Waziri awasimamisha 2 kazi ATC

Waziri Profesa Makame Mbarawa akiendelea na ukaguzi wa wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Songwe , Mkoani Mbeya
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewasimamisha kazi viongozi wawili wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kwa tuhuma za kufanya ufisadi katika masuala ya uteuzi wa marubani wanaopaswa kwenda kusoma nje ya nchi.
“Leo asubuhi nimewasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu Kapteni,  Johnson Mfinanga wa ATC na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uendeshaji katika shirika hilo, Sadick Muze wa shirika hilo kwa sababu za kufanya kazi kwa kubabaisha’’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Marubani wanaozungumziwa, wanatarajia kuondoka kesho kuelekea nchini Canada kwa ajili ya mafunzo ya kurusha ndege mpya mbili zinazotarajiwa kuwasili nchini katikati ya mwezi ujao.

Waziri Mbarawa amechukua hatua hiyo leo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi walio chini ya Wizara yake katika Bandari ya Itunge, Wilaya ya Kyela na kusisitiza kuwa hataki wafanyakazi wababaishaji.

Prof. Mbarawa amesema baada ya kukamilisha malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mbili mpya kwa ajili ya ATCL alitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo kuwachagua marubani watano wenye vigezo ambavyo vinahitajika kwa ajili ya mafunzo hayo jambo ambalo amebaini mmojawapo wa waliochaguliwa hajatimiza vigezo.

Shirika la Ndege Tanzania katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa ndege tatu.
PROF. MBARAWA ASISITIZA TATHIMINI UWANJA WA NDEGE SONGWE

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali haitaendelea na ujenzi wa jengo la pili la abiria katika uwanja wa ndege wa Songwe uliopo mkoani Mbeya mpaka tume ya watalamu iliyoundwa kuchunguza ili kujiridhisha kama utaratibu ulizingatiwa kabla ya kuaza ujenzi huo.

Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo mara baada ya kukagua jengo hilo linalojengwa na mkandarasi wa Kampuni ya Db Shapriya ya Tanzania ambapo amesema hadhi ya jengo hilo hairidhishi hivyo ipo haja ya kujiridhisha kama taratibu zote zilifuatwa kabla ya ujenzi.

Amebainisha kazi ya tume hiyo ya wataalamu ni kuhakiki namna utaratibu wa kumpata mkandarasi ulivyofanywa, gharama halisi za mradi na fedha iliyolipwa kwa mkandarasi kama inaendana na thamani ya jengo hilo.
"Serikali haiwezi kutoa fedha ya kumalizia jengo hili kabla ya kujiridhisha ili kuhakikisha fedha tutakazozitoa zitatumika kulingana na ilivyopangwa na thamani ya fedha inaendana na jengo lenyewe", amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha Waziri Prof. Mbarawa ameeleza ili kuwa na miundombinu imara na ya kudumu ni lazima kuhakikisha miradi ya ujenzi wa miundombinu inasimamiwa vizuri na taratibu za kupata mkandarasi bora zinafuatwa.
"Kutokuwa na miundombinu isiyo imara ni sababu ya wahusika kuweka mbele maslahi binafsi na siyo ya Taifa", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa
Pia ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhakikisha makosa yaliyojitokezo kwenye ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza hayajirudii katika kiwanja hiki.

Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Songwe Bw. Hamisi Amiri amemhakikishia Waziri Mbarawa kusimamia ujenzi uliobaki kwa kuzingatia taratibu na makubaliano yaliyowekwa ili jengo hilo lidumu kwa manufaa ya Taifa na Mkoa.

Uwanja wa Songwe ni kiungo muhimu kwa wananchi wa mikoa ya Katavi, Rukwa, Njombe na Ruvuma na katika mwaka huu wa fedha umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la abiria na taa uwanjani hapo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Waziri Profesa Makame Mbarawa akiendelea na ukaguzi wa karakana ya Mbeya

WAZIRI MBARAWA ATOA AGIZO KUBOMOA NYUMBA ZILIZOPO KWENYE MIUNDOMBINU YA RELI NA BARABARA
Serikali imeiagiza Mamlaka ya Reli ya Tanzani na Zambia (TAZARA), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), zianze kubomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi ya reli na barabara kuu zote nchini ili kuilinda miundombinu hiyo isiharibiwe.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa mkoani Mbeya mara baada ya kukagua Daraja la Reli ya Tazara lililopo Mbalizi nje kidogo ya mji huo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kulinda miundombinu

“Sheria iko wazi, lazima muisimamie msisubiri mpaka Waziri aseme. Mwananchi yeyote aliyeifata miundombinu ya reli lazima mmvunjie nyumba yake ili miundombinu iliyojengwa kwa kutumia fedha nyingi iweze kudumu”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema Serikali ipo katika hatua za kuboresha miundombinu ya reli ya kati na reli ya Tazara ili kuhakikisha mizigo yote ya ndani na nje ya nchi inayopitia kwenye bandari ya Dar es Salaam na kupita katika barabara inapita katika reli.

“Mizigo inayopita katika reli ni asilimia 4 tu kutoka bandarini hivyo lazima tujipange kuanza kutafuta masoko na kuchukua mizigo hiyo ili kulinda miundombinu ya barabara inayoharibiwa na uzito mkubwa”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha Waziri Prof. Mbarawa ameuhimiza uongozi wa TAZARA kuongeza juhudi katika utoaji elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya uchimbaji mchanga, kokoto kwenye hifadhi ya miundombinu ya reli hasa kwenye mito na chini ya madaraja ili kuzuia uharibifu kuhatarisha usalama wa usafiri wa treni.

Naye Meneja wa TAZARA wa mkoa wa Tanzania Bw. Fuad Abdallah amemueleza Waziri Mbarawa zoezi la kubomoa nyumba litatekelezwa kama sheria ya reli inavyosema kwa wananchi kuacha ya mita 30 kwa vijijini na mita 15 kwa mjini.

Ameongeza kuwa mamlaka itaendelea kutoa elimu ya utunzaji wa miundombinu ili wawe sehemu ya utunzaji kwa kuacha kufanya shughuli zao kwenye maeneo hayo.

Katia ziara hiyo.

Aidha Prof. Mbarawa amekagua pia Karakana ya TAZARA ya Mbeya ambayo inatoa huduma ya matengenezo ya vichwa vya treni 39 aina ya Diesel Electric (DE) pekee na kubaini ukosefu wa baadhi ya mitambo, uchakavu wa mitambo iliyopo na ukosefu wa vipuri.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, 
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.