Ujumbe wa Prof. Mbele kwa Polisi wa Tanzania Kuhusu UKUTA

Kwanza napenda kusema kuwa jamii yote inatambua kazi kubwa na muhimu inayofanywa na polisi katika kulinda usalama na mali za wananchi, pamoja na mazingira magumu na uhaba wa vitendea kazi unaowakabili polisi. Raia wema tunashukuru tunapoona polisi wakifanya doria mitaani, wakilinda sehemu muhimu kama mabenki, na kadhalika. Tunafurahi na kuwashangilia polisi wanapoweka mitego na kufanikiwa kuwanasa majambazi. Mioyo yetu inatulia tunapooa polisi wako kwenye mikutano wakilinda amani. Wakati wa kampeni mwaka jana, kwa mfano, tuliona polisi walivyokuwa wakilinda mikutano ya vyama vyote vilivyoshiriki kampeni. Hayo yote na mengine mengi ni ya kujivunia, na ni sherti tukumbushane.

Ninapenda kuongelea hali ya sasa inayotokana na azma ya CHADEMA kutangaza kuwa itafanya mikutano na maandamano nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta. Katika mazingira haya, tunawasikia viongozi wa CCM wakitoa vitisho dhidi ya kampeni hiyo inayoitwa UKUTA. Wanadai kuwa maandamano haya yanaashiria uvunjifu wa amani. Viongozi wa CCM wamefanikiwa kuliaminisha jeshi la polisi kuwa maandamano haya hayana nia njema bali kuharibu amani.
Napenda kusema kwamba hizi kauli za viongozi wa CCM ni za kijinga. Wananchi wanafahamu umuhimu wa amani. Ni wao ndio walinzi wakuu wa amani, kwa sababu wanajua kuwa wanaihitaji. Haijalishi kama wanachi hao ni wanaCCM au wapinzani. Haijalishi kama hawana chama. Wote tunataka amani.

Kauli za viongozi wa CCM kwamba CHADEMA wanataka kuharibu amani ya nchi hazina mashiko. Mheshimiwa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa CHADEMA, ni mfanyabiashara. Hainiingii akili kuwa mfanyabiashara asipende amani, kwani amani ikivunjika, biashara zake hazitapona. Duniani kote, tunaona jinsi vibaka wanavyopora maduka na kuharibu biashara wakati amani inapovunjika. Hapa Marekani, kwa mfano, ikivunjika amani katika mji wowote, tunaona katika jinsi vibaka wanavyopora maduka na kuharibu biashara. Amani ikivunjika, wafanyabiashara ni waathirika wakuu.

Watanzania tunaposikia kauli za viongozi wa CCM tunapaswa kujiuliza: Je, ni kweli kwamba Mbowe anataka kuharibu amani? Kama ni kweli, basi Mbowe atakuwa ni mfanyabiashara wa ajabu, tofauti kabisa na wenzake, kama vile akina Bakhressa, Mohammed Dewji, Reginald Mengi, na wauza chipsi mayai mitaani. Muuza chipsi mayai anataka amani. Sembuse mfanyabiashara mwenye biashara kubwa na mali nyingi kama Mbowe?

Duniani kote wafanyabiashara, wawekezaji, na wajasiriamali wanaombea amani. Wawekezaji hawapeleki mitaji kwenye nchi isiyo na amani. Tanzania tunajivunia amani, na tunawaalika wawekezaji waje. Kama kuna mtu mwenye maslahi makubwa katika kuhifadhi amani, ni mwekezaji na mfanyabiashara. Propaganda za CCM kwamba Freeman Mbowe anataka kuhujumu amani ni ujinga.

Ninasikitika kwamba polisi wamerubuniwa na propaganda za kijinga za viongozi wa CCM. Matokeo yake tunayaona. Polisi wanakiuka wajibu wao wa kulinda amani katika mikutano na maandamano. Sheria ya vyama vya siasa inatamka wazi kuwa chama chochote hakiruhusiwi kutumia vyombo vya dola kuvitisha au kuvikandamiza vyama vingine. CCM inakiuka sheria hiyo, na inalitumia jeshi la polisi kinyume na sheria. Hili ni tatizo kubwa, na jeshi la polisi linawajibika kujirekebisha.

---
Prof. J. Mbele via HapaKwetu blog