Zanzibar na siasa za pombe - Prof. Noor


Ndugu zangu,

Kila watu duniani wana mila na dasturi zao ambazo ni muhimu kuzilinda iwapo sharia hizo ni nzuri kwa jamii kwa jumla na zina manufaa kwa umma na iwapo haziwanyimi haki zao walio wachache. Sharia iliyowekwa na wakoloni wa Kiingereza ilitokana na Waislamu wenyewe walio wengi kutaka pawe na kizuwizi ambacho alitakiwa Muislamu akaombe na atoe sababu za kutaka kuingia madhambini kwa kulewa. Ilikuwa kama kuhakikisha kuwa huyo Muislamu anayetaka kulewa ana akili zake timamu. Ofisi ya D.C. ikiona kweli ana akili timamu, basi hupewa hiyo rukhsa ya kujitia madhambini. Khiyari ni yake mwenyewe. Pili, sharia hiyo ilitokana na Wazanzibari wake waliolalamika kuwa waume zao hutumia kipato chao kikubwa sana au chote katika ulevi na wake zao na watoto wakawa hawana hata chakula; na kuna sababu nyinginezo pia.

Iwapo mtu alikuwa si Muislamu, sidhani kuwa naye pia alitakiwa kuwa na liseni kununua ulevi. Na iwe iwavyo. Hapa kuna haki mbili zilikuwa zikilindwa. Ya kwanza ni haki ya anayetaka kulewa, na ya pili ya umma -- ambao sehemu kubwa kabisa ilikuwa ni ya Waislamu -- ambao mara nyingi husoneneka kwa vitendo na vitimbi vya walevi. Iwapo mtu ni mlevi na baada ya kulewe hufanya visa na miqasa ya kuudhi watu mitaani kwa maneno yake na vitendo vyake kama kutoa nyuchi zake hadharani na kwenda haja na huku wazee na vijana huyaona makruhi ayafanyayo, kiumbe kama huyo huwa hafai kulewa wala kupewa rukhsa ya kulewa maana haki yake ya kulewa inaingilia, pakubwa sana, haki ya umma wenye kuudhiwa na vitendo vyake vyenye kuvujna muruwa wa jamii. Na vijana wa kike na kiume huoneshwa vituko na kusikilizishwa kwa wasiyofaa kuyaona na kuyasikia kwa mujibu wa mila yetu. Na mila na dini yetu huwa zinapigwa dharba kubwa na chafu bila ya sababu. Uhuru wa mtu kulewa haina maana ya wengi kunyimwa uhuru wao wa kuishi maisha ya muruwa kwa kuingiliwa mitaani mwao na machafu ya walevi, hata iwapo si wote.

Fikiria jambo moja jingine muhimu linalokhusu uchumi wa mkoloni. Mkoloni wa Kiingereza alikuwa na mashirika yake mengi ya kutengenezea ulevi wa kila aina tokea kwao Uingereza mpaka katika makoloni yake. Wala hakuwa na lolote linalomkataza kuuza ulevi. Kwa hakika, mashirika ya ulevi yaliipatia Uingereza faida kubwa sana ya biashara ya ulevi. Hivyo basi, kwa nini Mkoloni ajinyime faida hiyo kwa kutunga sharia ya kuzuia raia zake katika makoloni wasiweze kununua ulevi ila kwa kibali? Waliowalazimisha Wakoloni Zanzibar ni idadi kubwa ya Waislamu waliokuwepo na madai yao ya kuwa na sharia hiyo, si jinginelo. Wazanzibari Waislamu walikuwa wakilinda ya dini yao na mila yao bila ya kuwanyima wengineo haki zao. Muingereza hakuwa na shida ya kuyakubali matakwa ya Wazanzibari wengi kwa sababu Zanzibar ni nchi ndogo sana na kibiashara ikuwa haiwashi wala haizimi ukiangalia idadi ya makoloni iliyokuwa nayo.

Tulikuwa na mila njema kabisa Duniani, kwa uadilifu wake, usalama, upole, mapenzi na kusaidiana kwa kila njia. Ukisikia mtu ameuliwa au amejiua, Zanzibar nzima ilikuwa ikistaajabishwa. Leo kuuwa kumekuwa kitendo kisitostaajabisha tena. Ulevi uliwekewa vikwazo na watu wakawa wanajihishimu na kuhishimiana. Mtu akipotelewa na kipochi chake ama hupelekewa nyumbani au hupelekwa polisi na akatafutwa mwenye haki yake. Leo unatafutiwa kila njia ya kuchomolewa haki yako. Kulikuwa hakuna madanguro, na kama yalikuwepo basi yalikuwepo kwa siri kabisa, leo tembelea Forodhani na katika fukwe nyingi uwaone mabarobaro na washichana, na wasichana wengine hata hawawajavunja ungo (baleghe) wanavyojiuza. Kwa ufupi sana, khasara kubwa kabisa iliyoikumba Zanzibar si ya kutawaliwa tu na wale wasiokuwa na dini za kisawasawa Tanganyika, na kuunyakuliwa uhuru wake, bali pia ya kuuwawa kwa lugha, mila, dasturi, utu na kila kilichokuwa Zanzibar kikijivunia nacho, na kutoudhibiti uhuru wa kulewa mtu apendavyo ni sehemu moja ya kuwa hatujitambui na hatutambuliwi wala hatutambulikani Duniani.

---
 
Prof. Ibrahim Noor