[update] Uongozi wa shule za Feza wasema hazitafungwa

Kauli ya serikali ya Agosti 13, 2016 kuhusu shule za Feza na wafanyabiashara kutoka UrurukiUONGOZI wa Shule za Feza nchini umeibuka na kukanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii, kuwa wao hawana uhusiano na Fethullah Gulen wala serikali ya Uturuki kwa vile hawajawahi kupokea misaada toka pande hizo mbili za uendeshaji na kuwa shule hizo hazitafungwa.

Kauli hiyo imetolewa baada ya hivi karibuni kuenea kwa uvumi kuwa shule za Feza zipo hatarini kufungwa kwa madai kuwa mmiliki wake ni yule aliyejihusisha na jaribio la kuipindua serikani nchini Uturuki.

Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hizo, Habibu Miradji aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari Kawe jijini Dar es Salaam leo asubuhi.

Alisema Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa Shule za Feza ni kama asasi zingine zilizosajiliwa kishera na serikali, hivyo ni mali ya watanzania.

“Shule za Feza zitabaki kuwa kiwanda cha kuzalisha wazalendo wa kitanzania na raia bora wa duniani, hivyo wazazi wanapaswa kuondoa hofu,” alisema.

Alisema toka mwaka 1995 shule hiyo imepata mafanikio ya kujenga shule za awali tatu, shule za msingi mbili, sekondari tatu na shule ya kimataifa moja.

Aliongeza kuwa huo ni uwekezaji wenye mchango katika kukuza pato la taifa, kutoka awamu ya pili, tatu, nne hadi awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.

Alisema shule ya Feza ni hazina kwa Tanzania kwani shule zake zimekuwa zikishika nafasi ya 10 bora toka mwaka 2004 hadi leo.

Alisema wanatoa wito kwa wazazi kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo kujua kinachoendelea kwenye shule husika kwa manufaa ya wanafunzi wetu na taifa bila kusikiliza uvumi huo unaoenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya shule hizo. --- Taarifa ya Dotto Mwaibale.

Serikali za Tanzania na Uturuki zashirikiana kupata taarifa kuhusu shule za Feza


Serikali imesema kwamba inaendelea kushirikiana na Serikali ya Uturuki ili kupata taarifa zaidi kuhusu wamiliki wa shule za Feza kuhusishwa na jaribio la kuipindua serikali ya Uturuki kama ambavyo imeripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alisema wanaendelea kuwasiliana na Serikali ya Uturuki kuhusu taarifa hizo ili kupata ukweli.

Balozi Mahiga alisema kuwa kumekuwepo na taarifa zinazohusisha wamiliki wa shule hizo na baadhi ya wafanyabiashara ambao walifadhili na kuongoza jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15, mwaka huu nchini humo.

“ Serikali inaendelea kufanya mawasiliano na Serikali ya Uturuki kupitia ubalozi wake hapa nchini ili tuweze kupata taarifa kuhusu kuhusishwa kwa wamiliki wa shule za Feza na baadhi ya wafanyabiashara katika jaribio la kuipindua serikali ya uturuki,” alisema Balozi Mahiga.

Aliongeza kuwa kwa sasa serikali ya Tanzania haiwezi kufanya uamuzi wowote kuhusu wamiliki wa shule ya Feza na wafanyabiashara wa uturuki waliopo hapa nchini.

Kuhusu wanafunzi wa kitanzania wanaosoma nchini humo, Balozi Mahiga alisema kuwa wamemuagiza afisa ubalozi wa Tanzania aliyepo Roma nchini Italia kufuatilia hatma ya wanafunzi katika vyuo vilivyopo kwenye miji ya Ankara na Instanbul baada ya kufungwa kwa shule na vyuo kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Bw. Yasemin Eralp, hivi karibuni alisema kuwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini mwake katika vyuo na shule zilizofungwa watahamishiwa vyuo vingine kuendelea na masomo yao.

Balozi Eralp alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kufungwa kwa baadhi ya vyuo na taasisi za kielimu zilizobainika kuwa na uhusiano na kikundi cha kigaidi cha Fetullah Terrorist Organization(FTO) kinachotajwa kufadhili na kuongoza jaribio la mapinduzi lililoshindwa hivi karibuni nchini humo.

Hivi karibuni Serikali inatarajia kukutana na balozi wa Uturuki nchini ili kujua ni vyuo vingapi vilivyofungwa nchini humo ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma katika vyuo hivyo ili kupatiwa msaada zaidi. ---Taarifa ya Abushehe Nondo na Immaculate Makilika.