Mkuu wa Mkoa aagiza Walimu Wakuu WOTE wa mkoa wavuliwe madaraka

Habari kuu kutoka katika Mkoa wa Simiyu, ni kuhusu agizo la Mkuu wa Mkoa huo Antony Mtaka, la kuwavua madaraka wakuu wa shule zote za msingi na sekondari za serikali, mkoa mzima kutokana na kubainika uwepo wa idadi kubwa ya wanafunzi hewa.

"Mkoa wa Simiyu una jumla ya shule za msingi za serikali 516 na shule za sekondari za serikali 140, ambapo jumla ya walimu wakuu wa shule zote wapatao 656 watavuliwa madaraka yao kuanzia sasa".

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka amewagiza Katibu Tawala Mkoa huo Jumanne Sagini, kuwavua madaraka mara moja wakuu wote wa shule za sekondari Mkoani humo 140 kutokana na kugundulika uwepo wa wanafunzi hewa.

Mbali na hilo Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza kuwa mara baada ya kufanyika mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka huu kwa shule za Msingi 516, wakuu wote wa shule hizo nao ameagiza wavuliwe nafasi hizo mara moja.

Mtaka alisema kuwa katika zoezi la uhakiki wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari Mkoa mzima, taarifa za awali zimeonyesha mpaka sasa katika shule za sekondari wamebainika kuwepo wanafunzi hewa 2331.

Zoezi hilo bado linaendelea katika shule za msingi, ambapo wilaya ya Baraidi, kwa taarifa hizo za awali, haina wanafunzi hewa kwa shule za sekondari.

Itilima imekutikana na wanafunzi hewa 2,137, Busega 110, Maswa 14, pamoja na Meatu 121. Zoezi bado linaendelea.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuvuliwa madaraka kwa walimu wote wakuu shule za msingi na sekondari, ni kutokana na kuwepo kwa wanafunzi hewa ambao kila mwezi fedha zao zilikuwa zikitumwa, huku zaidi ya milioni 10 kila mwezi zikipokelewa kwa wanafunzi hewa.

Mbali na kuvuliwa nafasi zao, katika shule ambazo wanafunzi hewa wamebainika hatua kali za kisheria amesema kuchukuliwa mara moja kwa walimu hao ikiwa ni pamoja na kurudisha pesa hizo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa uteuzi wa wakuu wapya wa shule zote mkoa mzima utafanyika chini ya uangalizi mkubwa, ambao vyombo vya ulinzi na usalama vitahusika katika kupatika kwa walimu wenye vigezo.

Alisema utafanyika usaili na vyombo hivyo ngazi za wilaya pamoja na mkoa, ambapo wataangaliwa uwezo wao wa kazi, taaluma zao, uwajibikaji, uwezo wa kuongoza, tabia zao pamoja na sifa.

"Katika uteuzi hakuna mtu kuingizwa kinyemela, wala kwa upendeleo, kila mmoja atachunguzwa kabla ya kumteua ili tuwapate watu watakao weza kuongoza shule na pesa za serikali" Alisema

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa mara baada ya zoezi hilo kufanyika, zamu itaamia kwa waratibu elimu kata mkoa mzima, ikiwa pamoja na maofisa idara ya elimu katika ofisi ya afisa elimu halmashauri.

Alisema waratibu elimu watafanyiwa uhakiki na uchunguzi mkali, ili kubaini wazembe na wabadhilifu ikiwa pamoja na kuteua wapya.

MWISHO.