Walimu Wakuu 90 S/M na Sekondari kuvuliwa vyeo kwa udanganyifu

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Salum Hapi, amesema kuwa walimu wakuu 68 wa shule za msingi na 22 shule za sekondari watavuliwa vyeo kwa kosa la udanganyifu wa takwimu za idadi za wanafunzi hewa tangu elimu itangazwe kuwa bure katika wilaya za Kinondoni na Ubungo --- imeripoti GPL.

Akizungumza na wanahabari leo ofisini kwake amemwagiza Katibu Mkuu Tawala wa Mkoa kuwavua walimu hao vyeo vyao na kuwapa walimu wengine kwa sababu ya kosa hilo.

Hapi alifafanua kuwa wakuu hao wamekuwa na wanafunzi hewa 2,534 kwa shule za msingi za wilaya ya Kinondoni.

Baadhi ya shule alizozitaja zilizo na wanafunzi hewa ni Bunju B yenye wanafunzi 155, Goba Mpakani wanafunzi 42, Hananasifu 154 na Boko wanafunzi 74 huku shule za sekondari zikiwa ni Msisiri B wanafunzi 395, Ubungo Msewe 267 na Upendo 273 na nyinginezo.