CHADEMA yaiomba serikali iwarudishe mabati waliyotoa kwa waathirika wa mafuriko MwakataKAHAMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Kahama mkoani Shinyanga kimetoa tamko la kuiomba serikali kurejesha msaada wa mabati zaidi ya 800 yaliyotolewa na Chama hicho kwaajili ya ujenzi wa nyumba za wahanga wa mafuriko

Tamko la Chama hicho kudai msaada huo limetolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Juma Protase Ntaimpera ambaye alisema azimio la Chama hicho linatokana na tamko la Rais John Magufuli kubainisha kuwa serikali haina nia ya kujenga nyumba za wahanga hao.

Ntaimpera alisema kutokana na tamko hilo la Rais alilotoa wakati wa ziara yake Wilayani Kahama mwshoni mwa mwezi Julai mwaka huu, CHADEMA waliandika barua kwa Mkuu wa Wilaya kuitaka serikali kurejesha msaada huo

Mwenyekiti huyo alisema baada ya serikali kurejesha mabati hayo, Chama kitayagawa kwa watu wenye mahitaji ili wayatumie katika ujenzi kwa kuwa wanaishi katika mazingira magumu.

Ntahimpera aliongeza kuwa CHADEMA walitoa msaada huo kwa nia njema kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wasiojiweza hasa kwa kuzingatia ugumu wa maisha wanaokutana nao baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kuezua nyumba zao. Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwakata kata ya Mwenda walibaki bila makazi na wengine kupoteza maisha.