Marehemu Rais Jumbe: Mahojiano ya Mei 2002; Jicho la Lissu; Taazia ya Moh'd Said na Makala 3 za Mihangwa

Apr 06, 1972 - Zanzibar City, Zanzibar, Tanzinia - SHEIKH ABOUD JUMBE and JULIUS NYERERE at the funeral of the first President of Zanzibar ABEID KARUME, who was assassinated by four gunmen. Exact date unknown..(Credit Image: KEYSTONE Pictures/ZUMAPRESS.com).
Mei 18, 2002, aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Yussuf Kajenje, alifanya mahojiano na marehemu Aboud Jumbe nyumbani kwake Mji Mwema Kigamboni.
Mahojiano hayo yalichapishwa katika gazeti la Mtanzania Jumapili, Mei 26, 2002, ambapo yalikuwa hivi;
“Siku hizi sisikii vizuri na pia sioni sawasawa. Hivyo niwie radhi kwa mapungufu yatakayojitokeza wakati wa mazungumzo yetu,” 
alianza kusema Aboud Jumbe wakati akikaa vizuri katika moja ya masofa yaliyokuwa sebuleni baada ya kutoka mahali ambako bila shaka alikuwa amejipumzisha.
Kwa wakati huo akiwa na zaidi ya miaka 80, Aboud Jumbe alionekana wazi kuwa umri ulikuwa umeanza kumtupa mkono, alikuwa amezeeka.

Hata hivyo, mbali na uzee huo bado alikuwa na uwezo mkubwa kufuatilia mambo yanayotokea duniani na alionekana kumbuka mengi aliyokutana nayo tangu enzi zake za utotoni.
“Tangu nilipotoka serikalini mwaka 1984, nimekuwa nikifanya shughuli mbalimbali za kujipatia riziki, na kutafuta mwisho mwema kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Aboud Jumbe.
Akizungumzia juu ya maisha yake tangu utotoni, Aboud Jumbe ambaye alizaliwa Zanzibar Juni 14, 1920 alisema mambo mengi yalimtokea kwa namna tofauti na jinsi alivyotarajia.
“Utastaajabu kwamba katika maisha yangu yote sikuwahi kuwa na mpango. Na kama ulikuwapo, basi haukufanikiwa.
“Kwanza nikiwa na miaka 10 nilipelekwa kusoma madrasa, lakini nikatolewa kwa nguvu na askari waliokuwa wakipita kuwakamata watoto wenye umri mkubwa wa kwenda shule. Nilipenda sana kuendelea na madrasa, lakini haikuwezekana.
“Ingawa nilipenda madrasa, sikutoroka katika shule ya Mnazi Mmoja (sasa inaitwa Ben Bella) ambako nilikuwa nimepelekwa kusoma. Nilifanikiwa kumaliza darasa la nane katika shule hiyo,” alisema Aboud Jumbe.
Alisema kwamba siku moja asubuhi akiwa anafua nguo, alifahamishwa na mkuu wa shule hiyo ambaye alikuwa mzungu kwamba alikuwa amefaulu mtihani, hivyo alitakiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule hiyo.

Alisema akiwa Makerere ndiko alikopata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Wote tulikuwa tunasomea ualimu na tulielewana sana,” alisema

Aboud Jumbe alisema kwamba mara baada ya kuhitimu Makerere, alifundisha kwa miaka 15. “Mwaka 1958, kiongozi wa chama cha ASP, Sheikh Thabit Kombo, alinijia akaniomba nisaidie harakati za chini kwa chini za kupambana na utawala wa kisultani.”
“Nilishauriana na mke wangu, mama, pamoja na dada yangu kuhusu uamuzi wa kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa ikinipa mshahara wa Sh 1,500. Walikubali, nami nikaingia katika harakati za chini kwa chini ambazo hazikuwa na mshahara mkubwa.”
Aboud Jumbe alisema kwamba mapinduzi yalipofanyika mwaka 1964, alipata wadhifa wa kuwa Katibu wa Mipango mpaka mwaka 1972 wakati alipochaguliwa kuwa Rais wa SMZ. “Kwa mara nyingine hilo halikuwa katika matarajio yangu.”

Akizungumzia juu ya maisha yake ya ndoa, Aboud Jumbe alisema kwamba alioa mke wa kwanza mwaka 1948, miaka mitatu tangu alipoanza kazi ya ualimu. Miaka minne baadaye, 1952, alijaliwa kupata mtoto wa kwanza. Mkewe huyo wa kwanza ambaye alifariki mwaka 2000, alizaa watot o wanane, wawili wa kike, na sita wa kiume.

Aboud Jumbe alisema kwamba baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, alioa tena mke mwingine ambaye alizaa watoto watano wa kiume. 
“Baadaye tuliachana, kisha nikaoa mke mwingine wa kutoka Pemba ambaye ndiye ninayeishi naye sasa (wakati wa mahojiano), na amezaa watoto wawili, wa kike na wa kiume.”
Mbali na wake zake hao watatu, Aboud Jumbe alioa mwanamke mwingine ambaye kwa kauli yake ndiye aliyekuwa akisafiri naye mara kwa mara katika safari za kikazi. Alizaa naye watoto watatu. Kwa ujumla alioa wake wanne, na hadi mwaka 2002 alikuwa amejaaliwa kupata jumla ya watoto 18.

Namna alivyojiuzulu

Akizungumzia juu ya kujiuzulu kwake mwaka 1984, Aboud Jumbe alisema kuwa kulitokana na baadhi ya viongozi aliokuwa nao serikalini Zanzibar kumfitini kuwa anataka kuiuza nchi.

Alisema viongozi hao wafitini (anamtaja Maalim Seif) walieneza uvumi kwamba kulikuwa na mpango wa kutaka kuipindua serikali ili kuua Muungano. “Hata hivyo, viongozi hao baadaye walipata matatizo nao wakatoka serikalini kwa kufukuzwa.
“Siku moja kabla ya Sherehe za Mapinduzi ambazo zilikuwa zimepangwa kufanyika Pemba, walikuja wajumbe wawili wa Baraza la Mapinduzi wakaniambia kuwa kule Pemba hali haikuwa nzuri, na kwamba kungetokea maasi.
“Nilimpa taarifa hizo Mwalimu Nyerere, naye akaja Zanzibar kama ilivyokuwa imepangwa bila kujali taarifa nilizokuwa nimempelekea,” alisema.

Aboud Jumbe alisema kuwa katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika Dodoma mwaka 1984 kujadili hali ya machafuko ya kisiasa Zanzibar, hakuna aliyejua kwamba angechukua uamuzi wa kujiuzulu. “Hata Mwalimu Nyerere hakujua”.
“Nilichukua uamuzi wa kujiuzulu kwa sababu masharti yangu matatu ya kufanya kazi popote pale yalikuwa yamevunjwa,” alisema.

Alisema kuwa sharti lake la kwanza kufanya kazi ni lazima isiwepo hali ya kutia shaka, na pawepo uwazi na ukweli.
“Sharti la pili ni kuwa na uwezo kimwili na kiakili, na si kuendeshwa na kufanywa kama sanamu,”.
Alitaja sharti la tatu ni kuwa ni lazima wote wakubaliane kufanya kazi pamoja, jambo ambalo Aboud Jumbe alisema masharti hayo yote yalivunjwa, hivyo aliamua kujiuzulu.
Alipojiuzulu alitaka kurudi kwao Zanzibar, lakini kwa maelezo yake Mwalimu Nyerere alimzuia. “Nyerere alinishauri nisirudi Zanzibar wakati huo kwa sababu hali haikuwa nzuri. Alisema nisubiri mambo yatulie kwanza,” alisema.
Baada ya kujiuzulu, mbali na mambo mengine ambayo alikuwa akiyafanya ni pamoja na kuandika vitabu. “Nimekuwa nakijishughulisha na kazi ya uandishi wa vitabu. Mpaka sasa (wakati wa mahojiano) nimekwishaandika vitabu vinne; cha kwanza ni ‘Safarini’ ambacho maudhui yake ni kwamba binadamu wote katika maisha tuko safarini.”

Aboud Jumbe alisema aliamua kuandika kitabu hicho kwa lengo la kuikumbusha nafsi yake pamoja na binadamu wengine mambo ya kufanya ili kupata mwisho mwema kwa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu.
**********************************
Jan 01, 1972 - Zanzibar City, Zanzibar, Tanzinia - SHEIKH ABOUD JUMBE giving a speech at a rally. Exact date unknown..(Credit Image: KEYSTONE Pictures/ZUMAPRESS.com)

Jicho la Lissu


Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia. Akiwa na miaka 96, Jumbe aliishi muda mrefu sana kwa kigezo chochote kile, anaandika Tundu Lissu.

Alikuwa mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya Januari 1964.

Alikuwa pia mwasisi wa Muungano ulioizaa Tanzania miezi michache baadaye. Baada ya Sheikh Abedi Amani Karume kuuawa mwezi Aprili 1972, Jumbe aliteuliwa kuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, na alishikilia madaraka hayo hadi Januari 1984.

Wasomi wa Muungano wameandika kwamba, wakati Rais Karume anauawa, uhusiano wake na Mwalimu Julius Nyerere ulikuwa umeharibika kiasi kwamba Jumbe (kwa upande wa Zanzibar) na Bhoke Munanka (kwa upande wa Tanganyika) ndio walikuwa kiunganishi cha mawasiliano kati ya Mwalimu na Karume.

Hii pengine ndio sababu Mwalimu alitumia ushawishi wake kuhakikisha Jumbe anateuliwa kumrithi Karume.

Hata hivyo, Jumbe atakumbukwa zaidi na historia kwa upinzani wake kwa mfumo wa sasa wa Muungano kuliko, pengine, kwa jambo jingine lolote.

Jumbe alikuwa mwanasiasa wa kwanza, baada ya era ya (uongozi wa) Karume, kutambua kwamba muundo wa serikali mbili ulikuwa umeipokonya Zanzibar mamlaka yake na kuyahamishia Tanganyika.

Alikuwa wa kwanza kutambua kwamba, kuzaliwa kwa CCM katika context (mtazamo) ya Muungano, kulimaanisha mwisho wa mamlaka yaliyokuwa Zanzibar chini ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964.

Sio tu alitambua bali pia Jumbe alichukua hatua kupinga Zanzibar kupokonywa mamlaka yake hayo.

Ili kufanikisha azma yake, Jumbe alilazimika kumwachisha kazi Mwanasheria Mkuu wake aliyempewa na Mwalimu Nyerere, Damian Lubuva, na kumwajiri Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy, Raia wa Ghana, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Kwaw Swanzy ndiye aliyeandaa ‘hati ya mashtaka’ dhidi ya Muungano iliyokamatwa na watu wa usalama wa Mwalimu na baadaye kutumika kumsulubu Jumbe kwenye kikao cha NEC ya CCM Dodoma Januari 1984. Kwa sababu ya upinzani huo, Jumbe aling’olewa madarakani pamoja na Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Kwaw Swanzy alitangazwa kufukuzwa nchini.

Mwalimu akatangaza ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar na Wazanzibari wengi wapinzani wa Muungano, kama Mwanasheria Mkuu wa kwanza Wolfgang Dourado, kuwekwa kizuizini.

Miaka 10 baada ya kuondolewa madarakani, Alhaj Aboud Jumbe alichapisha kitabu chake juu ya Muungano, ‘Miaka Thelathini ya Dhoruba’, ambako aliweka bayana ugomvi wake na Mwalimu juu ya Muungano.

Jumbe ni kiongozi pekee wa juu wa rika la wapigania uhuru wa Tanzania kuandika memoirs zake juu ya Tanzania na matatizo ya Muungano wake.

Hata Mwalimu hakufanya hivyo na alikufa na siri zake juu ya mambo mengi makubwa yalitokea wakati wa utawala wake.

Kwangu mimi, hii ndio merit (faida) kubwa na mchango mkubwa wa Alhaj Aboud Jumbe kwa kizazi cha sasa na vijavyo Tanzania.

Alikuwa na ujasiri wa kusema na kuandika juu ya ‘The Forbidden Subject’, tena katika kipindi cha Mwalimu Nyerere ambapo ujasiri wa aina hiyo ulikuwa ni jambo la hatari kubwa.

Kwa sababu hiyo hiyo, Jumbe alilazimika kuishi theluthi ya mwisho ya maisha yake ‘kifungoni’ Mji Mwema, Kigamboni, ambako alipelekwa mara baada ya kung’olewa madarakani mwaka ’84.

Sikuwahi kubahatika kuonana na Alhaj Aboud Jumbe wakati wa uhai wake. Hata hivyo, nimejifunza mengi sana kutoka kwake, hasa ujasiri wa kuuhoji Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Jumbe amekuwa na ushawishi mkubwa sana kwenye mjadala wa Muungano kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.

Ninadiriki kusema kwamba, hoja ya Serikali Tatu ilianzia kwa Jumbe. Roho yake ilikuwa kila mahali wakati wa mchakato wa Katiba Mpya kati ya 2011 na 2014.

Kivuli chake kilikuwa kila mahali wakati wa Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014. Pengine kuliko hata Mwalimu Nyerere, Jumbe ndiye aliyetufundisha kuufahamu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Atakumbukwa kama mmoja wa waTanzania maarufu na wapigania uhuru wakubwa wa Zanzibar ya baada ya Muungano.

Adieu Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi. Adieu Mtanzania jasiri. Adieu shujaa wa uhuru wa Zanzibar.
  • Imeandikwa na Tundu Lissu (Mbunge)
**********************************


TAAZIA
ABOUD JUMBE 1920 - 2016


George Githii alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Nation. Githii aliandika taazia ya Jomo Kenyatta wakati Kenyatta yu hai hajafa. Bahati mbaya sana kwa Githii, Kenyatta akapata taarifa kuwa kaandikiwa taazia mapema inamsubiri afe tu Githii aichape. Kenyatta hakufurahishwa na habari ile hata kidogo na inasemekana alimwita Githii Gatundu kwa ‘’mazungumzo.’’ Kenyatta hakupendezwa na kitendo kile kwa kuwa yeye akiogopa kifo na akiogopa kukutana na malaika wa mauti, hakutaka mtu amkumbushe kifo.

Aboud Jumbe alikuwa na yakini ya kukutana na Mola wake na hakusubiri mtu kumkumbusha hilo. Aboud Jumbe alijikumbushe mwenyewe kifo na akaandika kwa mkono wake mwenyewe usia wake na vipi angependa mazishi yake yawe. Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya viongozi hawa wawili. Aboud Jumbe alikitegemea kifo muda wowote na akajitayarisha na siku atakayokutana na Mola wake. Usia wa Jumbe vipi azikwe umewashtua wengi katika serikali ya Tanzania kwani alikataa kuzikwa nje ya taratibu za Kiislam. Kwa ajili hii basi Aboud Jumbe alizikwa kama Uislam ulivyofundisha na kuwa kiongozi wa kwanza wa juu katika historia ya Tanzania kuhitimishwa nje ya utaratibu uiiozoeleka wa ‘’sherehe.’’

Nimejuana na Mzee Jumbe katika takriban miaka ishirini na tano ya mwisho wa maisha yake. Huu usia ambao umezunguka sana katika mitandao ya jamii na kuzungumzwa sana mara tu ulipotolewa hadharani, mimi na wenzangu tuliusikia kutoka kinywani kwake mwenyewe. Mimi na wenzangu tulikuwa nyumbani kwake Mji Mwema na Mzee Jumbe akawa anatukumbusha sisi kama wanae hatari ya mja kutekwa na dunia akaisahau akhera kama vile iko mbali sana. Hiyo ndiyo siku alipotueleza kuhusu usia huu. Alituambia kuwa baada ya kuandika usia wake akamwita kiongozi mmoja wa juu katika Serikali ya Muungano kumfahamisha kuhusu usia ule na vipi angelipenda azikwe umauti utakapomfika. Alimweleza kuwa yeye angependa kuzikwa kama wanavyozikwa Waislam kwa mujibu wa sharia na akamsisitizia kuwa asingependa afanyiwe yale yaliyoko nje ya Uislam, mojawapo likiwa jeneza lake kufunikwa bendera. Mzee Jumbe akatueleza kuwa jibu alilotoa yule kiongozi lilimshangaza. Anasema yule kiongozi alimwambia Mzee Jumbe kuwa asiwe na hofu yote aliyoagiza katika usia wake watatekeleza. Mzee Jumbe akasema kwa masikitiko kuwa yeye hakutegemea jibu hili peke yake bali alitegema kuwa na yeye kwa kuwa ni Muislam angemuunga mkono na kusema kuwa hata yeye angependa kuzikwa kama Mtume (SAW) alivyofundisha. Hili kiongozi yule hakulisema. Msisitizo wake ulikuwa kwenye utekelezaji wa usia wa Mzee Jumbe, yeye atazikwa kwa, ‘’sherehe’’ na bendera juu ya jeneza lake. Hivi ndivyo iliyotokea miaka michache baadae. Kiongozi huyu alifariki ghafla na akazikwa kwa, ‘’sherehe,’’ na jeneza lake likafunikwa bendera ya CCM. Bahati mbaya sana kwake usia wa Mzee Jumbe haukumzindua.

Kenyatta alisoma taazia yake mwenyewe yungali hai akaghadhibika akamuita George Githii Gatundu kwa makemeo. Kiongoi huyu aliusoma usia wa Mzee Jumbe lakini yeye aliona haumuhusu. Hivi ndivyo Mzee Jumbe alivyokuwa, tofauti mno na viongozi wenzake. Kuna mwandishi mmoja katika taazia aliyomwandikia Mzee Jumbe, kwa kutoelewa maisha ya Mzee Jumbe kawapa wasomaji wake picha ya kuwa Mzee Jumbe amekufa akiwa ‘’mpweke.’’ Hii si kweli watu walikuwa hawapungui nyumbani kwake Mji Mwema. Nimekuwa nikienda nyumbani kwa Mzee Jumbe mimi na wenzangu mara ambazo hata siwezi kuzihesabu na sikupata hisia hata kidogo kama kuwa Mzee Jumbe alikuwa mpweke. Geti lake lilikuwa wazi ingawa kulikuwa na askari na silaha wakilinda pale. Ukiwa pale nyumbani kwake muda wote utawaona majirani zake wakiingia na kutoka ndoo kichwani wakija kuteka maji, akina mama na watoto mgongoni na wengine wakiwa na watoto wadogo wamewatangulia au wako nyuma yao. Askari walinzi wakiwaachia waingie na kutoka kama watu wa nyumbani. Nyumba ya Mzee Jumbe haikuwa nyumba iliyojiinamia. Sikuenda kwa Mzee Jumbe nikakuta lile geti limefungwa hata siku moja. Nyumba ilizidi uchangamfu kwa wavuvi kuingia na kutoka kuja kufata barafu kwani Mzee Jumbe alikuwa na mtambo wa kisasa kabisa wa kutengenzeza vinoo vya barufu kwa ajili ya uvuvi. Wakati wote wavuvi walikuwa wakipita nyumbani kwake kuja kununua barafu. Siku moja katika mazungumzo Mzee Jumbe katika hulka yake ya kutuchekesha alituambia kuwa yeye hakutaka kuwa tegemezi akae kusubiri hundi ya pensheni maana alisema huenda siku bwana fedha akasahau kukutumbukizia hundi yako. Yeye kwa ajili hii akaamua ajishughulishe kidogo na ndiyo akaleta mtambo wa barafu. Mzee Jumbe akatumalizia kwa kusema alichagua biashara ile ya barafu kwa sababu alijua itawasaidia sana nduguze wavuvi. Si wengi wenye kulijia hili lakini ukweli ni kuwa babu yake mkuu Mzee Othman Kitamaguru aliondoka Mji Mwema na kuhamia Chukwani Zanzibar kuendeleza shughuli zake za uvuvi.

Aboud Jumbe hakuwamo katika mpango wa mapinduzi. Huenda hili likawashangaza watu wengi. Labda kwake yeye hii ni kheri kubwa sana na ilimpa utulivu wa nafsi kwani wale wachache kutoka Zanzibar na Tanganyika waliohusika na mipango ya mapinduzi, hawakutaka baada ya mapinduzi majina yao yanasibishwe na mapinduzi yale. Kwani ni muda mfupi tu baada ya mapinduzi, mauaji na unyama uliofanyika Zanzibar ukajulikana dunia nzima. Kulikuwa na kambi Kipumbwi, nje kidogo ya Tanga ambapo kuliwekwa mamluki wengi wao Wamakonde kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura. Hawa ndiyo waliovushwa na kuingia Zanzibar kusaidia mapinduzi na inasemekana kuwa hawa Wamakonde waliua watu wengi sana hasa Waarabu. Kila Mzanzibari kiongozi niliyezungumzanae kuhusu mamluki hawa au hata kuwapo kambi yao Kipumbwi alisema hana taarifa hizo. Lakini kwa sasa hii si siri tena kwani kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,’’ kimeeleza kila kitu. Aboud Jumbe bila shaka alishukuru kuwa hakuwa na mkono katika mpango huu kwani imeshadhihirika hivi sasa kuwa mauaji yale yalikuwa mauaji ya kimbari.

Swali ambalo litakuja ni kuwa nani aliidhinisha kuwepo kwa kambi hii katika ardhi ya Tanganyika? Baada ya swali hili kujibiwa ndipo yatafuata maswali mengine ambayo historia ya Zanzibar na Aboud Jumbe akiwa mmoja wa walioandika historia hii ataweza kutupa majibu. Hivi ni kweli Mwalimu Nyerere alisaidia kuipindua serikali ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte kwa kuwa ilikuwa serikali dhalim au kulikuwa na sababu nyingine ambayo wanamapinduzi hawakuijua?

Inajulikana wazi kuwa mgongano wa Nyerere na Aboud Jumbe umetokana na Jumbe kuhoji muungano. Hiki ni kisa maarufu. Bahati mbaya hakuna mwandishi aliyekwenda zaidi ya hapo na kueleza kwa nini suala la Zanzibar kuwa na uhuru lau kidogo wa kujiamulia mambo yake likawa jambo kubwa sana kwa Nyerere? Suala la Zanzibar kuwa huru lilikuwa jambo zito kwa Nyerere kwa sababu ikiwa Zanzibar itatoka mikononi kwake itakuwa yeye alifanya kazi ya bure kusaidia mapinduzi ya Zanzibar. Kwa Aboud Jumbe kuitaka iwe huru pawepo na serikali tatu hii ilikuwa vita ya wazi dhidi ya Nyerere. Lakini muhimu kujiuliza Aboud Jumbe alifika vipi katika hali ile ya kuidai Zanzibar kutoka kwa Nyerere? Katika kitabu chake Dr. Harith Ghassany anaeleza Ali Muhsin anavyoieleza Zanzibar kama Ngome ya Kusini ya Uislam ambayo maadui wa Uislam walidhani wakiiangusha ngome hiyo basi na Uislam nao utaanguka. Ilimchukua muda gani kwa Aboud Jumbe na yeye kuliona hili ambalo wale waliopinduliwa waliliona zamani? Ni kweli kuwa Zanzibar ile kabla ya mapinduzi si Zanzibar hii ya mapinduzi.

Ili kumwelewa Aboud JRaismbe hadi kufikia pale ambapo aligongana na Nyerere ni vyema kwanza ijulikane kuwa Aboud Jumbe aliupenda Uislam wake kama vile Nyerere alivyokuwa anaupenda Ukatoliki wake ila tofauti kati yao ilikuwa moja tu. Wakati Nyerere alifanya mipango yake ya kusaidia dini yake kwa usiri wa hali ya juu, Jumbe yeye alifanya juhudi zake waziwazi bila ya kificho. Aboud Jumbe alisaidia kuanzishwa kwa Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA) mwaka wa 1984. Hii ni miaka 12 baada yeye kuwa rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania. Historia ya Nyerere inaonyesha kuwa hapajatokea kiongozi katika serikali yake akajinasibisha na Uislam na Waislam akanusurika. Aboud Jumbe kwa kule kujinasibisha na Uislam alikuwa tayari kwa fikra ya Nyerere kamtangazia vita. Nyerere alitoa, ‘’Presidential Notice,’’ akionya kuhusu viongozi wa serikali kufanya shughuli za dini.

Kwa hakika haikuwa ‘’viongozi wa serikali,’’ onyo lile lilikuwa kwa Makamu wa Rais Aboud Jumbe moja kwa moja. Uislam lilikuwa suala nyeti sana kwa Nyerere na alitumia nguvu za dola kuwamaliza wote walijaribu kuutia nguvu Uislam Tanzania. Sheikh Hassan bin Amir, Tewa Said Tewa, Bi. Titi Mohamed, Abubar Mwilima na Prof. Kighoma Malima wote hawa walishughulikiwa barabara na wote wakajikuta nje ya siasa za Tanzania, achilia mbali wale waliowekwa kizuizini. Uislm lilikuwa jambo linalotisha na hakuna kiongozi aliyekuwa na ujasiri wa kuleta agenda hiyo mezani.

Aboud Jumbe alikuwako wako katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM siku Abubakar Mwilima alivyomkabili Nyerere uso kwa macho kama Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM na kumuuliza imekuwaje Waislam wako nyuma wakati wenzao wanasongambele. Nyerere alikuwa kimya. Ukumbi mzima vilevile ulikuwa kimya. Wajumbe walikuwa wameshika roho zao mkononi. Swali hilo hakuna aliyekuwa hajui kuwa ni mwiko mkubwa kuulizwa. Kwa sekunde chache ilikuwa kama vile dunia imesimama, haizunguki, imetuwama mahali pamoja. Nyerere aliahirisha kikao wajumbe wakanywe chai. Aboud Jumbe alikuwako na alishuhudia jinsi wajumbe wa mkutano walivyomkimbia Mwilima. Hakuna aliyetaka kumkaribia wala kuongea na yeye. Mwilima alikaa mezani akinywa chai peke yake. Wenzake wote hata wale marafiki zake wa siku zote walimkalia mbali. Waliporudi kikaoni Nyerere aliendelea na mkutano kama vile hakuna kilichopitika. Nyerere hakutaka kulijibu swali la Sheikh Mwilima.
Haukupita muda Sheikh Abubakar Mwilima aliitwa kuhojiwa kuhusu kuuza dola za Kimarekani kinyemela. Haukupita muda na yeye kama wenzake waliomtangulia akajikuta yuko nje.

Siku moja Mzee Jumbe alitupa kisa cha, ‘’The Long Letter.’’ Hii barua ndefu ilikuwa ile barua iliyotayarishwa na Bashir Swanzy Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ndani yake yakiwa mashtaka dhidi ya Muungano kuhoji uhalali wa wa Muungano. Barua hii ilikuwa imekusudiwa iwasilishwe kwenye Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Mzee Jumbe alikuwa akitualika mara kwa mara nyumbani kwake na yeye akipenda sana kuandalia. Mzee Jumbe akikualika nyumbani kwake kula, inabidi ujitayarishe vyema kwani alikuwa akichafua uwanja. Ilikuwa katika moja ya barza zetu kama hizi ndipo siku hiyo akatuhadithia yale yaliyotokea Dodoma kati yake na Nyerere kupelekea yeye kujiuzulu nyadhifa zake zote. Mzee Jumbe alikuwa ana namna ya kuhadithia jambo hata liwe zito vipi, wewe msikilizaji likakufikia kwa wepesi na wakati mwingine katika njia ya kukufanya ucheke. Alikuwa keshatuhadithia jinsi mashtaka yale yalivyokuwa yametayarishwa na hapo ndipo alipokuja na jina hilo la, ‘’The Long Letter,’’ na sisi ikawa huo waraka tunauita, ‘’Long Letter,’’ kama yeye mwenyewe, katika njia ya utani alivyopenda kuita.

Mzee Jumbe alipokuwa anaeleza kupotea kwa waraka ule na ukaibuka mikononi kwa Nyerere Dodoma, Mzee Jumbe alikuwa akitushekesha alivyokuwa akitueleza jinsi Nyerere alivyoinga’nga’nia, ‘’The Long Letter,’’ na akawa anasoma vipande alivyovipenda yeye na Jumbe akimwambia endelea na soma na mahali pengine, Nyerere alivyokuwa hataki akishikilia hapo hapo kama mtoto mdogo aliyepewa pipi na sasa anahisi anataka kunyang’ang’anywa. Huku tukishusha biryani na juisi baridi, hakika ilikuwa ni burdani ya aina yake. Mzee Jumbe akicheka na sisi wasikilizaji tukicheka pia. Mzee Jumbe Uislam na kukubali qadir ya Allah kulikuwa kumemweka pazuri sana. Mzee Jumbe hakuwa mtu aliyejuta kutoka katika uongozi kiasi alikuwa sasa anatushekesha kuhusu madhila ya uongozi. Akawa siku zote tukiizungumza na yeye kuhusu, ‘’The Long Letter,’’ masikitiko yake ni kuwa kuikosa, ‘’The Long Letter,’’ hawezi kuandika kitabu kuhusu matatizo ya Muungano.

Siku zikenda na miaka ikapita. Siku moja tuko kwake akatuangushia bomu lililotuacha midomo wazi. Mzee Jumbe akatuambia kuwa, ‘’The Long Letter,’’ kaiona nyumbani kwake Migombani kwenye, ‘’Study Room,’’ yake. Tulimuuliza Mzee Jumbe kaiona vipi? Yeye akatujibu kuwa na yeye amepigwa na mshangao kama tulivyopigwa sisi. Akatuambia kuwa na keshaanza kuandika kitabu. Siku zile Mzee Jumbe tayari alikuwa keshaanza kupoteza nuru ya macho na akiandika na kusoma kwa msaada wa ‘’lens.’’ Iko siku mimi na mwenzangu sasa tukikihariri mswada wa kitabu cha Mzee Jumbe kilichokuja kujulikana kama, ‘’The Partner-ship: Tanganyika-Zanzibar Union 30 Turbulent Years.’’ alitualika nyumbani kwake Zanzibar Migombani na tulisafiri meli moja. Siku ile alituingiza katika ‘’Study Room,’’ yake na akatuonyesha ‘’desk,’’ alipoikuta, ‘’The Long Letter,’’ikimsubiri, imerejeshwa kama ilivyoibiwa ofsini kwake Ikulu Zanzibar. Kwangu mimi binafsi ilikuwa furaha ya pekee. Nakumbuka wakati tumekaa tunajiuliza ni nani aliyeirudisha, ‘’The Long Letter,’’ nyumbani kwa Mzee Jumbe na asionekane na mtu. Hakika kilikuwa kitendawili. Mzee Jumbe alikuwa mtu wa kupenda kuandalia chakula kama nilivyosema hapo awali. Wakati sote tumeinamisha vichwa tunamsikiliza jinsi alivyoiona, ‘’The Long Letter, ghafla wakaingia watu wa ‘’catering,’’ na mavazi yao meupe wamebeba sahani za vyakula wanatuandalia. Ilikuwa kiasi cha saa kumi na moja jioni.

Kile ambacho Aboud Jumbe hakupewa nafasi kukisema Dodoma Allah akamuwezesha kukisema miaka kumi baadae kupitia kitabu chake, ‘’The Partner-ship: Tanganyika-Zanzibar Union 30 Turbulent Years.’’ Mzee Jumbe alikuwa mtu wa vichekesho sana. Tulikuwa tunachagua picha za kitabu sasa tukawa tunaangalia picha moja Karume na Nyerere wamepanda gari la wazi. Mmoja wetu akamuuliza Mzee Jumbe, ‘’Hii picha tuweke, ‘’caption gani?’’ Mzee Jumbe mara moja hapo kwa hapo akajibu, ‘’Karume being taken for a ride by Nyerere.’’ Sote tuliangua kicheko.

Nadhani hapa tulipofika panatosha. Huwezi mtu ukammaliza Mzee Jumbe. Nina mengi ningeweza kueleza kuhusu Aboud Jumbe na juhudi zake za kuwasaidia Waislam khasa wa Bara. Mzee Jumbe alikuwa karibu sana na viongozi wa Waislam Bara na alijitahidi sana kuwasaidia kwa hali na mali akifanya mambo yake kimya kimya. Darul Iman walipofanyiwa hujuma wasijenge shule ya ufundi Kibaha. Darul Iman walifunga virago na fedha zile wakataka kuzipeleka Somalia. Mzee Jumbe hakukubali aliwaambia kuwa ikiwa watafanya hivyo watakuwa wamewadhulumu Waislam wa Tanzania kwani hizo fedha zmetolewa kwao. Mzee Jumbe akawaambia kuwa Tanzania ni nchi mbili, ikiwa bara Waislam wanazuiliwa kujengewa hiyo shule hizo fedha zipelekwe Zanzibar na yeye atahakikisha kuwa ardhi inapatikana na shule inajengwa. Mzee Jumbe alipotuambia kuwa kanifanikiwa kuzirejesha fedha za Darul Iman na shule itajengwa Zanzibar, tulimshauri kuwa itakuwa bora badala ya shule kijengwe Chuo Kikuu. Hivi ndivyo ilivyokuja kujengwa Zanzibar University, Tunguu.

Allah tunakuomba umsamehe dhambi zake mzee wetu huyu na umweke mahali pema peponi.
**********************************


Rais Aboud Jumbe: Ilikuwaje chama kikampindua?


WAKATI alipokubali kuunganisha chama chake cha Afro-Shirazi (ASP) na chama cha Tanganyika African Union, Oktoba 1976, Rais wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, hakujua kwamba kwa kufanya hivyo, alikuwa anajitia kitanzi cha kupoteza urais wa Zanzibar miaka minane baadaye.

Tangu mwanzo, chale zilimcheza Jumbe, pale Mwalimu Julius Nyerere, Septemba 5, 1975, alipopendekeza kwenye kikao cha pamoja cha Halmashauri Kuu [NEC] za TANU na ASP, kwamba vyama hivyo viungane. Lakini Jumbe, kwa kusita, na kwa hofu na shaka iliyofichika, alitaka chama chake kipewe muda zaidi kuweza kufikiria pendekezo hilo.

Hatimaye, makubaliano ya Oktoba 1976 yalizaa chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977. Ni CCM kilichompiga buti Jumbe, Januari 1984, kwa tuhuma za kuthubutu kuhoji muundo wa Muungano, akapoteza nafasi zote za uongozi – urais wa Zanzibar, umakamu mwenyekiti wa CCM Taifa, na umakamu wa rais wa Muungano. Ilikuwaje?

Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi aliongoza Zanzibar kuanzia Aprili 1972 baada ya kifo kwa kupigwa risasi cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume. Alirithi nafasi hiyo kwa msaada mkubwa wa Mwalimu Nyerere dhidi ya matakwa ya baadhi ya Wazanzibari ambao walitaka mtu mwenye kuenzi na kuendeleza fikra na utawala wa kibabe wa Karume, arithi nafasi hiyo. Walimtaka Kanali Seif Bakari.

Mwalimu hakukubaliana na maoni ya Wazanzibari ya kumteua Kanali Seif Bakari, mwanajeshi, kuwa Rais wa Serikali ya awamu ya pili, Zanzibar. Alijenga hoja kwamba, kwa kuwa Karume aliuawa na mwanajeshi, Luteni Hamud Hamud, kumteua mwanajeshi mwingine (Bakari) kuwa Rais, kungeleta picha na hisia kwamba, kuuawa kwa Karume yalikuwa ni mapinduzi ya kijeshi.

Nyerere akampendekeza aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (mambo ya Muungano), Aboud Jumbe, kuchukua nafasi hiyo. Hoja yake ikapita.

Jumbe na Nyerere walifanana kwa mengi: wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu Makerere; kisha wote wakawa waalimu. Jumbe alilegeza mengi yenye ukakasi yaliyokithiri wakati wa utawala wa Karume. Hata ile misuguano iliyotia fora kabla ya hapo, kati ya Karume na Nyerere juu ya Muungano na kutishia kuvunjika kwa Serikali ya Muungano, ilitoweka.

Hatimaye Jumbe alianza kukubalika Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, Mwalimu Nyerere. Mara nyingi alialikwa Bara na baadaye akapaona kama nyumbani kwake.

Lakini kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Nyerere, ndivyo alivyozidi kujitenga na siasa pamoja na mambo mengi ya Visiwani. Hatimaye alipaona Dar es Salaam kuwa kwake zaidi kuliko Zanzibar. Aliweza kuruka kwa ndege kwenda Zanzibar mchana kwa ziara fupi, na kurejea Dar jioni.

Kutokuwepo kwake Zanzibar kwa muda mrefu kulizua pengo na ombwe la kiuongozi kwa kuwa hakuna miongoni mwa wasaidizi wake aliyethubutu kumfuata Dar Es Salaam kwa mashauriano. Kwa sababu hii kila kitu kilisubiri arudi Zanzibar kwa “ziara” fupi, hata kama ni idhini ya kukata mti.

Nyerere alifurahishwa na utendaji wa Jumbe na kuingiwa hamu ya kutaka Muungano zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuviunganisha TANU na ASP, kama tulivyoona mwanzo.

Ili kumfurahisha Mwalimu Nyerere juu ya Muungano, mara nyingi hotuba zake zilianza hivi: “Tunataka umoja; ni kwa njia hii pekee kwamba tunaweza kubadili mambo mengi, ili kwamba palipo na kukata tamaa pawe na matumaini, penye chuki pawe na upendo na amani……”.

Muungano ulivyozidi kuimarika, ulifika wakati Jumbe akajiona kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais Nyerere, na hivyo kujimwaga zaidi roho na mwili kwa mambo ya Muungano, badala ya kushughulikia utawala wa Visiwani. Ni matarajio hayo ya kurithi nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, yaliyomfanya akubali kirahisi kuungana kwa ASP na TANU. Ingekuwa enzi za Karume, na kwa jinsi tofauti kati yake na Nyerere zilivyokuwa dhahiri na kubwa, huenda TANU na ASP visingeungana.

Kuanzia Februari 1972 hadi Aprili 1983, Chama kipya – CCM kilifurahia ndoa mpya kwa utulivu; lakini pale Nyerere alipopendekeza marekebisho zaidi ya “kuimarisha Muungano”, mlipuko mpya wa malalamiko ulitokea Zanzibar, moja ya hayo ni hofu ya nchi hiyo kumezwa na “Tanganyika”.

Hofu ya Wazanzibari iliongezeka pale Watanzania Bara walivyozidi kupendekeza kuwa na Serikali moja ya Muungano, badala ya muundo wa Serikali mbili ndani ya Muungano. Hofu hizi za Wazanzibari zilianza kumweka pabaya Jumbe juu ya uswahiba wake na Nyerere; alianza kuitwa “msaliti” wa Wazanzibari na Zanzibar, naye akaanza kugeuka nyuma, lakini kwa kukanganyikiwa; alikuwa njia panda.

Ili kurejesha imani ya Wazanzibari kwake, lakini kwa chukizo kwa Nyerere, Jumbe aliomba mawazo ya kiserikali kutoka kwa makatibu wakuu wote wa wizara na watendaji wakuu wengine wa Serikali ya Zanzibar.

Wote walikataa muundo wa Muungano wenye Serikali moja, wakapendekeza kuwe na Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano tu. Lakini kubwa lililomchanganya akili Jumbe lilikuwa njiani, likimnyemelea.

Mwaka 1983, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Muungano, Edward Moringe Sokoine, aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Sokoine alikuwa kiongozi makini, shupavu, mnyoofu na mwenye mvuto mkubwa kwa watu. Na katika kipindi kifupi tu, alijidhihirisha kuwa “chaguo la watu” na mrithi halali wa Nyerere ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo. Akawa anaonyesha upendeleo dhahiri kwa Sokoine. Kuna sababu nyingi kwa hilo; lakini itoshe kutaja tatu tu kati ya hizo.

Moja ni kwamba, Nyerere alianza kumwona Jumbe kama kiongozi mpweke, asiyeungwa mkono na watu wa chini (umma) Visiwani. Alimwona pia kama dikteta mkimya, asiyeweza kushauriwa akashaurika na watu wa chini yake.

Nyerere aligundua pia kile pekee kilichomsukuma “ang’are” kwake na kwa Wabara: kiu ya kurithi nafasi ya Rais baada ya Nyerere.

Baya zaidi lililomuudhi Mwalimu ni kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Jumbe alizuru nchi nzima akitoa mihadhara kwenye misikiti hata Serikali ikalazimika kutoa waraka mkali wa Rais (presidential circular), kuwakumbusha viongozi wa kitaifa kutojitambulisha na mambo ya kidini. Hata hivyo, Jumbe alipuuza waraka huo, akaendelea kivyake.

Habari zikamfikia Jumbe juu ya kuanza kupoteza upendeleo wa Nyerere na kuchuja; zikauma, zikamvunja moyo; uhasama kati ya Jumbe na Nyerere ukazuka. Katika hali hiyo Muungano ukaanza kutikiswa.

Hatua ya kwanza iliyoanza kutikisa Muungano ilikuwa ni kumrejesha Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva; badala yake akamteua raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy na kumpa uraia.

Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto. Wengi watakumbuka matangazo ya redio ya mafichoni, maarufu kama “Kiroboto tapes”, ya kudai Wazanzibari warejeshewe visiwa vyao, yalivyopamba moto hadi ilipogunduliwa msituni na wanajeshi kutoka Bara na kuzimwa.

Kwa kupitia Jaji Bashir Swanzy, iliandaliwa hati ya mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kazi yake pekee, kwa mujibu wa ibara ya 126 ya Katiba ya Muungano ya 1977, “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar”.

Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Jumbe katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere. Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa waliofanikisha kazi hiyo ni pamoja na wakubwa wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakati ule wakiwa SMZ.

Haraka haraka na hima, kikaitishwa kikao cha NEC ya CCM mjini Dodoma, Januari 1984 na Jumbe akawekwa kiti moto kwa dhambi ya kujaribu kutua mahali malaika wanapopaogopa kutua, kwa maana ya kuhoji Muungano; kisha ikatangazwa “kuchafuka kwa hali ya siasa Zanzibar”.

Bila kumeza maneno, Jumbe alikiri kuandaa hati hiyo kama moja ya haki zake za kikatiba.

Mbali na hati ya mashitaka, Jumbe aliandaa pia barua ndefu kumkumbusha Nyerere jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyokuwa zikikiukwa. Alihoji pamoja na mambo mengine, mantiki ya kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM na mamlaka chama hicho kiliyojipa, ya kutunga Katiba ya kudumu ya 1977.

Kwa msaada wa Mwanasheria Mkuu Swanzy, Jumbe alifanya rejea Sheria ya kuahirisha na kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, Namba 18 ya 1965, Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965, na ubatili wa Katiba ya kudumu ya 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa.

Kwa kuwa barua hiyo ndefu ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, alimtaka Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa Kiswahili iweze kujadiliwa na Baraza la Mapinduzi.

Kama ilivyotokea kwa hati ya mashitaka, barua hiyo nayo ilitoweka mezani kwa Jumbe katika mazingira ya kutatanisha na kumfikia Nyerere. Kwa kuwa alikuwa hajaitia sahihi ilibidi kikao cha NEC kimtake Jumbe aseme kama hayo ndiyo yalikuwa mawazo yake; naye kwa mara nyingine, na bila ya kutafuna maneno, alikiri, na hivyo mvua ya mawe ikazidi kumnyea.

Awali, Januari 12, 1984, Jumbe alihutubia wananchi kwenye kilele cha sherehe za Mapinduzi, siku chache tu kabla ya kuitwa Dodoma. Katika hotuba hiyo, hakuficha kukerwa kwa Serikali yake namna Muungano ulivyotekelezwa kinyume na matakwa asilia. Aliwataka wananchi wawe wavumilivu na wenye subira wakati tatizo hili likiendelea kushughulikiwa.

Bila kumeza maneno, na Mwalimu Nyerere akisikia; Jumbe alisema, kama pasingepatikana mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya jambo hilo, angelipeleka kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba kupata ufumbuzi kwa yote haya.

Katika kikao cha NEC cha Dodoma, Jumbe alielezewa kama “kiongozi dhaifu na msaliti wa Muungano”. Alipinduliwa sawia na kupoteza nafasi zote, kisha akasindikizwa nyumbani kwake na kuwekwa chini ya ulinzi wakati harakati za kusafisha hewa ya kisiasa zikiendelea.

Tetemeko likawakumba wasaidizi wake wakuu, wakiwamo Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji, Waziri wa Nchi, Aboud Talib, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Wolfango Dourado wakati Swanzy alirejeshwa kwao Ghana.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Muungano na Mjumbe wa NEC, Kanali Seif Bakari, alipigana kiume kikaoni kujaribu kumwokoa Jumbe, lakini aliishia kuwekwa chini ya ulinzi wa nyumba yake na hatimaye kizuizini Tanzania Bara.

Nafasi ya Jumbe ilichukuliwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi, na Seif Sharrif Hamad akaukwaa Uwaziri Kiongozi.

Je, hayo yalikuwa Mapinduzi dhidi ya Jumbe, kutekwa nyara au zilikuwa hatua za kinidhamu za chama?.

Jumbe alikuwa Rais wa “nchi” ya Zanzibar kwa mujibu na kwa misingi ya Katiba ya Zanzibar ya 1979. Na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano [Articles of Union] wa 1964, ambao ndio unaosimamia na kutawala Katiba zote mbili – Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar, suala la Vyama vya Siasa halikuwa, halijawa na halipashwi kuwa jambo la Muungano.

Kwa mantiki hii, kitendo cha chama cha siasa kumwondoa madarakani Rais wa “nchi” yenye Katiba yake, yenye Serikali yake na Bunge lisilotawaliwa na Katiba ya Muungano, ni dhahiri kilikuwa kimevuka mipaka ya uwezo wake. Kwa sababu hii, hayo yalikuwa Mapinduzi ya kutumia nguvu ya kisiasa).

Baada ya kazi ya kumpindua Jumbe kukamilika, na ili kuhakikisha “vituko” vya kuhoji Muungano vimedhibitiwa Visiwani, suala la Usalama wa Taifa, ambalo kabla ya hapo halikuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni Ulinzi tu), liliingizwa kwenye Muungano kusomeka “Ulinzi na Usalama”.

Kitendo cha Mwalimu Nyerere cha kusimamia na kufanikisha mapinduzi dhidi ya Jumbe kupitia NEC ya CCM, chama pekee kilichoshika hatamu za uongozi wa nchi; na kitendo cha kutiwa kizuizini kwa Kanali Seif Bakari, si tu kilichochea chuki miongoni mwa Wazanzibari kwa Muungano, bali pia kilizua mgawanyiko wa makundi mawili miongoni mwa viongozi waandamizi Visiwani na hatimaye kuenea Bara.

Kundi moja ambalo halikufurahishwa na kupinduliwa kwa Jumbe na ambalo lilitaka kudumisha mapinduzi na fikra za Karume lilijiita “Wakombozi” (Liberators), na la pili lililotaka mabadiliko haraka na Zanzibar mpya, lilijiita “Wanamstari wa mbele” (Frontliners). Makundi haya yalipogongana, moto uliwaka kwa kishindo cha radi.

Kundi la “Wakombozi”, huku limesheheni chuki na hasira ya kulipa kisasi kwa Nyerere, lilisubiri nafasi na wakati mwafaka kwa tukio zito kutokea ili limpe kibano na kumdhalilisha, yeye na Muungano kwa ujumla. Jambo zito hilo lilikuwa nini? Je, kundi hilo liliweza kutekeleza azima yake?.

Rais Aboud Jumbe: Ilikuwaje chama kikampindua? II


KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona namna Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichoshika hatamu zote za uongozi wa nchi wakati huo, kilivyoweza kumpindua Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi, Januari 1984; na jinsi hatua hiyo ilivyozua makundi mawili yenye uhasama visiwani.

Makundi hayo yalikuwa ni kundi la “Wanamstari wa mbele” (Frontliners), lililofurahishwa na mapinduzi hayo na lililotaka kuona Zanzibar mpya. Kundi la pili, lililoitwa “Wakombozi” (Liberators), lilichukizwa na mapinduzi hayo na kujenga chuki na uhasama mkubwa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesimamia na kufanikisha mapinduzi hayo; na likaapa kumpa ‘kibano’ na kumdhalilisha nafasi ikitokea. Je, nafasi hiyo ilitokea? Endelea na sehemu hii ya pili na ya mwisho kupata jibu.

Wakati akijiandaa kung’atuka urais, Mwalimu Nyerere aliwauma sikio marafiki na wasiri wake wa karibu kwamba, safari hii (mwaka 1985) angependelea Rais wa Muungano atoke visiwani. Hata hivyo, chini ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union), Sheria ya Muungano ya 1964 na Katiba ya Muungano, utaratibu huo haukuwepo wala kutambulika. Kwa hiyo, hayo yalikuwa mawazo ya Mwalimu Nyerere pekee na kutumia ushawishi ili wengine nao wakubaliane naye.

Ilivyotokea ni kwamba, CCM kilipeleka Kamati Kuu, majina matatu tu ya wagombea. Hao walikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti CCM taifa wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, Rashid Mfaume Kawawa, na aliyekuwa Waziri Mkuu, Dk. Salim Ahmed Salim. Kati ya hao watatu, ni Rashid Kawawa pekee ambaye hakuwa Mzanzibari.

Mwinyi, licha ya kuzaliwa Kisarawe, mkoani Pwani -Tanzania Bara na kukulia Zanzibar alikuwa Mzanzibari kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Mzanzibari ni Mtanzania yeyote aliyeishi kwa miaka sita mfululizo visiwani. Lakini si Mzanzibari aliyeishi Tanzania Bara kwa kipindi hicho kuweza kuitwa Mtanzania Bara; yeye huyo, anabakia “Mzanzibari” tu.

Ili kumpata mrithi wake kati ya hao watatu, Mwalimu Nyerere alianzisha mchezo wa karata za kisiasa kwa “kuwashika” wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM. Kwa bahati mbaya sana, vyombo hivi – CC na NEC, vilisheheni makundi yenye uhasama, yaani kundi la “Wanamstari wa mbele” na kundi la “Wakombozi”; kila kundi likiwania kumwangamiza mwenzake. Miongoni mwa kundi la “Wanamstari wa mbele” walikuwemo ni Dk. Salim Ahmed Salim, Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF sasa), Hamad Rashid Mohamed (Mbunge wa Wawi-CUF) na Khatib Hassan.

Wengine walikuwa ni Kanali Adam Mwakanyuki, Isaac Sepetu, Shabaani Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu.

Kundi la wakombozi, ambalo lilijiona kama warithi halali wa sera za Karume na ASP, lilikuwa na Brigedia Abdullah Said Natepe (kiongozi wao), Ali Mzee, Hassan Nassoro Moyo, Muhamed Seif Khatib na Salmin Amour.

Walikuwamo pia maofisa wastaafu wa jeshi na wa Idara ya Usalama wa Taifa kama Brigedia Ramadhan Haji ambaye pia alikuwa Waziri Kiongozi wakati wa Jumbe; Mkuu wa Jeshi la Zanzibar mstaafu, Brigedia Jenerali Khamis Hemed na wengineo.

Tangu mwanzo, “Wakombozi” hawakumtaka Dk. Salim. Itakumbukwa, kwa mfano, mwaka 1982, pale Dk. Salim alipoteuliwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano, Natepe (wakati huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Muungano, mwenye dhamana ya Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (aliyekuwa na wadhifa kama huo kwa Serikali ya Zanzibar), walikwenda kwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, kumwambia kwamba, walikuwa na mamlaka kutoka kwa Rais Jumbe na Seif Bakari, kuwataka Sokoine na Mwalimu, wafute uteuzi wa Salim.

Walitoa sababu kuu mbili: moja ni kwamba, kulikuwa na makubaliano ya siri ya kudumu tangu utawala wa Karume, kwamba wanachama wote wa vyama vya siasa vya zamani mbali na ASP, wasishike nyadhifa zozote za uongozi wa kichama na kiserikali visiwani na kwenye Muungano, bali watumike kwa kazi za kitaaluma tu. Salim alikuwa mmoja wa viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha “Umma Party”, kilichosimamia kishujaa Mapinduzi ya Januari 12, 1964, kwa kushirikiana na vijana wenye siasa za mrengo wa Kikomunisti ndani ya ASP, akiwamo Kassim Hanga na wengine.

Kwa mantiki hiyo, walengwa wa makubaliano hayo ya siri walikuwa Wazanzibari wote, ndugu na koo zao, waliowahi kuwa wanachama wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Babu.

Uhasama huu wa kihistoria umedumu kwa zaidi ya nusu karne mpaka hivi karibuni, ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani. Baadaye katika uhasama huo, nafasi ya ASP ilichukuliwa na CCM Zanzibar; na ile ya ZNP/ZPPP/UP ilichukuliwa na CUF Zanzibar. Ni kwa sababu hii, kulikuwa na msuguano mkali wa CCM na CUF Zanzibar, na si hivyo kwa vyama hivyo Tanzania Bara.

Pili, walidai kuwa, Wazanzibari wanapoona mtu suriama wa Kiarabu na Kiafrika kama Salim akishika nafasi za madaraka, inawakumbusha chuki kubwa ya utawala wa Sultani aliyepinduliwa.

Lakini pamoja na uongo huo wa kizandiki, “Wakombozi” hao walisahau kwamba, kufuatia Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Karume alimteua Salim Ahmed Salim, Balozi wa Zanzibar nchini Misri.

Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakuvumilia mizaha, majungu na uzandiki, aliwafukuzia mbali wazushi hao, na nyota ya Salim ikazidi kung’ara kiasi kwamba, Sokoine alipofariki Salim alirithi nafasi yake.

Wakombozi hawakukubali kushindwa; walibadili staili kwa kuanzisha kampeni Tanzania Bara dhidi ya Salim, safari hii kwa kudai kwamba alikuwa hakubaliki visiwani, na pia kwamba kama angepewa madaraka, angeshirikiana na nchi za Kiarabu kurejesha ubepari nchini.

Hapo tena, hawakujua kuwa nchi yetu ilikuwa mbioni kupata Ubalozi wa Saudi Arabia nchini, na pia ilitarajia kufungua Ofisi za Ubalozi kwenye nchi nyingi za Kiarabu.

Kisha wakaja na tuhuma nzito zaidi, kwamba Salim alihusika na kifo cha Karume mwaka 1972, wakati huo akiwa Balozi nchi za nje. Karume aliuawa kwa kupigwa risasi, Aprili 7, 1972 na mwanajeshi, Luteni Hamud, kulipa kisasi kwa uhasama wa kisiasa.

Nassoro Hassan Moyo, ndiye alikuwa kiunganishi kikubwa kwa kundi la visiwani na kundi la Tanzania bara katika kuhakikisha kwamba jina la Salim halipiti; akisaidiana na Ramadhan Haji, Ali Mzee na Aboud Talib, wote wa Visiwani.

Kiunganishi mkubwa kwa Bara kwenye CC na NEC katika kampeni hizo, alikuwa Waziri wa Mali asili na Utalii, Paul Bomani.

Ali Hassan Mwinyi alionwa na “Wanamstari wa mbele” siku ya uteuzi, wakiamini kwamba walikuwa wamemshawishi kikamilifu na vya kutosha kuweza kukubali kutogombea. Hata hivyo, mambo hayakuwa hivyo Agosti 12, 1985, pale CC ilipoketi kupendekeza jina la mgombea, wakati ahadi ya Mwinyi ya kujitoa ilipoota mbawa.

Mwalimu Nyerere alielewa fika jinsi mchezo huo mchafu wa kupakana matope na kubomoana, ulivyokuwa ukichezwa. Licha ya kumpendelea Salim, lakini hakutaka kuonyesha, wala kuegemea upande wowote.

Rashid Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijiengua; wakabakia Mwinyi na Salim, kisha wakaombwa watoke nje ya chumba, ili wajadiliwe.

Kilichotawala mjadala pekee ni sifa za Mwinyi, kiasi kwamba Salim hakujadiliwa. Wakombozi walitumia vyema muda huu, huku Moyo na Natepe wakitawala mazungumzo.

Mjumbe mwingine wa CC wa Kambi ya Bomani aliyezungumza kwa kirefu, alikuwa Mama Getrude Mongela. Hoja yao ilikuwa kwamba, kumruka Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Makamu wa chama tawala na kumteua Salim, kungetafsiriwa vibaya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kwamba, Watanzania hawakuwa na mipango thabiti ya kuandaa watawala na kurithishana madaraka. Isitoshe, Mwinyi angejiona vibaya kwa kurukwa. Kwa njia hii, Mwinyi akaibuka mshindi kama pendekezo la CC kwenda NEC kwa uteuzi wa mwisho.

Mwinyi angeweza kujitoa kutekeleza ahadi yake kwa Nyerere na kwa kambi ya Wanamstari wa mbele, lakini hakufanya hivyo, badala yake alisema: “Kama haya (uteuzi) ni mapenzi ya wananchi, nakubali”. Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao, hakupinga, pengine kwa kutarajia kwamba NEC ingemwinua Salim.

Kambi ya Wakombozi ilitamba kwa kulamba dume kwa mara nyingine kwenye kikao hicho, ilipofika uteuzi wa mgombea kiti cha Rais wa Zanzibar, baada ya kupendekeza kwa sauti moja, jina la Idrisa Abdul Wakil, ambapo Wanamstari wa mbele walimpendekeza Seif Sharrif Hamad.

Mapendekezo ya CC yaliwasilishwa NEC Agosti 15, 1985 kwa uteuzi wa mwisho. Kwenye kikao hicho, kambi ya “Wanamstari wa mbele” ilipata mtetezi kwa jina la Mzee Thabit Kombo, swahiba mkubwa wa Nyerere; aliyewasilisha hoja kwamba, kumtoa Mwinyi Zanzibar ili awe Rais wa Muungano, kungevuruga hali ya amani na utulivu aliyosaidia kujenga na kusimika katika uongozi wake wa miezi 18 tu Visiwani.

Kauli ya Kombo ilimezwa kwa sauti za kupinga za wajumbe wa NEC kutoka Bara, kuonyesha kwamba Bomani na Mongela walikuwa wamefanya kampeni yao vyema. Nyerere akaahirisha kikao kwa muda, akawaita pembeni wasiri wake wachache, wakiwamo Mwinyi, Kawawa na Kombo; wote hao, wakateta jambo.

Kikao kiliporejea, Kombo alikuwa amegeuka, alimuunga mkono Mwinyi; na kwa mara ya kwanza alimuunga mkono Wakil, kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar. Kura zilipopigwa, ni kura 14 tu kati ya 1,746 zilizomkataa Mwinyi.

Kwa upande wa Zanzibar, ambapo ni wale wajumbe 163 tu wa NEC kutoka Zanzibar waliokuwa na haki ya kupiga kura kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, Wakil alipata ushindi mdogo wa kura 85 dhidi ya 75 za Seif Sharrif Hamad.

Ushindi huo kwa nafasi zote mbili uliwapagawisha kambi ya wakombozi, wakaonekana kuchezesha maungo yao dhahiri hadharani, huku Getrude Mongela akipiga mbiu kwamba ni wao, waliopendekeza jina la Mwinyi na la Wakil, kwenye CC; na kupigana kufa na kupona kwenye NEC kuokoa jahazi.

Kwa kambi ya “Wakombozi” kutoka Bara, ushindi wa Mwinyi uliwafanya wapumue kwa matarajio, kwamba angalau sasa nchi ingetawaliwa na mtu (Mwinyi) asiye na makuu, asiye na msimamo, msikivu lakini rahisi kuyumbishwa; kuliko kama angetawala Salim, kiongozi mwenye kujiamini, mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kujenga hoja, mchangamfu lakini mwenye tahadhari daima.

Shamra shamra za “ushindi” wa “Wakombozi” zilivyozidi kuwa adha kubwa hata wakati wa Kampeni za Urais Zanzibar, ilibidi Nyerere, Mwinyi na Kawawa wavae njuga kuzikabili, ili kufuta dhana kwamba “Wakil amepona kutoswa” kwa nguvu na Wakombozi na kuanza kuwasafisha Wanamstari wa mbele ili wasidhalilishwe bila sababu za msingi. Mwalimu, huku akimlenga Natepe na kundi lake alisema:

“Nataka mjue kwamba, nawaelewa vyema vijana (Wanamstari wa mbele) hawa. Ni vijana wakweli makini na si wasaliti. Sitavumilia kuona wakichukuliwa kuwa maadui (wa Zanzibar na Wazanzibari). Na hilo ndilo agizo langu”.

Katika uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 1985, mgombea pekee, Abdul Wakil Nombe, alipata ushindi duni wa asilimia 58.6 tu, ambapo kwa Pemba pekee, alipata chini ya asilimia 25.

Pamoja na kinyang’anyiro cha madaraka miongoni mwa Wana-CCM Zanzibar kufikia kikomo, bado mpasuko kwa njia ya vikundi hivyo vyenye uhasama uliendelea chini kwa chini. Na kwa sababu CCM kilikuwa Chama cha kitaifa, migongano yote ya Zanzibar ililetwa kwenye NEC Tanzania Bara (Dodoma) kwa usuluhishi na uamuzi.

Hata hivyo, hali ilipoendelea hivyo, miaka miwili baadaye, yaliandaliwa mashitaka toka CCM Zanzibar, dhidi ya “Wanamstari wa mbele” saba, maarufu kama “the magnificent seven”, kisha NEC ikakaa Kizota, Dodoma na kuwafukuza uanachama Seif Sharrif Hamad, Shabaan Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na Ali Salim.

Kundi hili la waliofukuzwa, lilijikusanya na kuanzisha Chama cha upinzani kwa siri, kwa jina la “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru” (KAMAHURU) ambacho, miaka minne baadaye juu yake, pamoja na vyama vingine, palimea na kukua Chama cha Wananchi – CUF, chenye nguvu kubwa karibu sawa na CCM Visiwani.

Leo, CUF Zanzibar na CCM Zanzibar vimefunga ndoa kuwa mwili mmoja chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Je, ndoa hiyo itaweza kuondoa au kufuta kabisa minyukano ya chini kwa chini miongoni mwa “Wakombozi” na “Wanamstari wa mbele” ndani ya Serikali hiyo?. Muda, kama ilivyo ada, ni shahidi wetu mzuri.
**********************************

Kupaa na kutunguliwa kwa Aboud Jumbe Mwinyi

Nasaha za Mihangwa

Joseph Mihangwa
Toleo la 292&293
1&8 May 2013
Gazeti: Raia Mwema.

MIAKA 29 iliyopita, Januari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua (ilimpindua?) nafasi zote za uongozi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaj Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutenda ‘dhambi kuu’ ya kuhoji muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Nyadhifa alizovuliwa kiongozi huyo na kubakia kuwa raia wa kawaida na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake kwa kipindi kadhaa, ni pamoja na urais wa Zanzibar, uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umakamu wa Rais wa Tanzania na umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Mkutano huo ulitawaliwa na kampeni chafu dhidi ya Jumbe, huku kambi mbili za Zanzibar zikiumana, kwa kambi moja kuunda tuhuma dhidi yake na nyingine kujibu mapigo, na hivyo kuchonga ufa na uhasama mkubwa miongoni mwa viongozi wa Zanzibar kati ya kambi mbili hizo kinzani; kambi iliyojiita ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoundwa na waliojiona kama watetezi halisi wa Mapinduzi ya 1964 na ile ya kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Front liners), iliyotaka mabadiliko ya sera visiwani.

Katika msuguano huo, Kamati ya Wakombozi ilishindwa na Rais Jumbe akatunguliwa kwa mzinga mzito, akaisha. Jumbe alikuwa mrithi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa, Aprili 7, 1972. Kabla ya hapo, Jumbe alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia mambo ya Muungano.

Kuuawa kwa Karume kulifikisha tamati ya utawala wa awamu ya kwanza kufuatia Mapinduzi ya 1964, utawala uliotawaliwa na vitisho, hofu, umwagaji damu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya yeyote aliyetoa sauti kuhoji utawala huo, na au kwa aliyedhaniwa tu kuwa mpinzani wa Mapinduzi.

Uporaji huo wa demokrasia, ulitekelezwa na utawala wa Karume kupitia genge katili lilojulikana kwa jina la ‘The Gang of Fourteen (Genge la Watu 14), likiongozwa na Kanali Seif Bakari. Kugongewa mlango tu usiku na genge hilo enzi hizo, kulitosha mtu kupatwa hofu kabla ya kuhojiwa.
Genge hili na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, walitaka kuendelezwa kwa sera za Karume, na mtu pekee waliyeona angeweza kufanikisha hilo kama mrithi halali wa Karume, ni huyo Kanali Seif Bakari.

Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliposikia hilo, akaona giza mbele. “Sera za Karume tena? Ukatili na mauaji ya kutisha kwa watu wasio na hatia? Hapana!” alisikika Mwalimu aking’aka mbele ya watu wake wa karibu, na kuamua kutokubaliana na pendekezo la Wazanzibari lililomtaka Kanali Bakari kumrithi Karume. Akajenga hoja nzito kupangua kisayansi hoja hiyo kwa kuhusisha na tukio la kuuawa kwa Karume!

Jaribio la mapinduzi lililoshindwa liliandaliwa na wanasiasa makini wa Kizanzibari kwa kuhusisha baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Zanzibar, ambalo hadi akiuawa, Karume alikuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wake; kwa kushirikisha pia wanajeshi kadhaa wa Kizanzibari waliokuwa kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kwa upande wa Bara.

Muuaji wa Karume, Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, alikuwa wa Jeshi la Zanzibar. Alichukua hatua hiyo yeye mwenyewe baada ya kuhisi kwamba mpango wa mapinduzi umegunduliwa siku hiyo, na kwamba yeye na wenzake walikuwa wanatafutwa; na kwa sababu kikosi cha pili cha mapinduzi kutoka Dar es Salaam kilishindwa kufika Zanzibar muda uliopangwa, baada ya kuonywa kikiwa baharini juu ya kugunduliwa kwa mpango huo na kurejea hima Dar es Salaam. 

Luteni Hamoud aliona kwa mikasa hiyo miwili, kwa vyovyote vile, angekamatwa na kuuawa kikatili. Akaamua na lolote liwe, na bila kupoteza muda akaamua kutekeleza mauaji hayo yeye mwenyewe na wenzake wengine watatu tu.

Imeelezwa kwamba ushiriki wa Luteni Hamoud katika jaribio hilo, mbali na kubeba hisia (sentiments) za kisiasa, pia alidhamiria siku nyingi tangu nyuma, kulipiza kisasi kwa Karume kwa kifo cha baba yake, Mzee Mohammed Hamoud, aliyeuawa kikatili na kiongozi huyo akiwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.

Mwalimu Nyerere hakutaka mauaji ya Rais Karume yatafsiriwe au yahusishwe na jaribio la mapinduzi, bali alitaka yatafsiriwe kama mauaji ya kisiasa tu. Akasema, hatua yoyote ya kumteua Kanali Seif Bakari ambaye ni mwanajeshi, kuchukua nafasi ya Karume aliyeuawa na mwanajeshi pia, kungetafsiriwa kama Mapinduzi ya Kijeshi. Hapo, Wazanzibari wakanywea, wakatazamana kwa ishara bila kupata jibu kwa hoja ya Mwalimu Nyerere. Hawakuwa na namna isipokuwa kufuta pendekezo la uteuzi wa Kanali Seif Bakari kumrithi Karume.

Ndipo ikawadia zamu ya Mwalimu Nyerere kushawishi na kushauri nani ateuliwe. Akasema, pamoja na kuuawa kwa Karume, ambaye alikuwa mwasisi mwenza wa Muungano wa Tanzania, Muungano huo lazima uendelezwe bila kuyumba; na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, alikuwa ni Aboud Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu:-

Mosi, ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari. Pili, ni mtu ambaye hakuwa na majungu wala makundi yenye kuhasimiana. Tatu, wadhifa wake wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu, ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu, na uwezo wa kuendeleza na kudumisha Muungano. Hoja ya Mwalimu ikapita; Jumbe akapaa, akawa Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili.

Jumbe na Mwalimu Nyerere walifanana kwa mengi. Wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, na kisha wote wakawa walimu wa sekondari. Kwa uhusiano mzuri huo, Jumbe alianza kulegeza mengi yenye ukakasi visiwani ambayo yasingewezekana enzi za Karume ambaye aligeuka mwiba kwa Mwalimu, akidai mara nyingi wavunje Muungano kwa kuwa uligeuka koti lililowabana Wazanzibari. Chini ya Jumbe, misuguano kati ya Bara na Visiwani ambayo kabla yake ilizua kero za Muungano, ilianza kutoweka.

Jumbe alianza kukubalika haraka kwa wengi Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, naye akaanza kupaona Bara kama nyumbani kwake. Akajenga makazi yake eneo la Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na kurejea tena jioni baada ya kazi. Ufanisi wake wa kuihudumia Zanzibar ulipungua kwa sababu ya kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye Muungano. Na kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Mwalimu, (majukumu ambayo Mwalimu hakuthubutu katu kumpa Karume), ndivyo alivyozidi kujiweka mbali na siasa za Zanzibar na Wazanzibari.

Kwa kutumia hali hiyo ya maridhiano, Mwalimu alizidi kuchanja mbuga kwenda mbele zaidi bila Jumbe kushuku kitu. Katika kikao cha pamoja cha NEC ya TANU cha Bara na NEC ya ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es Salaam, Septemba 5, 1975, Mwalimu Nyerere alipendekeza vyama hivyo viungane ili kuimarisha zaidi Muungano.

Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa ya kuunda Chama kipya ‘Chama cha Mapinduzi’ (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20 nyuma, mwaka 1957.
Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama chao, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno ‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.

Na hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika hatamu zote za uongozi wa nchi na kuweza kumng’oa madarakani Jumbe miaka saba baadaye, mwaka 1984, kama kitanzi alichojitengenezea mwenyewe. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hati (Mkataba) ya Muungano ya Aprili 22, 1964, vyama vya siasa si jambo la Muungano kuweza kusimamia mamlaka za Muungano. Hivyo utaratibu uliotumika kumng’oa Jumbe unahojika kisheria!

Kadri Jumbe alivyozidi kujiona kukubalika kwa Mwalimu Nyerere, ndivyo alivyojiona pia kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais wa Muungano kuliko mtu mwingine yeyote, Bara na Visiwani. Lakini kutokuwepo kwake Zanzibar mara kwa mara kulizua ombwe la uongozi kwa kuwa kila kitu kilimsubiri yeye, hata kama ni idhini ya kukata mti. Na kwa jambo la dharura, Waziri mwenye dhamana ya dharura hiyo ilibidi amfuate Dar es salaam.

Kana kwamba ombwe hilo halikutosha, hofu ilitanda miongoni mwa Wazanzibari pale Mwalimu alipopendekeza mabadiliko zaidi ya Katiba kutaka kuunda Serikali moja badala ya Serikali mbili, wakihofia nchi yao kumezwa na Tanganyika. Hali hii ilimweka pabaya Jumbe Visiwani juu ya uswahiba wake na Nyerere, wakimwita ‘msaliti’ wa Mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari. 

uona hivyo, Jumbe alianza kugeuka nyuma kwa kuchanganyikiwa; akawa njia panda. Wakati hilo halijapoa, jingine kubwa zaidi lilikuwa njiani likija. Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa na mvuto wa watu, shupavu na mwadilifu kiasi kwamba katika kipindi kifupi tu alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi halali wa Mwalimu, ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.

Kwa kuridhika na Sokoine, taratibu Mwalimu alianza kumbeza Jumbe kwa sababu nyingi, lakini itoshe hapa kutaja mbili tu. Kwanza, alimwona kama kiongozi mpweke asiye na sapoti na aliyepoteza mvuto Visiwani, pia kama dikteta mkimya asiyeshaurika na watu wa chini yake.

Pili; Mwalimu aliudhika kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Kwa hili, Jumbe alizuru nchi nzima akitoa hotuba kwenye misikiti, na Serikali ikalazimika kutoa Waraka mkali wa Rais, kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa kitaifa kutojipambanua au kuendekeza mambo ya kidini. Jumbe alipuuza Waraka huo; kwake ndio kukawa kumekucha.

Habari za Mwalimu kupoteza imani na upendeleo kwa Jumbe hatimaye zilimfikia kiongozi huyo, zikamuuma sana na kumvunja moyo. Hapo uhasama ukazuka kati yake na Mwalimu kwa njia ya kukomoana. Kwa hasira na kukata tamaa, Jumbe akaanza maandalizi ya kuumbua Muungano, kwa minyukano na Mwalimu.
Kuanzisha minyukano hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza Jumbe arejeshe imani yake iliyopotea kwa Wazanzibari, kutokana na hatua yake ya kuhamia Mji mwema, Kigamboni na kwa kuwatelekeza Wazanzibari. Baada ya kuridhika kwamba mambo ameyaweka sawa, aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji Wakuu wengine wa Serikali, ni aina gani ya Muungano unaotakiwa.

Wote, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian Lubuva, walikataa muundo wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja uliokuwa umeanza kupigiwa upatu na Mwalimu na baadhi ya wanasiasa. Jumbe na watendaji wake hao ndani ya Serikali ya Zanzibar wakapendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo kumi na moja tu yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.
Mtizamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake kiitwacho ‘The Partnership,’ yaani ‘Ubia kati ya Tanganyika na Zanzibar,’ kilichosambazwa mwaka 1984. Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Muungano, “Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.” (The Partnership, uk. 22).

Vivyo hivyo, anathibitisha kwa kunukuu Ibara ya Sita (a) ya Mkataba, inayotanabahisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano, atasaidiwa na Makamu wawili wa Rais (mmoja kwa ajili ya Tanganyika na mwingine kwa ajili ya Zanzibar), Mawaziri na Maofisa wengine anaoweza kuwateua kutoka Tanganyika na Zanzibar ambapo kufuatia uteuzi huo, utumishi wao utahamishiwa kwenye utumishi wa Serikali ya Muungano.

Anahoji: “Kwa kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, vinatambua uwapo na kubakia kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya Muungano, kwanini Muundo uliokusudiwa usitafsiriwe kuwa Shirikisho? Kama Tanganyika na Zanzibar zinatajwa kuwa nchi ndani ya Muungano, lakini kwa vitendo na hulka kuna nchi ya Zanzibar pekee, Tanganyika ilikwenda wapi?

Hatua iliyofuata na aliyochukua Jumbe, ilikuwa ni kumrejesha kwao Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, akimwelezea kama mtumishi asiyeweza kusimamia maslahi ya Wazanzibari; na badala yake akamteua rafiki yake wa zamani, raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy kuwa Mwanasheria Mkuu.

Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao walikuwa na malalamiko yao.

Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la ‘Kiroboto Tapes,’ hadi ilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara. Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.

Jumbe aandaa mashitaka dhidi ya Muungano
Kwa kumtumia Alhaj Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana aliyemteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kushika nafasi ya Damian Lubuva, na kumpa uraia kwa njia ya usajili, Rais Jumbe aliandaa Hati ya Mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, kazi yake pekee (nanukuu) “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba; iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Katika hili, Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Wolfgang Dourado (sasa marehemu), naye alishirikishwa. Hata hivyo, Hati hiyo ya mashitaka ilipotea mezani kwa Rais Jumbe katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere (Ikulu, Tanzania Bara).

Mbali na Hati ya Mashtaka, Rais Jumbe aliandika pia barua ndefu kwa Mwalimu kubainisha jinsi Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano zilivyoendelea kukiukwa na utawala wa nchi, na kuhoji pia mantiki ya kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM, na mamlaka turufu Chama hicho kiliyojipa kusimamia Muungano, wakati vyama vya siasa si jambo la Muungano.

Kwa msaada pia wa Jaji Swanzy, Rais Jumbe alifanya rejea kwa kuhoji uhalali wa Sheria Namba 18 ya mwaka 1965, iliyoahirisha kwa kusogeza mbele muda wa kuitisha Bunge la Katiba, ubabe wa Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965 na ubatili wa Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977 kwa namna ilivyobuniwa na kutungwa bila kuzingatia matakwa ya Mkataba na Sheria ya Muungano.

Kwa kuwa barua hiyo iliandikwa kwa lugha ya Kiingereza, alimwagiza aliyekuwa Waziri Kiongozi wake, Ramadhan Haji, ahakikishe imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili iweze kujadiliwa kikamilifu kwenye Baraza la Mapinduzi.

Kabla ya hapo, akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1984, Rais Jumbe alionyesha kukerwa na jinsi Muungano ulivyokuwa ukiendeshwa na kuwataka Wazanzibari wavute subira wakati tatizo hilo likishughulikiwa, na kwamba bila ya mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya muundo sahihi wa Muungano, Zanzibar ingekwenda Mahakamani.

Kwa mara nyingine, kama ilivyopotea Hati ya Mashitaka katika mazingira ya kutatanisha, ndivyo pia barua hiyo ndefu ilivyopotea hata kabla Rais Jumbe Mwinyi hajaitia sahihi na kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.

Kwa kuona hatari mbele yake, haraka haraka kikaitishwa kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma kumjadili Rais Jumbe kwa dhambi kuu ya kuthubutu kutua mahali ambapo ‘Malaika’ waliposhindwa kutua.
 
Humo ndani ya kikao, mizinga ikalia. Mizinga ya piga nikupige, huku kambi mbili za Kizanzibari zikiumana kutaka kuangamizana. Kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Frontliners) ilitaka Rais Jumbe atoswe, huku ikimwelezea kama msaliti wa Muungano, kiongozi dhaifu na asiyekubalika Visiwani, mbinafsi na mwenye makundi.

Kambi ya pili, ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliona Rais Jumbe anazushiwa mengi na wabaya wake, wapinga Mapinduzi wasioitakia mema Zanzibar. Kanali Seif Bakari (marehemu), ambaye wakati huo alikuwa pia Naibu Waziri wa Ulinzi, alijitahidi mno kumwokoa Rais Jumbe kikaoni humo bila mafanikio, lakini baadaye akaishia kuwekwa chini ya ulinzi nyumbani, na hatimaye kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa zaidi ya miezi sita.

Kwa kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa CCM, na kwa kutumia pia udhaifu wa Wazanzibari, kama ulivyojidhihirisha wakati huo kwa utengano wao, wivu na chuki miongoni mwao kwa wao, ilikuwa rahisi kwa Mwalimu kumtungua Rais Jumbe bila sauti ya umoja kutoka Zanzibar, na saa ilipowadia; akavuliwa nyadhifa zake zote za uongozi kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya makala haya.

Tetemeko na mafuriko yakawakumba pia wasaidizi wake wa karibu, wakiwamo aliyekuwa Waziri Kiongozi, Ramadhani Haji; Waziri wa Nchi wa Zanzibar, Aboud Talib, ambapo Mwanasheria Mkuu Mteule wa Rais Jumbe, Jaji Bashir Swanzy, alifukuzwa Zanzibar kwa taarifa ya saa 24 na kurejeshwa kwao Ghana.

Naye Jaji Dourado, kama ilivyokuwa kwa Rais Jumbe na Kanali Seif Bakari, aliwekwa kizuizini kwa miezi sita, kisha ikatangazwa sawia hali ya hatari kisiasa, maarufu kama ‘kuchafuka kwa hali ya hewa Visiwani.’ Mambo ya Usalama wa Taifa, ambayo kabla ya hapo hayakuwa jambo la Muungano (ilikuwa ni Ulinzi tu), yakaingizwa kwenye Katiba kuwa jambo la Muungano, na kwa hiyo ikasomeka ‘Ulinzi na Usalama’ ili kudhibiti zaidi hali hiyo. Kufikia hapo, ilikuwa ushindi mkubwa kwa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ dhidi ya kambi ya ‘Wakombozi.’

Mwandishi wa makala haya, ambaye alikuwa mmoja wa Vijana wa CCM kutoka Tanzania Bara, walioshiriki kwenye zoezi la kulegeza na kudhibiti mkakamao wa hali hiyo tete Visiwani, kwa lengo la ‘kusafisha’ hewa iliyochafuka, alishuhudia jinsi kambi hizi mbili zilivyokamia kuumizana, licha ya Zanzibar kupata Rais mpya, Sheikh Ali Hassan Mwinyi; huku kambi ya ‘Wakombozi’ iliyoshindwa ikiapa kulipiza kisasi kwa ‘Wanamstari wa mbele’ na kwa Mwalimu Nyerere pia. Nafasi hiyo ilikuja pale Mwalimu Nyerere alipotangaza nia yake ya kung’atuka mwaka 1985 na kutafuta mrithi wake.

Nyerere aandaa mrithi wake
Kifo cha Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Dk Salim Ahmed Salim, kilimweka Mwalimu njia panda kuhusu uteuzi wa mrithi wake baada ya yeye kung’atuka. Ili kuweka mzani wa kidiplomasia za kimuungano sawa na kwa lengo maalum, iliazimiwa kwamba Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano, atoke Zanzibar. 

Na katika kutekeleza lengo hilo, nafasi za wagombea zilidhibitiwa kuwa watatu tu. Nao walikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Muungano na pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Ali Hassan Mwinyi; Waziri Mkuu wa Muungano na Mjumbe wa NEC na Kamati Kuu (CC) ya CCM, aliyekuwa na nguvu kubwa kisiasa wakati huo, Dk Salim Ahmed Salim; na Mjumbe mwingine wa NEC na CC, aliyekuwa na nguvu kubwa pia kisiasa, Rashid Mfaume Kawawa.

Ukimwacha Kawawa ambaye alikuwa anatokea Bara, Mwinyi na Dk Salim ndio pekee walikuwa Wazanzibari, na hivyo kufifisha dhamira nzima kwamba Rais wa Awamu ya Pili atoke Zanzibar. Mwinyi, pamoja na kuzaliwa Kisarawe (Tanzania Bara), alikulia na kusomea Zanzibar. Na kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Mtanzania yeyote aliyeishi Zanzibar kwa miaka sita mfululizo, anastahili kuitwa Mzanzibari; na ndivyo ilivyokuwa kwa Mwinyi.

Mwalimu Nyerere alikuwa na mtihani mgumu kumpata mrithi kutokana na vigogo hao watatu waliokuwa na sifa na nguvu sawa katika siasa za Tanzania enzi hizo. Kwa hiyo, akaanzisha mchezo wa karata na ushawishi katika ngazi za juu za Chama, lakini bila rushwa wala matumizi ya fedha kama ilivyo siku hizi ndani ya CCM.

Ikumbukwe kwamba katika ngazi hizo za juu, kwa maana ya NEC na CC ya CCM, zilikutanishwa kambi mbili zenye kuhasimiana juu ya ukuu wa kisiasa Zanzibar. Kambi hizo zilikuwa ni zile zile za ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoongozwa na Brigedia Abdullah Said Natepe. Wengine walikuwa ni Ali Mzee (aliyekuwa Waziri wa Nchi (Serikali ya Muungano), Hassan Nassoro Moyo (aliyekuwa Waziri wa Kilimo Zanzibar), Mohammed Seif Khatib (aliyekuwa Katibu Mkuu na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM), pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano, Dk Salmin Amour Juma.

Kambi hii ilikuwa pia na maofisa wastaafu wa Jeshi na Usalama wa Taifa. Hao walikuwa ni pamoja na Brigedia Mstaafu na Waziri Kiongozi wa zamani, Ramadhan Haji (aliyeng’olewa pamoja na Jumbe) na Mkuu wa Jeshi la Zanzibar, Brigedia Khamis Hemed.

Kambi hiyo ya Wakombozi ilikuwa bado ikipiga kampeni kushinikiza kuachiwa kutoka kizuizini mtu wao, Kanali Seif Bakari, pamoja na Mjumbe mwingine wa zamani wa Baraza la Mapinduzi, Hafidh Suleiman, ambao hao wawili walikuwa sehemu ya watesi maarufu (Genge la watu 14) na vinara wa ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji enzi za utawala wa Abeid Amani Karume.

Kwa upande wa kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ ilikuwa na Dk Salim Ahmed Salim, Seif Shariff Hamad (wakati huo Waziri Kiongozi), Hamad Rashid) wakati huo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Muungano) na Khatib Hassan. Wengine walikuwa ni Kanali Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu, Shaaban Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu, ambao wote walikuwa Wajumbe wa NEC ya CCM. 

Kambi ya ‘Wakombozi’ ilijua mapema chaguo la Mwalimu Nyerere ni Dk Salim Ahmed Salim kuwa kumrithi wake. Kambi hiyo ikaona hiyo ilikuwa ni nafasi nzuri kulipiza kisasi kwa majeraha iliyopata kutokana na mtu wao Aboud Jumbe, kuondolewa madarakani.

Mwalimu akwaa kisiki kuteua mrithi

Tangu mwanzo, kambi hii ya ‘Wakombozi’ ilikuwa na chuki ya kudumu dhidi ya Dk Salim kwa sababu za kisiasa na kijamii. Mwaka 1982, wakati Dk Salim alipoteuliwa na Mwalimu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Brigedia Natepe (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa) na Ali Mzee (wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais), walikwenda kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Sokoine, wakadai kwamba walikuwa na maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe na Kanali Seif Bakari, ya kuzuia Dk Salim asiwe Waziri wa Mambo ya Nje.

Walitoa sababu mbili. Mosi, kwamba kuna makubaliano ya siri tangu enzi za Karume, kwamba wanachama wa zamani wa vyama vya zamani vya siasa mbali na ASP, na ndugu zao, wasipewe nafasi za uongozi katika Chama, Serikali ya Zanzibar wala katika Serikali ya Muungano; bali watumike kwa shughuli za kitaalam tu.

Dk Salim alikuwa mmoja wa viongozi wakuu wa chama cha siasa cha mrengo wa kushoto (Ki-Marxist/Kikomunisti) cha Umma Party kilichofanikisha Mapinduzi ya 1964 kwa kushirikiana na ASP, kisha akateuliwa na Karume kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Misri, chini ya Serikali ya mseto kati ya ASP na Umma Party. Pili, walidai kwamba rangi ya ngozi ya Dk Salim iliwakumbusha Wazanzibari, kwa kilio cha kusaga meno, utawala wa Sultani aliyepinduliwa Januari 12, 1964.

Sokoine, Waziri Mkuu ambaye hakupenda mzaha wala majungu, aliwafukuzia mbali viongozi hao. Kuanzia hapo, nyota ya Dk Salim ilizidi kung’ara na hatimaye kumrithi Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari miaka minne baadaye.

Mikakati ya ‘Wakombozi’ kumzuia Dk Salim asimrithi Mwalimu Nyerere ilikuwa thabiti ikihusisha vigogo wa Visiwani na Bara pia. Wasukaji wa mikakati Visiwani, walikuwa ni Hassan Nassoro Moyo, Natepe, Ramadhan Haji na Aboud Talib, kwa kumshirikisha mwanamkakati kiungo chao Tanzania Bara, Waziri wa Utalii wa wakati huo, Paul Bomani, aliyeunda na kuongoza kikosi cha Wajumbe wa NECwa Bara dhidi ya Dk Salim. 

Mwalimu Nyerere alijua yote haya, lakini hakujihusisha kupiga kampeni kwa kuheshimu demokrasia na misingi ya uongozi bora. Mwinyi alifuatwa na ‘Wanamstari wa mbele’ siku ya uteuzi na kushauriwa, naye akakubali, kujitoa katikati ya mchakato ili kumwachia Mzanzibari mwenzake, Dk Salim.

Walidhani wamemshawishi vya kutosha kufikia uamuzi huo, lakini mambo hayakuwa kama walivyotarajia siku ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM cha kuteua mgombea, hapo Agosti 12, 1985. Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijitoa kugombea, kwa hiyo wakabakia wawili. Mwinyi na Salim wakatoka nje ili wajadiliwe, lakini hadi hapo bila dalili zozote za Mwinyi kujiengua.

‘Wakombozi’ wa Visiwani na maswahiba wao wa Bara, walitumia vizuri nafasi waliyopewa na hivyo kutawala mazungumzo, huku Moyo na Natepe wakiongoza. Mjumbe mwingine aliyezungumza, alikuwa Getrude Mongella, wakati huo akiwa pia Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (kikulacho kinguoni mwako?) na mpambe mku wa Bomani kwa kampeni za Bara.

Hoja ya Mongella ilikuwa kwamba kumwacha Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, na kumteua Dk Salim, kungetafsiriwa vibaya kitaifa na kimataifa kwamba Watanzania hawaheshimiani kiuongozi. Kamati kuu ikamteua Mwinyi. Kambi ya ‘Wakombozi’ ikachekelea kwa ushindi.

Bado ilitarajiwa kuwa Mwinyi angejitoa baada ya hapo, lakini hakufanya hivyo. Akajikausha chini ya mkazo wa macho ya ‘Wanamstari wa mbele’ waliotarajia afanye hivyo. Kinyume chake, alipojulishwa juu ya kuteuliwa kwake kikaoni humo, jibu lake lilikuwa rahisi na fupi. Alisema: “Kama hayo ndiyo matakwa ya watu, nakubali.” Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere hakupinga. Tayari alikuwa amekwaa kisiki cha ‘Wakombozi,’ wakafanikiwa kulipiza kisasi chao kwake.