Mfumuko wa bei kwa mwezi Julai 2016

Ephraim Kwesigabo (kulia) na Kushoto ni Kaimu Meneja, Idara ya Takwimu ya Ajira na Bei, Ruth Minja
Na Dotto Mwaibale

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2016 umepungua hadi asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 ilivyokuwa mwezi Juni, 2016.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwekisigabo wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu mfumuko wa bei wa taifa wa mwezi Julai, 2016.

"Hii inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2016" alisema Kwesigwabo.

Kwesigabo alisema kuwa Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 103.50 Mwezi Julai, 2016 kutoka 98.48 mwezi Julai 2015 na kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi mwezi Julai 2016 umepungua hadi asilimia 7.6 kutoka asilimia 8.1 ilivyokuwa mwezi Juni, 2016.

Kwesigabo aliongeza kuwa kupungua kwa mfumuko huo wa bei wa mwezi Julai 2016 kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Julai, 2016 zikilinganishwa na bei za mwezi Julai 2015.

Alisema mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilionesha kupungua ni pamoja na bei za samaki kwa asilimia 6.6, mafuta ya kupikia kwa asilimia 4.9 na maharage kwa asilimia 1.9.

Aliongeza kuwa kwa upande mwingine mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa ziliso za vyakula zilionesha kupungua ni pamoja na bei za gesi kwa asilimia 21.5, mafuta ya taa kwa asilimia 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3

Alisema pamoja na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 kuna baadhi ya bidhaa zilionesha kuongezeka katika kipindi hicho zikiwa ni pamoja na bei za mchele kwa asilimia 4.7, mahindi kwa asilimia 31.6, unga wa mahindi kwa asilimia 24.1, vyakula kwenye migahawa kwa asilimia 15.6 na mkaa kwa asilimia 16.0.
  • Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062