Michezo 10 Inayosubiriwa kwa Hamu msimu Mpya wa NBA

Ligi ya mpira wa kikapu Marekani (NBA) ambayo inaongoza kwa kutazamwa zaidi duniani imetangaza ratiba ya msimu mpya utakaoanza mwezi Oktoba (unaweza kuisoma kwa kubofya hapa) Kama ilivyo ada kila msimu unakuwa na michezo inayosubiriwa kwa hamu ikitumiwa kama kipimo cha namna timu zitakavyofanya kwenye hatua ya mtoano, na hii ni 10 bora kati ya hiyo.

Oct 25: CAVS kwa KNICKS
Mabingwa wa msimu uliopita Cavs wanakutana na kigingi cha kwanza watakapoifuata Knicks ambayo imeongeza nguvu baada ya kumchukua MVP wa za zamani Derrick Rose na Joachim Noah toka Chicago Bulls.

Oct 25: SPURS kwa WARRIORS
Hiki kitakuwa kipimo kizuri kwa Golden State ambao msimu uliopita walikata pumzi mwishoni, tutajua kama Big 4 mpya ya Curry, Klay, Green na Durant itafika mbali watakapokutana na kati ya timu bora kabisa kwenye ligi San Antonio Spurs. Itakuwa pia kipimo kwa Spurs ambayo kuona wapoje baada ya Tim Duncan kustaafu.

Nov 3: OKC kwa WARRIORS
Kama kuna usajili uliogusa hisia za wengi offseason hii basi itakuwa ni wa Kevin Durant alieondoka OKC kwenda Warriors. Kuna waliomuona kama msaliti, wengine wakamchukulia kama askari anaeamua kuhamia kwa adui baada ya kuona silaha nzuri nk. Lakini mwisho wa yote kinachosakwa ni ubingwa hasa ukizingatia kwa miaka mitano mfululizo Thunder wamekuwa wakikata pumzi mwishoni. Novemba 3 ndio siku KD anakutana na marafiki zake wa zamani.

Nov 10: CHICAGO BULLS kwa MIAMI HEAT
Kivutio kwenye mchezo huu atakuwa Dwayne Wade ambaye aliichezea Heat kwa misimu 13 mfululizo kabla ya kuhamia Bulls na hii ikiwa mara ya kwanza anarejea American Airlines Arena ambako ana heshima kubwa . Kila mtu atataka kuona mashabiki wa Heat watampokea vipi Flash au Father Prime.

Nov 18: WARRIORS kwa CELTICS
Boston Celtics nusra iivunje rekodi ya Warriors kutopoteza mchezo hata mmoja msimu uliopita kabla ya kuwa timu ya kwanza kuichapa Golden State nyumbani kwake. Mechi nzuri kuipima Celtics imeimarika wapi zaidi.

Dec 25: WARRIORS kwa CAVALIERS
Tuseme ukweli tu, huu ndio mchezo utakaosubiriwa kwa hamu zaidi na pengine kwa kutambua hilo NBA wakaamua kuuweka siku ambayo watu wengi wanakuwa majumbani na familia zao, siku ya Krismasi. Inazikutanisha timu mbili zilioingia fainali msimu uliopita huku Golden State ambao walionekana kama wanabeba ubingwa baada ya kuongoza 3-1 wakikata ring na Cavs ikiongozwa na LeBron ikibeba ndoo kwa 4-3. Curry, Klay, Green na Durant vs LeBron, Kyrie, Love na JR.

Dec 25: CLIPPERS kwa LAKERS
Inaitwa The Battle of LA ikizikutanisha timu za jiji moja na zote zikiitumia Staples Centre kama uwanja wa nyumbani. Lakers ikiwa na kocha mpya Luke Walton na ikiwa imechukua wachezaji wazuri wakati wa NBA draft itakuwa na kazi ya kufuta uteja kwa Clippers ambayo ina wakongwe kama Chris Paul, Blake Griffin na DeAndre Jordan.

Jan 29: OKC kwa CAVALIERS
Russell Westbrook atakuwa na kazi ya kuwaongoza OKC watakapokutana na mabingwa watetezi Cavs kitu ambacho tulizoea kuona akikifanya akiwa na Kevin Durant.

Feb 3: LAKERS kwa CELTICS
Miaka kadhaa nyuma hili lilikuwa kama pambano la watani wa jadi ingawa kwa siku hizi imepoteza mvuto kutokana na timu zote mbili kutofanya vizuri hasa Lakers ambayo kwa misimu kadhaa imeshindwa hata kuingia Playoffs. Hata hivyo tutatataka kujua kama wana jipya hasa ukizingatia timu zote mbili zimeongeza nguvu offseason.

CAVS kwa SPURSTimu mbili kwenye ligi zinapokutana inakuwa nafasi nzuri ya kuangalia na kuwapima wachezaji bora nap engine kutabiri mechi za mtoano zitakavyokuwa. Mechi hii inasubiriwa kwa hamu na wengi.

HIZO ndio game kali zaidi za kutegemea msimu ingawa hali inaweza kubadilika kutegemea na msimu unavyokwenda kama Toronto Raptors walivyofanya msimu uliopita. Kwa wale wanaofuatilia NBA wakiwa Afrika kama mimi anza kujiandaa kwa mkesha.

Makala hii imeandikwa na Shafiq Mpanja ambaye ni mpenzi wa mkubwa wa mchezo wa kikapu. Unaweza kumpata katika mtandao wa Twitter @Tanganyikan