Afariki akisaidiwa na mjamzito mwenziye kujifungua; DC aagiza kusimamishwa watumishi waliozembea

MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda ameagiza kusimamishwa kazi na kufanyika kwa vikao vya kisheria ili kuwafukuza kazi watumishi wawili wa idara ya afya wilayani humo kwa uzembe ambao ungesababisha kifo cha mama mjamzito.

Mtanda alitoa agizo hilo jana baada ya mjamzito Catherine Gideon (33), mkazi wa kijiji cha Kasu wilayani humo, kujifungua kwa kupewa msaada na baadhi ya wagonjwa waliokuwapo hapo, ikiwa ni pamoja na kusaidiwa kukata kitovu cha mtoto na mjamzito mwenzake aliyekuwapo hospitalini hapo.

Mzazi huyo alifikwa na mkasa huo katika hospitali teule ya wilaya juzi, alisema Mtanda, baada ya kukosa huduma kutoka kwa muuguzi wa zamu, Godfrey Lazaro na muuguzi msaidizi, Maria Msafiri.

Imedaiwa kuwa wauguzi hao hawakuwapo kazini tangu saa 4:00 usiku, alisema.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Mtanda alisema amelazimika kuchukua hatua za kinidhamu baada ya watumishi hao kushindwa kutekeleza wajibu wao licha ya kwamba walikuwa zamu ya usiku.

Alisema watumishi hao walirejea kazini saa 12 asubuhi na kukuta tayari wagonjwa wamemsaidia mzazi, hali iliyozua manung’uniko kutoka kwa wagonjwa dhidi ya watumishi hao.

Mtanda alisema ameuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuwaandikia barua ya kuwasimamisha kazi kuanzia jana na kuagiza vikao vya kisheria na nidhamu vianze kuketi kuanzia leo ili kubaini makosa yao na kuwatimua kazi kwa vile wilaya yake haipo tayari kuwalea "watumishi wa aina hiyo."

Kiongozi huyo wa serikali pia aliwaonya watumishi wote wa umma pamoja na sekta binafsi kutofanya mzaha katika majukumu yao huku akiwataka wale wanaoona wamechoka kazi, waachie ngazi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mathias Abuya, alisema wanaendelea na vikao vya kisheria na watafukuzwa kazi ikiwa watathibitika kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume na sheria za taaluma ya udaktari na afya ya binadamu.