AfCHPR yapata Rais mpya baada ya jaji Augustino Ramadhani kung'atuka

Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) imepata Rais mpya, Jaji Sylivian Ore kutoka Ivory Coast, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani aliyeitumikia Mahakama hiyo kwa miaka sita.

Katika kikao cha 42 kilichofanyika Arusha, majaji wanne walistaafu utumishi wao baada ya kuitumikia mahakama hiyo kwa miaka sita kila mmoja. Majaji hao ni Fatsah Ouguergouz (Algeria), Duncan Tambala (Malawi), Elsie Thompson (Nigeria) na Ramadhani.

Kikao hicho pia kiliwaapisha majaji wawili, Ntyan Ondo Mengue kutoka Cameroon na MarieTherese Mukamulisa wa Rwanda, waliochaguliwa kwenye mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) Julai 13 hadi 15 mwaka huu, nchini Rwanda.

Mahakama hiyo inaundwa na majaji 11 ambao huchaguliwa kutoka katika kanda tano za Bara la Afrika, ambazo ni Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi na Kati na kwa sasa kuna nafasi mbili zilizobaki wazi ambazo zitajazwa Januari 2017 na majaji kutoka Kaskazini mwa Afrika.