CUF kufa kifo cha mende?

CHAMA cha Wananchi (CUF) ni kama kipo kuzimu. Kimelegea, kimechuja na kwa sasa kimegota, --- limechapisha gazeti tando la MwanaHALISI Online.

CUF ya Prof. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa kabla ya kujiweka pembeni, si hii inayoongozwa na Twaha Taslima ambaye amebeba mikoba ya uenyekiti kwa ‘dharura’.

Wapo wanaochekelea kuiona CUF ya sasa ikikosa miguu ya kusimama, ikipoteza mvuto na mvumo wake katika siasa za nchi hii.

Wapo wanaotamani CUF ifutike leo, kesho, wapo wanaovutiwa na mwenendo wa kuchechemea wa CUF kwa sasa lakini pia wapo wanaotamani Taslima awe mwenyekiti wa taifa wa chama hicho. Si kwa wema, isipokuwa ni kwa imani kwamba, Taslima ndio njia sahihi ya kuzima nuru ya CUF kwenye uwanja wa siasa nchini. Dalili hizo zipo wazi, tangu Taslima aingie madarakani chama hicho hakijulikani kinafanya nini, kina mipango gani na kina mwelekeo upi? Chama hicho kwa upande wa Bara ni kama kimebemendwa.

CUF inayovuma ni ile ya Zanzibar chini ya Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho. Kwa sasa unapozungumzia CUF unazungumzia Zanzibar. CUF ya Bara ipo ziiii! Sababu ni kwamba, CUF ya Bara baada ya Prof. Lipumba haijapata mbadala, anayeshika mikoba yake hana sifa, uwezo, ubunifu na hata uono wa kisiasa.

CUF ya Bara kwa sasa inajifichwa kwenye kwapa la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Inategemea huruma ya matamko ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha NCCR-Mageuzi ili kusikika.

CUF ya Taslima imepoa, haina harakati kama zile zilizokuwa zikifanywa na Prof. Lipumba. Watendaji wa CUF kwa sasa wanaishi kwa majungu. Baadhi yao wana fikra finyu kuhusu mwelekeo wa chama hicho. Unapozungumza nao hawaoneshi mwelekeo wa chama hicho, wanachojali ni kwamba ‘wapo huru’.

Prof. Lipumba alijiuzulu Agosti mwaka jana kwa madai kuwa, viongozi wenzake wanne kutoka UKAWA  kumkaribisha ndani ya umoja huo Edward Lowassa na kisha kumteuwa kuwa mgombea wake wa urais. Ndipo Taslima akatwaa nafasi hiyo kwa muda. Kinachofanyika ndani ya chama hicho hakieleweki, mwelekeo wa CUF unatia mashaka.

Taslima ana utofauti mkubwa na Prof. Lipumba kwenye siasa za ushindani katika nchi hii, ni kwa kuwa Prof. Lipumba alikuwa na uwezo wa kuchambua na kuandika mambo ya kijamii, kiuchumi na kisasa jambo ambalo halipo kwa kaimu mwenyekiti wa sasa (Taslima). Prof. Lipumba ana ushawishi mkubwa na kwa watu wengi tofauti na Taslima ambaye mpaka sasa sehemu kubwa ya Watanzania hawamjui, hawajawahi kumuona na pia uwezo wake hauonekani.

Kwa bahati mbaya Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu (Bara) hana uwezo wa kuhuisha harakati za CUF.

Lipo la kujifunza kwa CHADEMA wakati walipoamua kumtwaa Lowassa ambaye alikuwa amechafuka kutokana na kauli zao za awali.

Tathimni ndani ya CHADEMA zilionesha kuwa Lowassa bado ‘keki’ kwa taifa. Licha ya baadhi ya viongozi wa chama hicho kutotaka kumpokea lakini alijiunga na chama hicho hivyo kuwa mwiba kwa CCM. CHADEMA ilisoma alama za nyakati na kwa kuwa, lengo la siasa ni mafanikio, ilimtwaa Lowassa ambaye mafanikio yake ndani ya CHADEMA na UKAWA hakuna anayeweza kubeza. CHADEMA ilimpoteza Dk. Willibrod Slaa kwa kuwa, thamani yake mbele ya Lowassa ilikuwa ndogo.

Turudi CUF, thamani ya Taslima ni kubwa kuliko Prof. Lipumba katika mazingira ya sasa? Sihitaji jibu.

Bila shaka, uamuzi wa kukurupuka, uliojaa chuki, husda na ujinga uliotamalaki unaweza kuizika CUF.

Pamoja na kutangaza nia ya kuitaka nafasi ya uenyekiti, lakini kwa sasa Taslima sio mtu sahihi kwa nafasi hiyo vinginevyo chama hicho kitakufa kifo cha mende.