Muhimbili kutumia mitandao ya simu, kadi za benki kwa malipo ya huduma za tiba

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutumia mitandao ya simu, kadi maalimu na kadi za benki kwa ajili ya kulipia huduma za matibabu ili kudhibiti changamoto za upotevu wa fedha na wizi katika ukusanyaji wa mapato ya hospitali hiyo.

Mpango wa kutumia njia za kieletroniki umelenga kukusanya mapato zaidi ili kuiwezesha hospitali hiyo kukabiliana na changamoto mbalimbali za uendeshaji na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Lengo la hospitali hiyo ni kuongeza mapato na kupunguza matumizi na kutengeneza mazingira ya kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wagonjwa mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja, Bwana Aminiel Aligaesha, hospitali hiyo imelenga pia kuimarisha njia za ukusanyaji mapato ili kuboresha huduma za matibabu na kuboresha maslahi kwa wafanyakazi.
“Hospitali imelenga kuboresha wadi za kulaza wagonjwa wanaohitaji huduma na malazi binafsi, kuhakikisha wagonjwa wanachangia huduma za matibabu na kuboresha mfumo wa kuandaa hati za madai kwa kampuni na mifuko ya Taifa ya bima ya afya.
“Hospitali imekusudia kutoa motisha na kuwahamasisha madaktari kuwaona wagonjwa kwa wingi wanaolipia huduma ili kuwavutia kutibiwa katika hospitali hii,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba hospitali hiyo imedhamiria pia kutoa motisha kwa wafanyakazi wengine ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Katika hatua nyingine, hospitali hiyo imeweka mikakati ya kupunguza gharama za kununua dawa na vifaa tiba kutoka viwandani (Manufacturers) moja kwa moja.
“Kwa mfano, baada ya kupata kibali kutoka TFDA, Hospitali imenunua dawa za figo (immunosuppressant) kutoka India kwa Sh 226 milioni wakati hapa nchini zingegharimu Sh 500 milioni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, hospitali hiyo imeagiza nyuzi za kushonea wagonjwa (sutures) kutoka kiwandani (Ethicon) kwa gharama ya Sh 321 milioni wakati zingegharimu Sh 668 milioni endapo zingenunuliwa nchini.

Katika taarifa hiyo imebainisha kuwa hospitali hiyo imeweza kupunguza gharama za uchujaji wa damu (dialysis) kutoka wastani wa Sh 250,000 kwa kila zamu (session) hadi kufikia Sh171,000.
  • Imeandikwa na John Stephen, MNH.