Waziri Mbarawa amteua Kadogosa kuwa Mkurugenzi Mtendaji TRL

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amemteua Bw. Masanja Kungu Kadogosa kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL). Uteuzi huo umeanza Julai 01, 2016.

Bw. Kadogosa, mwenye umri wa miaka 41, mapema Februari 4, 2016 aliteuliwa na Serikali kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa awali Mhandisi Elias Mshana kuanza likizo ya kustaafu.

Aidha kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa juu katika TRL Bw. Kadogosa alikuwa Mkurugenzi wa Mikopo katika Benki ya ya Maendeleo ya TIB.

Kitaaluma Mkurugenzi huyo mpya ni msomi wa Masuala ya Uhasibu, Usimamizi wa Fedha na Benki akiwa na Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara aliofuzu katika Chuo kikuu cha Umea mwaka 2004 nchini Sweden. 

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Dar es Salaam,
Julai 15, 2016