Kuhusu kutenguliwa Mkurugenzi na uhusiano wa kushindwa CCM Morogoro 2015.

Taarifa kwa vyombo vya habari

Agosti 1, 2016


Kuhusu kutenguliwa kwa Mkurugenzi wa Bagamoyo na uhusiano wa kushindwa CCM katika majimbo ya Mlimba na Kilombero, mkoani Morogoro 2015.

Julai 30, mwaka huu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bagamoyo, Bibi Azimina A. Mbilinyi. Taarifa hiyo iliyosainiwa na Eng. Musa Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, ilisema Rais alitengua uteuzi huo kwa sababu hakuridhishwa na utendaji kazi wa Bibi Azimina A. Mbilinyi.

Baada ya taarifa hiyo, wapo watu wanaohusisha kutenguliwa mkurugenzi huyo na kushindwa kwa CCM katika majimbo ya Mlimba na Kilombero. Kabla ya kuhamishimiwa Bagamoyo, Bibi Mbilinyi alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero, yenye majimbo mawili ya uchaguzi, ambayo yote wabunge wake ni wa kambi ya Chadema; Peter Lijualikali-Kilombero na Suzan Kiwanga Mlimba.

NINACHOKIJUA KUHUSU MAJIMBO HAYA

Naandika haya kama mtu ambaye nilishiriki kura za maoni na niliona kasoro zilizotokea na ndizo zilizosababisha CCM kushindwa, unaweza kuona hata madiwani tumepata wachache kuliko wenzetu. Nilikuwa kati ya watia nia katika CCM Jimbo la Mlimba, wengine niliogombea nao ni Dk Frederick Sagamiko (ambaye sasa ni Mkurugenzi-Maswa), Senorina Kateule, Godwin Kunambi (ambaye ndiye alipitishwa na chama kugombea), Augustino Kusalika, George Swevetta, Castor Ligallama, Profesa Jumanne Mhoma, Jane Mihanji, Fred Mwasakilale.

Kwa upande wa Jimbo la Kilombero watia nia walikuwa Kanali mstaafu Harun Kondo, Vitus Lipagila, Abdullah Lyana, Oscar Mazengo, Japhet Mswaki, Paul Mfungahema, John Guninita, Abubakari Asenga (ambaye sasa ni katibu tawala Rombo) na Abdul Mteketa.

MCHAKATO WA KURA ZA MAONI

Katika mchakato wa kumpata mgombea wa Ubunge, hapo ndipo tatizo lilipoanzia; Kwa mfano katika Jimbo la Mlimba, tangu siku ya kwanza ya kampeni katika kumsaka mgombea, tukiwa tunatoka makao makuu ya wilaya (Ifakara), tulipofika hotelini kata ya Mlimba ugomvi uliibuka miongoni mwa watia nia.

Msingi wa ugomvi huo uliozaa uhasama, ilikuwa mmoja wa watia nia kumrushia maneno mwingine kiasi cha kutaka kupigana; sababu kubwa ni kwamba sote tuliwahi kufika katika kambi yaani hoteli ambayo tulitakiwa kuwepo kabla ya kwenda vijijini kwa wanaCCM wenzetu kujinadi, lakini kuna mtia nia ambaye alichelewa zaidi ya saa masaa matano kufika tulipotakiwa kuwepo yaani hapo kwenye kambi, kitendo ambacho kilitafsiriwa kama alikuwa anafanya kampeni.

Aidha mtia nia huyo aliambiwa na mtia nia mwenzake (huyo waliyekuwa wakigombana) kwamba yeye hakupaswa kugombea Jimbo la Mlimba, kwa sababu makazi yake ni kata ya Mkamba, ambayo iko katika Jimbo la Kilombero.

Kama hiyo haitoshi, katika kura za maoni kulikuwa na malalamiko kuwa baadhi ya watia nia ni kama walipandikiza watu, kwamba yuko mtia nia ambaye kulipokuwa na mkutano wa wana CCM ili kusikia sera za watia nia, aliposimama yeye alikuwa anashangiliwa sana, na wakati mwingine kama yeye alikuwa wa kwanza kuzungumza, basi baada ya yeye kuongea, wengi wa wana CCM walikuwa wakiondoka kwenye mikutano.

OFISI YA CCM WILAYA KUTOCHUKUA HATUA

Licha ya malalamiko hayo kuwasilishwa wilayani, hapakuwa na hatua za haraka zilizochukuliwa. Kitendo hiki kiliendelea kuimarisha ufa ndani ya CCM hasa miongoni mwa wagombea (watia nia).

KURA ZA MAONI NA BAADA YA MATOKEO

Baada ya kumaliza kujinadi, uchaguzi ulifanyika katika vituo mbalimbali huku tukiambiwa tuweke mawakala katika maeneo ya kupigia kura. Wengi tulifanya hivyo. Kwenye kura za maoni, miujiza ilianza kutokea, kwamba katika kata fulani, wakala wako anakwambia umepata kura kiasi fulani, wilayani tulikuwa tukiona kura tofauti. Wengi tulipohoji tuliambiwa tutulie kungekuwa na vikao kujadili kama kuna kasoro na namna gani twende sawa.

NINI KILITOKEA?

Hadi leo hakuna kikao kilichoitishwa na wilaya kujadili malalamiko ambayo watia nia waliyawasilisha wilayani. Matokeo yake ni nini? Ukweli ni kwamba wapo wanaCCM wengi walijitoa CCM moja kwa moja na kuungana na upinzani, huku wengine walifanya hivyo kwa siri, sababu kubwa ni kwamba waliona ofisi ya Wilaya haikuwatendea haki kwa kutofanya kikao, kitendo ambacho kilitafsiriwa kama walikuwa na mgombea wao waliyemtaka, japo ofisi ya CCM wilaya Kilombero imekuwa ikikanusha hilo.

Anguko la CCM katika Wilaya ya Kilombero lilitokana na dharau; baadhi ya viongozi kuamini kwamba wanaweza kwenda mbele hata kama watawadharau au watayadharau malalamiko ya watia nia wengine.

USHAHIDI WA HILI

Ni mimi, Dismas Lyassa pekee ndiye niliyeshiriki kwenye mikutano ya kuwanadi wagombea, niliwasha gari yangu kutoka Dar es Salaam hadi Ifakara kwenye kumnadi Abubakar Assenga. Wengine walikuwa na sababu zao zikiwamo kutofurahishwa na mchakato mzima wa upatikanaji wa wagombea.

INAWEZEKANAJE BIBI AZIMINA A. MBILINYI AKATENGULIWA HARAKA HIVI
BAADA YA KUHAMISHIWA BAGAMOYO?

Kama nilivyotangulia kusema, natoa taarifa hii kama mtu ambaye nayajua mazingira ya kushindwa kwa CCM yangu katika uchaguzi, mtu ambaye najua kwanini CCM tulishindwa mwaka 2015. Huenda wengine waliona tofauti lakini haya ni kwa namna ninavyoona mimi kama Dismas Lyassa.

Kwa bahati nzuri katiba inaruhusu kila mtu kutoa maoni yake katika jambo kwa kadri anavyoona yeye, ndivyo ninavyoona mimi kilichotokea kwenye uchaguzi 2015, wengine wanaweza kuwa na maoni tofauti, nao waheshimiwe kwa sababu kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni kwa kadri anavyoona yeye.

Katika mitandao ya kijamii, yuko mwanasiasa mmoja maarufu nchini anahusisha kuanguka CCM eti kwa sababu alishindwa kuisaidia CCM kushinda. Kwa mazingira niliyoyaeleza wagombea wetu wangewezaje kushinda? Mfano katika kijiji cha Mofu pekee, zaidi ya viongozi 15 wa matawi na taasisi mbalimbali walihama CCM na kwenda upinzani, jumatano ya kuelekea jumapili ya uchaguzi. CCM haijapoteza majimbo ya Mlimba na Kilombero pekee, kwa hiyo sioni mantiki ya kuhusisha haya ya Azimina na siasa.

Wapo wanaoweza kusema aaah sasa mbona Rais amechukua maamuzi saa chache baada ya CCM kushindwa kesi za kupinga matokeo….jambo humtokea mtu wakati wowote, iwe anatoka usingizini…kazini nk…mtu anaweza kufa hata kama anatoka nyumba ya ibada…huwezi kusema si angesubiri kwanza.

Bibi Azimina A. Mbilinyi

Akiwa Mkurugenzi Kilombero niliwahi kuwasiliana nae kwa simu/whatsap kuhusu kijana mmoja aliyesomeshwa na mjane. Kwamba, kijana huyo alipata ajira katika halmashauri hiyo kama afisa maendeleo, lakini aliporipoti akaambiwa arudi atatafutwa. Nilimpigia Azimini mara kadhaa kujua juu ya suala hili na majibu yalikuwa ni kwamba anafanyia kazi, huku kukiwa na utata wa kama nafasi hiyo ambayo ilikuwa ni kwa mujibu Tume ya Utumishi wa Umma kama ilikuwa bado au la.

Maana yake ni nini? Ikiwa mimi najua hili, je wewe ulikuwa unajua? Kumbe ni kwamba sio sahihi kuzungumza mambo tusiyoyajua. No research, no right to SPEAK. Huyo kijana ambaye amesomeshwa na mjane, hadi leo hana kazi, anaishi kwa mama yake kwenye nyumba moja inayotazamana na hoteli ya Landmark Ubungo, Dar es Salaam. Hana ajira, licha ya kwamba tayari alishaipata, ameambiwa asubiri, leo ni zaidi ya miezi nane tangu aambiwe asubiri, hakuna jibu lililonyooka.

Ambacho nataka umma ufahamu ni kwamba ukweli kuhusu majimbo ya Kilombero na Mlimba ni huo, kwamba wapo wana CCM walioshirikiana na vyama vya upinzani ili tu ishinde kwa sababu waliamini hawakutendewa haki na chama hasa pale kilipofunga milango ya kuwepo kwa mikutano ya suruhu.

NILIWAHI KUSHAWISHI WANACHAMA NA VIONGOZI WA CCM KUWAONDOA VIONGOZI WA WILAYA LAKINI NIKAOMBWA NIACHANE NA HILO ILI LISILETE ATHARI KWA CHAMA

Kama mtakumbuka baada ya uchaguzi mkuu, niliongoza mpango wa kufufua CCM Kilombero, niliwasiliana na viongozi wa kata zote, matawi na wanachama; azma ilikuwa kwanza ni kuwaondoa viongozi wa wilaya, hata hivyo nilishawishiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa chama kwamba suala hilo lingeweza kuharibu zaidi, kwa hiyo niwe na utulivu na nifanye mawasiliano na wote ambao nilishawasiliana nao ili kuahirisha chochote nilichokuwa nimekipanga.

Nilifanya hivyo, kutokana na kuwatii hasa baada ya kuelezwa njia nyinginezo ambazo zingeweza kuweka mambo sawa ndani ya chama.

Naomba ulimwengu ufahamu kwamba hayo ndiyo yaliyotokea katika majimbo ya Mlimba na Kilombero; shida kubwa ni sisi wenyewe tulishindwa kuungana baada ya kura za maoni, na viongozi hadi leo hawajatuunganisha. 

Kwa kuanguka kwa CCM wa kuondolewa ni viongozi wote wakuu wa CCM Wilaya kutokana na sababu 1.Kushindwa kuwa na mkakati wa kuimarisha chama, hasa kutokana na ukweli kwamba hata wakati wa kura za maoni, wapo wanachama walitoa lawama za wazi kwamba viongozi wa wilaya wamekuwa wazito kutembelea kata na matawi ili kuyaimarisha. 2. Pia hawakuona umuhimu wa kuweka suruhu baina ya watia nia 3. Kuna haja ya viongozi wakuu wa chama chetu (CCM) kuomba kibali ili waingilie mawasiliano ya simu ya viongozi wa CCM Wilaya Kilombero, hasa laini za tigo na Airtel, kuanzia Julai 2015hadi Oktoba 2015. Nafahamu ninachokiongea ndio maana sijataja laini za simu za makampuni mengine.

TUUNGANE KUIMARISHA NCHI

Kutangaza mambo tofauti ni kupotosha umma bila sababu, tuungane na Rais katika kuimarisha nchi. Miaka mingi tumekuwa tukililia Rais mchapakazi, sasa amepatikana ni vema kumtia moyo.
Kwani hujawahi kuwa na rafiki, halafu ukabini kwamba haikuwa sahihi kuwa nae? 

Ni mambo ya kujitafakari badala ya kulaumu.

Tanzania kwanza; tuungane kuijenga nchi yetu.

Wako katika ujenzi wa taifa


Dismas Lyassa
0754498972
0712183282
Taarifa hii nimeitoa leo Agosti mosi, 2016

****mwisho****