Utawala wa sheria vs Sheria za utawala

Sakata linaloendelea kati ya Serikali na CHADEMA ni kilelezo cha wazi cha kutamalaki kwa sheria za utawala, badala ya utawala wa sheria nchini Tanzania.

Katika nchi ya kidemokrasia, ainisho la utawala wa sheria linasema utawala wa sheria ni hali ya kuweko vizuizi vya kisheria kuzuia maamuzi ya kiimla na udhibiti wa kisheria kwa ajili ya kumlinda mwananchi na kuwepo utaratibu na uwazi wa kisheria.

Katika nchi yenye utawala wa sheria huwezi kukuta mgongano kati ya sheria na maamuzi au matamko ya viongozi.

Kwa mfano, huwezi kukuta sheria inaruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa, huku viongozi wanaweka mpaka wa mikutano hiyo kwamba ifanyike katika maeneo ya viongozi husika tu au nyakati za uchaguzi pekee.

Viongozi wa vyama vyote vya siasa wako huru kwenda mahali popote pale katika nchi kufanya shughuli za kisiasa iwe ni kukutana na wanachama wao katika mikutano ya ndani au kukutana na wananchi katika mikutano ya hadhara.

Si busara hata kidogo kuwazuia viongozi wa vyama vya siasa wa kitaifa au hata kama si wa kitaifa kwenda sehemu yoyote ya nchi kufanya siasa, kwa sababu hiyo ndiyo kazi ya viongozi na chama cha siasa.

Utawala wa sheria maana yake ni kuhakikisha kutumika kwa sheria kama zilivyokusudiwa na siyo kuzipa tafsiri waitakayo watawala. Kufanya hivyo ndiko kunakohakikisha kwamba haki za wananchi zinalindwa na haki za watawala pia zinalindwa.

Kinyume cha utawala wa sheria ni kile kiitwacho ‘sheria za utawala’au kwa Kiingereza; ‘Law of rule’. Hali hii hutokea pale ambapo utawala unatoa amri zake kinyume cha sheria hali ambayo hukaribisha upinzani kutoka kwa wananchi.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa kada mbalimbali kwamba nchi yetu imeanza kubobea kidogo kidogo kwenye sheria za utawala.

Wataalamu wa mambo ya sheria na katiba wanasema kukosekana kwa utawala wa sheria na kutamalaki sheria za utawala, ni hali inayoweza kujitokeza katika nchi zote, zile za kidemokrasia na hata zile za kidikteta.

Ndiyo maana wakaja na msamiati “dictatorial democracy” yaani demokrasia ya kidikteta au ya kiimla kwa lugha nyepesi. Kinachoendelea katika nchi yetu hii ya kidemokrasia ni sheria ya utawala badala ya utawala wa sheria.