Ndoa za utotoni: Waziri wa Sheria atamka sababu serikali kukata rufaa

Wakati vuguvugu la kupinga hatua ya Serikali kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu kutaka umri wa kuolewa uongezwe hadi miaka 18, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema wamefikia uamuzi huo ili kupata uamuzi wa Mahakama ya Rufani ambao hautaweza kubadilishwa na hivyo kuwa kama Sheria.

Dk Mwakyembe amesema Serikali haipingi uamuzi hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, ila inatumia utaratibu wa kawaida utakaoiwezesha Serikali kuwa na uamuzi kutoka chombo cha juu cha Mahakama nchini. Alisema chombo hicho kikitoa uamuzi hautaweza kutenguliwa na mtu au chombo chochote.

Hivi karibuni, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu ambayo ilisema vifungu namba 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike aolewe akiwa na umri wa miaka 14 au mzazi kubariki ndoa akiwa na miaka 15, vinapingana na Katiba. Kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na mwanaharakati, Rebecca Gyumi na kusimamiwa na Mwanasheria, Jebra Kambole ulivuta hisia za wengi za kutengeneza historia mpya ya kumlinda mtoto wa kike nchini.