Gereza lilivyoharibiwa na tetemeko la ardhi Kagera; Waziri aagiza wafungwa wahamishweSerikali imeagiza wafungwa 280 katika gereza la Kitengule wilayani Karagwe, wahamishwe katika kipindi cha wiki moja kupelekwa gereza la Mwisa.

Watahamishwa baada ya mabweni yao kuharibiwa kwa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, 2016.

Agizo hilo lilitolewa jana, Septemba 18, 2016 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, Jeremiah Nkonda.

Mwigulu aliagiza hilo baada ya kufanya ziara mkoani hapa na kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuona uharibifu uliojitokeza kutokana na tetemeko hilo, lililoripotiwa kusababisha vifo vya watu 17, majeruhi, nyumba kubomoka na uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu ya barabara.
“Nimetembelea magereza yetu, lakini gereza la Kitengule limeharibika sana, kuta zimeanguka, mabweni yameharibika kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hawapaswi kuishi watu. Kwa hiyo, naagiza mkuu wa magereza hapa kuwahamishia wafungwa hawa katika gereza la Mwisa lenye mabweni manne yaliyo wazi,” aliagiza Mwigulu.
Alisema katika kipindi cha wiki moja, kazi hiyo iwe imekamilika kwa sababu wakiendelea kuwaacha wafungwa hao katika gereza hilo lililoharibika ni hatari, kwani wanaweza kudondokewa na kuta zinazoning’inia na kusababisha maafa mengine.

Mwigulu alisema kutokana na tukio hilo, Wizara inaandaa mpango wa muda mrefu wa kujenga bweni kubwa, litakalokuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 400 kwa wakati mmoja kwa kuwa hilo ni gereza la kikazi linalobeba watu wengi.

Kwa upande wake, Nkonda alisema kilichochangia zaidi kushuka kwa kuta hizo ni kwamba matofali yaliyojenga kuta hizo yanaonekana yalikuwa mabichi.

Alisema kwa hali hiyo haitawezekana kufanya ukarabati, bali ni kuhakikisha wanabomoa mabweni hayo na kujenga upya.

Alisema gereza hilo, lilikuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 380 kati ya hao 100 wako kwenye kambi ndogo na 280 ndio watakaohamishiwa kupelekwa katika gereza la Mwisa.