Viongozi zaidi ya 60 wa CHADEMA wakamatwa; Lema atoka rumandeViongozi wa CHADEMA zaidi ya 60 wakiwemo wabunge na viongozi wa kitaifa (Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti, Naibu - Bara, Naibu - Zanzibar) wamekamatwa leo na jeshi la polisi likiongozwa na OCD wa Oysterbay majira ya saa 9 wakiwa katika kikao cha pamoja cha kamati kuu kilichokuwa kikifanya katika Hoteli ya Giraffe.
Viongozi hao walifikishwa wa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati (Central) kwa mahojiano zaidi.

Akizungumzia hatua ya kukamatwa kwa viongozi hao, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), alisema wameshangazwa na hatua hiyo ambayo aliita ya uonevu.

Alisema hatua ya kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA si jambo la kushangaza kwani pamoja na hali bado hawajakata tama na wataendelea na harakati za kudai demokrasi ya kweli nchini.

Aliongeza kuwa kikao hicho kulikuwa na wajumbe 178 -- limearipoti gazeti la MTANZANIA.


Wakati huo huo, mjini Arusha inaripotiwa na TBC kuwa Mbugne wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefikishwa katika mahakama ya hakimu Mkazi wa mkoa huo na kusomewa kesi mbili zinazomkabili. Akisoma mashitaka hayo, mbele ya hakimu wa Mahakam hiyo, Desidery Kamugisha, Waziri wa serikali, Innocent Njau amesema Lema anakabiliwa na kesiya kumwandikia ujumbe wa vitisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha kupitia simu ya mkononi, huku kesi nyingine ikiwa ni kusambaza ujumbe wa sauti kupitia mtandao wa simu za mikononi wa kuhamasisha maandamano ya tarehe Mosi Septemba. Kesi imeahirishwa hadi Septemba 13, 2016 huku mtuhumiwa akiachiwa kwa dhamana kwa masharti ya kutokusafiri nje ya nji ila kwa kibali cha mahakama.

Huko mkoani Kilimanjaro katika wilaya ya Rombo, madiwani watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na mjumbe wa serikail ya kijiji cha wamefikishwa katika mahakama ya Rombo leo kwa tuhuma za uchochezi. Ripota wa habari wa Radio Sauti ya Injili akiwa Rombo amesema madiwani Nicholaus Kimario (Kata ya Kirongo Samanga), Anisia Mede (Viti Maalum) na Daudi Mlasini (Kingachi) na mjumbe wa Kirongo Samanga.

Kwamba, mwendesha mashitaka Bernard Machibya akisaidiana na mwendesha mashitaka wa polisi Stanslaus mbele ya Hakimu Mkazi, Naomi Mwirinde amedai kuwa watuhumiwa walitenda kosa kinyume na kifungu 55 (1) sura 16 kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marakebisho mwaka 2012 ambapo wanadaiwa tarehe 25 Agosti walifanya mkutano wa ndani huko Kirongo Samanga bila uhalali kwa kuhamasisha na kusababisha wananchi kuichukia mamlaka ya Jamhuri ya Muungano pamoja na serikali yake. Daudi Mlasani amedaiwa kufany akosa kama hilo huko Useri.

Washitakiwa walikana mashitaka yote. Waendesha mashitaka waliiomba mahakama iwanyime washitakiwa dhamana chini ya kifungu cha 148 (4) kwa hoja kuwa upepelezi wa awali haujakamilika, watuhumiwa wengine wanatafutwa na kuwa washitakiwa wakiachiwa watasababisha uvunjifu wa amani katika maeneo yao, ombi ambalo liliridhiwa na Hakimu hadi tarehe 5 Septemba siku kesi hiyo itakaposomwa tena.