Nguzo za "The Stone Age" Isimila hatarini kutowekaNa Frank Leonard

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Annastazia Wambura ameiomba Idara ya Mambo ya Kale kutafuta wataalamu wa miamba watakaosaidia kunusuru nguzo za asili (pillars) za eneo la kihistoria la Zama za Mawe za Kale la Isimila wilayani Iringa zisipotee kutokana na mmomonyoko.

Wambura alitoa ombi hili juzi baada ya kutembelea kivutio hicho cha utamaduni mkoani Iringa katika ziara yake ya siku mbili iliyompeleka pia katika Makumbusho ya Chifu Mkwawa na katika eneo la Kikongoma Kalenga ambako mama yake chifu huyo alijiua ili asitoe siri ya nguvu za mwanae huyo aliyewashinda wajerumani katika vita ya mwaka 1891.

“Naona baadhi ya nguzo zimeanguka na zingine zipo katika hatari ya kuanguka, kuna haja ya kulinda kivutio hiki. Tutumie wataalamu wa miamba watushauri kama kuna uwezekano wa kutumia teknolojia yoyote ile kuzilinda zisiendelee kuathiriwa na mmomonyoko,” alisema.

Awali Meneja Msaidizi wa Mradi wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini (Fahari Yetu), Jimson Sanga alisema; “kama mamlaka zinazohusika zitaweka azimio la dhati, kuna uwezekano wa kutunza nguzo hizo kwa njia ya kisayansi.”

Pamoja na kufikiria kuzitunza nguzo hizo na kivutio hicho kwa ujumla wake, Sanga alisema kuna haja serikali ikashirikiana kwa makubaliano maalumu na wawekezaji wenye nguvu kifedha na kitaalamu kuliendeleza eneo hilo ili livutie watalii wengi zaidi.

Afisa Mhifadhi wa Zama za Mawe za Kale, Hillary Jabiri alisema idadi ya watalii wanaotembelea bonde la Isimila lilikaliwa na watu miaka milioni tatu iliyopita siyo ya kuridhisha kwasababu ya changamoto zake mbalimbali.

“Mbali na kutotangazwa kama vinavyotangazwa vivutio vingine, hasa hifadhi za Taifa, miundombinu ya kivutio hiki sio rafiki sana kwa wageni wanaotembelea kwahiyo kuna haja ya kuliangalia hilo,” alisema.

Mbali na nguzo za asili, alisema katika bonde hilo kuna zana za mawe za kale kama mikuki iliyotumiwa na watu hao wa kale kujihami, visu, shoka, nyundo na nyembe.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema; “eneo la Isimila ni kivutio cha aina yake kinachoweza kuvuta wanafunzi, watafiti na watalii wengi tofauti na hali ya sasa.”

Alisema ili kuinua sekta ya utalii katika wilaya yake, ataitumia ofisi yake kutengeneza utaratibu utakaohusisha wanahabari na vyombo vyao vya habari kutangaza vivutio vyote wilayani humo.

Pamoja na kuvitangaza alisema watahakikisha miundombinu ya kwenda katika vivutio hivyo inaboreshwa ili kuwavutia watalii wengi zaidi.