NW Amsimamisha kazi Mku wa CHuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala

NW Stella Manyanya (kushoto) akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bi. Levina Mrema (kulia).
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhandisi Stella Manyanya amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala kilichopo Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu Bw. Ramadhani Said, kutokana na utendaji usioridhisha na kumteua Bi. Levina Mrema kushikilia wadhifa huo kwa muda, wakati taratibu zingine zikiendelea.

Mhandisi Manyanya amechukua uamuzi huo alipopokea taarifa baada ya kutembelea chuo hicho alipokuwa katika ziara yake Mkoani Simiyu, ambapo amesema hajaridhishwa na utendaji kazi katika chuo hicho kikongwe kilichofunguliwa rasmi mwaka 1978 ambacho kwa sasa kina watumishi 10 wanaolipwa mshahara na Serikali kwa kuwahudumia wanafunzi 8 tu.

“Nimepata taarifa kuwa kuna wakati chuo hiki hakina wanafunzi kabisa lakini watumishi mpo na mnaendelea kulipwa mshahara na Serikali, kwa nini vyuo vingine vina wanafunzi hiki cha kwenu hakina wanafunzi?Wewe kama Mkuu wa Chuo umefanya jitihada gani kuhakikisha chuo kinakuwa na wanafunzi wa kutosha? Maana chuo siyo majengo tu”, alisema Manyanya.

Manyanya amesema amemteua Levina Mrema kuwa Kaimu Mkuu wa Chuo hiki, kwa kipindi cha matazamio kwa miezi sita ili atumie uzoefu wake kuja na mawazo mapya akishirikiana na uongozi wa Mkoa na wilaya kukifanya chuo kinarudi katika hadhi yake.

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho Ramadhani Said amesema amefanya jitihada za kukitangaza chuo lakini wanafunzi wanapofika chuoni wanaondoka baada ya kukutana na changamoto ya miundombinu chakavu ya majengo,ukosefu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na ukosefu wa umeme.


Aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Bunamhala Ramadhani Saidi (Aliyesimama) akitoa maelezo juu ya chuo hicho kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (hayupo pichani) wakati wa ziara yake.


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (katikati) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) wakati alipokuwa akikagua miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala Mjini Bariadi, wakati wa ziara yake Mkoani humo, (kulia) ni Mkurugenzi wa VETA Kitengo cha Masoko, Ajira na Mipango Enock Kibendera


Watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Bunamhala Mjini Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (hayupo pichani) wakati wa zira yake ya siku moja mkoani humo