa watu, na watu hao pia wana wawakilishi wao ambao ni madiwani. Kwa hiyo fanyeni kazi kwa karibu na madiwani, sikilizeni shida za wananchi na pangeni vipaumbele vya kazi na pia msiache kujifunza. Soma wajibu wako kisheria na kikatiba ni upi lakini pia jipe muda wa kujifunza,” alisisitiza.
“Wewe ni kiongozi kwa hiyo tengeneza watu wako ili wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya. Fanyeni kazi kwa bidii kwa sababu Tanzania inaenda kwa spidi sana lakini pia mjihadhari na kashfa za matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia fedha vibaya utapata fedheha…” aliongeza.
Akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt John Pombe Magufuli aliwataka wawe ni watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwa watengeneza kero na akasisitiza wawe mitume wazuri kwa wananchi.
“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogondogo hata za kuuza mchicha tu. Mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi, ni lazima kodi hizi mkazizuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisema.
Alisema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo alilopo, waitekeleze hiyo mipango, na wafanye kazi kwa kushirikiana na viongozi walio juu yao na walio chini yao. 
 
Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini.
“Nendeni mkajipange tuwe na viwanda vidogo vidogo katika maeneo yenu”, alisisitiza.
“Nataka watu wafanye kazi. Bila kazi hakuna hela. Nataka mkahimizie tabia ya kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yetu. Watanzania wote bila kujali dini zetu, vyama au makabila ni lazima tufanye kwa sababu nataka Tanzania iingie haraka kwenye mataifa ya uchumi wa kati, na hili linawezekana,” alisema huku akishangiliwa.
(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, JULAI 12, 2016.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Luhende Pius akionesha cheti chake cha taalum kwa waandishi wa habari baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na uwepo wa taarifa potofu juu ya taaluma yake. wakati wa hafla ya kula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa,Miji na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni.Leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. John pombe Magufuli akiongea na wakurugenzi wateule wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji Ikulu jijini Dar es salaam Julay 12, 2016Baadhi ya Wakurugenzi wateule wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji wakimsikiliza kwa makini Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam Julai 12, 2016

Mkurugenzi wa halmashauri ya Itigi Luhende Pius Gerald akionyesha vyeti vyake vya masomo kwa wandishi wa habari, Luhende alichafuliwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa elimu yake ni cheti cha usimamizi wa hoteli, amewaonesha wandishi wa habari kuwahakikishia kuwa Elimu ya UzamiliPicha ya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji 185