Buriani Mzee Aboud Jumbe Mwinyi


Aliyewahi kuwa Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kati ya tarehe 7 Aprili 1972 hadi 30 Januari 1984, na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia mchana wa leo nyumbani kwake Kigamboni, jijini Dar es Saalam baada ya kuugua kwa muda mrefu,

Mzee Jumbe ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 96 akiacha watoto 13 na wajukuu takariban 40.

Kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe kimethibitishwa na mtoto wa marehemu, Mustafa Aboud Jumbe akisema kuwa marehemu anatarajia kuzikwa kesho mchana nyumbani kwake Migombani, Zanzibar

Marehemu Jumbe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuiongoza Zanzibar akichukua nafasi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo marehemu Abeid Aman Karume aliyefariki mwaka 1972.

Enzi za uhai wake akiwa rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar alishirikiana na rais wa wakati huo wa Tanzania na mwenyekiti wa chama cha TANU marehemu Julius Nyerere kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuvunja vyama vya TANU na ASP na kuunda chama kimoja cha CCM.

Imeelezwa kuaw, Alhaji Jumbe aliwahi kutoa wosia wake hadharani akitaka mazishi yake yasibene sura ya kitaifa na wala jeneza lake lisifunikwe bendera ya taifa au ya chama na kuomba yawe ya mazishi ya Muislamu na mwananchi wa kawaida.