WM Majaliwa akabidhiwa portable clinical labWaziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitazama sanduku ambalo ni maabara inayohamishika inayoweza kutumika katika zahanati na vituo vya afya ambayo imetengenezwa na kampuni ya Acuuster Technologies Pvt Limited ya India, Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Julai 12, 2016.

Kulia kwa Waziri Mkuu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Dkt. Mpoki Ulisubisya na kushoto kwake ni Mkurugezi Mtendaji wa kampuni hiyo, Amit Bhatnagar. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhiwa maabara ya kitabibu inayoweza kubebwa kwenye sanduku (Mobile and Compact Portable Clinical Laboratory) ambayo ni rahisi kutumika mahali popote hata kwenye maeneo yasiyo na umeme.

Maabara hiyo ambayo inatumia umeme wa mionzi ya jua inaweza pia kuchajiwa na betri ambayo inawashwa na umeme wa kwenye gari.

Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu jana (Jumanne, Julai 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ACCUSTER ya India, Bw. Amit Bhatnagar alisema maabara hiyo imeundwa kwa lengo la kusaidia kupunguza tatizo la umbali kwa wananchi waishio vijijini.
“Jumla ya taasisi za kijamii 100 nchini India zimekwishanunua maabara hii na kikubwa wanachojivunia ni kuweza kuchukua vipimo vya wagonjwa hadi mlangoni kwao kwenye vijiji zaidi ya 45, wakati mgonjwa halazimiki kutembea umbali mrefu na majibu anayapata hapohapo,” alisema.
“Kwa wastani maabara hii inaweza kuhudumia watu 150 kwa siku na kila kipimo kinachowekwa kinatumia muda wa sekunde mbili kupata majibu yake. Taarifa zake zinaweza kuhamishika kwa kutumia USB au Bluetooth connection,” aliongeza.
Bw. Bhatnagar ambaye alikuwa miongoni mwa wafanyabiashata 50 waliombatana na Waziri Mkuu wa India aliyezuru Tanzania Jumamosi iliyopita, alisema maabara hiyo ina vifaa vyote muhimu kama Biochemistry Analyzer, Centrifuge, Incubator, Data Recorder with Patient Data Management Software, Micropipettes na power back-up. Pia inakuwa na Laptop ndogo ya kupokelea na kuhifadhi taarifa za vipimo vya wagonjwa.

Pia alimweleza Waziri Mkuu kwamba vifaa vya maabara hiyo vinaweza kufanya kazi kwenye mazingira yasiyohitaji ubaridi kwani vina uwezo wa kuhimili joto kuanzia nyuzijoto 00 hadi nyuzijoto 500.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ambaye alimwita Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya aje kushuhudia maabara hiyo, alisema ameguswa baada ya kubaini kuwa maabara hiyo inaweza kufanya vipimo vingi vikiwemo vya malaria, magonjwa ya ini, na moyo.

Kwa upande wake, Dkt. Ulisubisya alimweleza Bw. Bhatnagar kwamba itabidi maabara hiyo pamoja na vifaa vyake ikafanyiwe uchunguzi juu ya matumizi na kwamba vikikamilika atapatiwa ripoti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).
“Utatakiwa kuandika write-up na kuiwasilisha TFDA na wakikamilisha uchunguzi, watatuletea taarifa ambayo tutaituma kwako,” alisema.
Vilevile, Dkt. Ulisubisya alimweleza Waziri Mkuu kwamba ameridhika na wastani wa gharama za vipimo kwa kila mgonjwa ambayo ni kama sh. 15 lakini bei ya maabara hiyo iko juu. Awali, alielezwa na Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa bei yake ni rupia za India 326,000 (sawa na sh. milioni 10.4).

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.

JUMATANO, JULAI 13, 2016