Sekondari itakayofanya vyema Musoma Vijijini katika masomo ya sayansi kupewa mini bus na Mbunge


Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Sekondari zitakazofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi jimboni humo zitapatiwa zawadi ya basi dogo aina ya mini-bus.

Profesa Muhongo aliyasema hayo jimboni humo alipokuwa akitoa zawadi kwa washindi wa ngoma katika mashindano yaliyomalizika hivi karibuni jimboni humo.

Alisema rafiki zake alio soma nao nchini Ujerumani katika chuo kikuu cha Goettingen University na chuo cha Technical University of Berlin wameahidi kutoa zawadi hiyo kwa masharti makuu mawili ambayo aliyataja kuwa ni ufaulu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Hisabati na Baiolojia (PCM & PCB).

Sharti lingine lililotolewa na wadhamini hao ni kwamba ushindi wa daraja la kwanza yaani Division I ambapo inatakiwa wanafunzi wasipungue 8 na daraja la pili yaani Division II inapasa wasipungue wanafunzi 12.

Alisisitiza kwamba ushindani wa aina hiyo utaboresha elimu jimboni humo na hivyo kuwasisitiza walimu na wanafunzi jimboni humo kuongeza juhudi ili kushinda zawadi hiyo nono.

"Ushindani utaboresha elimu jimboni mwetu, tujitume tupate mafanikio," alisema.

Profesa Muhongo ameendeleza juhudi mbalimbali za kuhakikisha jimbo hilo linakuwa na maendeleo endelevu kwani amefanikisha kupunguza kero ya madawati jimboni humo na vilevile kuboresha sekta ya afya kwa kugawa madawa na gari za wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya jimboni humo.