Jeshi la polisi lawaengua zaidi ya watumishi 600 wasio askari


Jeshi la Polisi limewaengua watumishi wake zaidi ya 600 wasiokuwa askari, limeripoti gazeti la NIPASHE Jumapili hii.

Uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo walilopewa Julai 18 mwaka huu na Rais John Magufuli, la kuhakikisha kuwa wanabaki na watumishi askari katika kila eneo, lengo likiwa ni kuepuka kuchafuliwa kwa taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyodaiwa kufanywa zaidi na watumishi walio raia wakawaida ndani ya jeshi hilo.

Magufuli alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi wa Polisi 35, Ikulu Jijini Dar es salaam mara baada ya askari hao kula kiapo cha uadilifu.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema tayari mchakato wa kutekeleza ushauri wa Rais Magufuli kwa kubainisha majina ya watumishi hao (zaidi ya 600) na kuyawasilisha Wizara ya Utumishi kwa hatua ya kuwaondoa katika orodha ya watumishiwa Jeshi la Polisi.

Meja Jenerali Rwegasira aliongeza kuwa majina hayo ya watumishi wasio kuwa polisi ya meshawasilishwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Angela Kairuki.

“Tayari mchakato umefanyika na zaidi ya watumishi raia wakawaida 600 tumeshapeleka majina yao Utumishi kwa ajili ya kuwaondoa kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza,” alisema Meja Jenerali Rwegasira.

Akifafanua zaidi, Rwegasira alisema watumishi raia watakaoonekana kuwa wanapaswa kubaki ndani ya jeshi hilo kutokana na weledi wao mbalimbali, watawabakiza kwa sharti kwamba nilazima waende kuhudhuria mafunzo na kufuzu ili wawe na sifa za kuwa askari.

“Wale ambao wanafaa na kukubaliwa watapewa nafasi ya kwenda kuchukua mafunzo ya Jeshi… siyo kwamba sasa kuna watu wamepelekwa kuchukua mafunzo.

Nasema ikitokea nafasi wanaweza kupelekwa na yeyote atakayetoka kwenye mafunzo hayo atalazimika kufanyakazi kwa kufuata vyeo vya Jeshi la Polisi,” alisema.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi limekuwalikikumbana na taarifa mbaya za kuwapo kwa vitendo kadhaa vya rushwa na ufisadi, baadhii vikiwa ni kulipwa mamilioni ya fedha za posho maalumu wanazopata askari kwa watumishi wasio kuwa askari na pia madai ya jeshi hilo kuingizwa katika mikataba mbalimbali isiyo kuwa na maslahi kwao (polisi) nataifa.

Aidha, ni wazi kuwa uamuzi huo wa kuwaondoa watumishi wote raia ndani ya jeshi hilo utawaacha baadhi yao wakipata mshituko, wakiwamo wale waliotumikia jeshi hilo kwa muda mrefu katika fani mbalimbali zikiwamo za uhasibu, ufundi mbalimbali, udaktari wa binadamu, ufundi na wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Hili ni pigo kubwa kwa baadhi ya watumishi hao raia kwa sababu sasa hatima yao itategemea maamuzi ya Wizara ya Utumishi. Sijui itakuwaje… lakini ukweli ni kwamba Rais yuko sahihi. Kuna watu wasio kuwa askari walikuwa wakijisahau na kuchafua mwenendo wa jeshi kutokana na kutanguliza zaidi maslahi yao binafsi,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana.
Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Waziri Kairuki alisema ni kweli amepokea majina ya wahusika wote na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa.

Aliongeza kuwa, hatua kama hiyo inachukuliwa pia katika majeshi mengine baada ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa kuwasilisha orodha ya watumishi raia 100 ambao wanatakiwa kuondolewa.