Polisi Iringa yaanza msako wa wacheza bao, wanywa pombe asubuhi

Jeshi la polisi mkoa wa Iringa limeendelea na utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuwakamata wote wanaokunywa pombe asubuhi na wale wanaoshinda vijiweni wakiwemo wacheza bao asubuhi.

Msako huo umepokelewa kwa hisia tofauti kwa baadhi ya wananchi wa mji wa Iringa kutaka msako huo usiwakamate wauza pombe asubuhi kwa madai kuwa ni kazi yao inayowaingizia kipato na huku baadhi wakitaka wanywa pombe asubuhi wasikamatwe kwa kuwa wao ni wahitaji.

Wakizungumza na MtukioDaimaBlog baadhi ya wananchi ambao hawakupenda majina yao kuanikwa hapa walisema sehemu kubwa ya watu wamekuwa wakijishughulisha na biashara ya kuuza pombe na hivyo kuwakamata ni kutowatendea haki.

Baadhi ya wanywaji wamedai kukamatwa kwao ni kuwaonea kwani ilipaswa wakamatwe wauzaji.

Siku za hivi karibuni MtukioDaimaBlog imeshuhudia kazi nzuri inayofanywa na jeshi la polisi kwa kuwakamata wale wote wanaokunywa ama kuuza pombe asubuhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais.