RC aagiza muuguzi afutwe kazi kwa kuchelewa kumhudumia mtoto aliyebakwa

UPDATE: Video

Mtoto (5) ambaye ni mwanafunzi wa shule mmoja mjini Iringa mkazi Kihodombi katika Manispaa ya Iringa akiwa na mzazi wake wakisubiri matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa
MKUU wa mkoa wa Iringa Amina Masenza ameagiza kufutwa kazi mmoja kati ya wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa baada ya kuchelewa kumhudumia mtoto wa miaka mitano aliyebakwa kwa zaidi ya masaa matano, inaripoti blogu ya MatukioDaima.

Mkuu huyo wa mkoa amefikia hatua hiyo baada ya kupigiwa simu ya viongozi wa serikali ya mtaa wa Kihodombi ambao walikuwa wakimlalamikia kuhusu ucheleweshwaji wa matibabu kwa mtoto huyo aliyebakwa na mtoto mwenzake wa miaka 16 mkazi wa Kihodombi mjini Iringa .

Mkuu huyo wa mkoa ambae alifika hospitalini hapo majira ya saa 8 alikwenda moja kwa moja eneo la OPD na kumkuta mtoto huyo aliyebakwa akisumbuka bila kupatiwa matibabu na baada ya kumuuliza mmoja kati ya wauguzi hao juu ya sababu ya mgonjwa huyo kutopewa kipaumbele kutibiwa, aliishia kupewa lugha chafu kutoka kwa muuguzi huyo hali iliyomkasilisha Mkuu huyo wa Mkoa na kujitambulisha.

Mbali ya kujitambulisha bado, mhudumu huyo alidai kila jambo linakwenda kwa utaratibu na kumtaka RC na mgonjwa huyo aliyebakwa kuwa na subira. Hali hiyo ilimfanya RC Masenza kuagiza mtumishi huyo afukuzwe kazi kwa kukosa maadili ya kazi yake.

Awali, MatukioDaimaBlog ilizungumza na watu ambao walidai kuwa mtoto huyo alibakwa mwendo wa saa 3 asubuhi wakati akipelekwa shule na mbakaji, ambaye hadi sasa yupo chini ya polisi.