Lugha za vibandiko kwenye bodaboda, daladala, bajaj, guta, malori...

Maneno kwenye guta
Gazeti la MTANZANIA katika utafiti katika baadhi ya mikoa likiangalia vijana waendesha bodaboda wanapendelea nini zaidi katika kuongeza mbwembwe katika biashara zao, lilibaini kuwa ni maandishi yenye kuvutia katika mapepe ya pikipiki zao.

Kila mmoja anashindana na mwenzake kuweka jina alipendalo ambalo wakati mwingine humjengea umaarufu kupitia maneno hayo katika pepe.

Dar es Salaam

Baadhi ya vijana katika pikipiki zao walikuwa wameandika kama ifuatavyo:
 • Kitambi bila Yesu?
 • Mkanye mkeo bodaboda si yangu.
 • Kazi mbaya ukiwa nayo.
 • Ukikosa tumaini kula, kula tumbo.
 • Ukitaka kujua njia ya mkato kula nauli.
 • Ukitaka kusahau shida vaa viatu vinavyokubana.
 • Mapenzi kipaji si wote wanaojua
 • Usijisifu una mimba, msifu na aliyekupa mimba.
 • Yatima hadeki.
 • Hata bibi alikuwa bikra.
Hivyo ndio vibwagizo vya waendesha bodaboda jijini, ukisoma mwenyewe unacheka kwanza kisha unapanda pikipiki yake kama umevutiwa.

Mtwara
 • Kunenepa wakati nakudai ni dalili ya dharau.
 • Kunya anye kuku akinya bata kaharisha.
 • Ukikosea kujenga utabomoa, ukikosea kuoa utajuta.
Tabora
 • Kikubwa pesa ya bosi kwanza
 • Ulifikiri kumwambia baba yako hello kwenye simu ndio heshima.
Morogoro
 • Dalalila ange ane dibwe (yaani mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio)
 • Nyuki hakumbatiwi.
 • Usiyempenda kaja.
Dodoma
 • Safari za nje tuachieni sisi.
 • Mchezo wa mapenzi hauhitaji hasira.
Kagera
 • Kuku kuku, jogoo jina.
 • Gari bovu linavutwa kwa gari zima.
Wasomaji wa vituko vya bodaboda hizo ni mbwembwe kwa baadhi ya mikoa lakini mikoa yote vijana wanaweka maneno katika mapepe. Maneno hayo wanayatumia katika maisha yao ya kila siku na yanaashiria kwamba waendesha bodaboda wengi ni vijana. 

Yako maneno mengi yanaandikwa yakiwa na maana kwa mwendeshaji wa bodaboda husika kama vile kuandika Jembe katika pepe lake. Nilipofuatilia nilibaini anajiona mshindi, ni mnywaji mzuri wa viroba na aliwahi kupata ajali akiwa amekunywa viroba. Kijana alirushwa na gari maeneo ya Mtoni Mtongani lakini alipokuja kuokotwa katika mtaro alikutwa akiwa hana jeraha. Aliondoka na bodaboda yake hadi Kiwalani, alijiona mzima hakufika hata hospitali japo pikipiki ilikuwa imeharibika sana. Kila alipokuwa akiulizwa kuhusiana na ajali yake alikuwa anamalizia na kibwagizo ‘mimi Jembe’ ndipo wenzie walipoanza kumuita hivyo. Kijana anasahau kwamba majeraha yanayoweza kuwa ndani na baadaye yakatokea madhara makubwa hasa kichwani.

Kila aliyeandika anamaanisha nini anachosema hivyo mapepe ya kila bodaboda yana maana kubwa.

wavuti.com imetafuta picha mtandaoni zenye misemo mbalimbali kwenye vyombo vya usafiri na usafirishaji na kupata hizi....