Hivi ndivyo wengine "wanavyoisoma numero"

KILE kibano cha kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma alichoahidi Rais John Magufuli kimeendelea kuwakumba maofisa wengi wa juu katika idara na taasisi mbalimbali za Serikali huku athari zake zikizidi kuonekana kila uchao. 

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa siku kadhaa umethibitisha pasi na shaka kuwa hatua hizo za kubana matumizi yasiyo ya lazima ikiwamo pia kupunguza mishahara ‘kufuru’ waliyokuwa wakilipwa baadhi ya viongozi wa idara, mashirika na taasisi mbalimbali za umma zimeanza kuwaletea changamoto nyingi za kimaisha baadhi yao kulinganisha na neema tele walizokuwa nazo kabla ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano.

Hivi karibuni, Rais Magufuli anayesisitiza kila uchao kuwa ni lazima serikali yake ibane matumizi yasiyo ya lazima ili fedha zinazopatikana zielekezwe katika kuwanufaisha wananchi wa kawaida kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, aliahidi kushusha mishahara inayofikia hadi Sh. milioni 40 kwa badhi ya vigogo serikalini ili mwishowe kiwango cha juu kiwe Sh. milioni 15, sawa na punguzo la asilimia 62.5.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa wale waliokuwa wakivuna fedha nyingi kiasi cha kuishi kama ‘malaika’ wateremke ili kuondoa tofauti kubwa iliyokuwapo katika malipo ya mishahara baina yao na watumishi wengine wa kada mbalimbali. Alikwenda mbali pia kwa kuutaja hadharani mshahara wake wa kila mwezi kuwa ni Sh. milioni tisa.

Aidha, katika kutekeleza maelekezo hayo ya Rais Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki, alitoa waraka rasmi wa Serikali unaoelekeza viwango vya juu vya mishahara kwa wakuu wa taasisi mbalimbali za umma kuwa ni Sh. milioni 15.

WANAVYOLIZWA

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa mbali na kupunguzwa mishahara kwa baadhi ya vigogo, wengi wao hutaabika hivi sasa na kujikuta wakibadili mwenendo wa maisha yao kutokana na hatua nyingine mbalimbali za kubana matumizi zilizochukuliwa na Serikali katika kipindi cha miezi 10 tangu kuapishwa kwa Rais Magufuli Novemba 5, 2015.

Uchunguzi huo umebaini kuwa hivi sasa, wengi kati ya maofisa wa juu na wa kati wanaoshikilia nafasi mbalimbali kwenye taasisi za umma wanateseka kutokana na kukatwa kwa mirija ya fedha zilizokuwa zikimiminika kwao kila uchao, baadhi zikiwa ni safari mfululizo za ndani na nje ya nchi ambazo kwa pamoja, ziliwahakikishia kuvuna malipo manono kupitia posho za nauli na zile za kujikimu.

Akizungumza wakati akizindua Bunge la 11 Novemba 20, 2015, Magufuli alisema kupitia safari za nje ya nchi, serikali ililipa Sh. bilioni 356.3 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015, ambazo kati yake Sh. bilioni 183.1 ziligharimia tiketi za ndege, Sh. bilioni 68.6 mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zililipwa kama posho kwa maofisa waliohusika na safari hizo.

Eneo jingine ambalo vigogo wamepata pigo hivi sasa baada ya mirija kuzibwa ni kufutwa kwa maadhimisho mbalimbali kama yale ya “Wiki ya Utumishi wa Umma” yaliyokuwa yakifanyika kuanzia Juni 16 hadi 23 ya kila mwaka na pia “Wiki ya Maji” na “Siku ya Ukimwi Duniani”.

Kupitia maadhimisho hayo, vigogo mbalimbali waliokuwa wakiratibu walikuwa wakipata mwanya kujiingizia fedha kirahisi kwa kupitisha zabuni mbalimbali kama za kutengeneza vipeperushi, kukodi mahema, kukodi viti, wazabuni wa kuwaletea vyakula na wakati mwingine kutengeneza kumbukumbu za picha za mnato na video.

Katika “Wiki ya Utumishi wa Umma” mwaka huu, Waziri Kairuki alisitisha ulaji baada ya kuagiza kuwa maadhimisho hayo yafanyike ofisini huku kila Idara ama Wizara husika ikiutakiwa kutenga siku moja ya kusikiliza kero za wafanyakazi wao na siku moja ya kusikiliza kero za wananchi badala ya kwenda kwenye viwanja vya wazi kama vya Mnazi Mmoja.

Chanzo kimoja kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kilisema kuwa ulaji maarufu utokanao na posho za semina na makongamano ni kama umefutika kabisa hivi sasa na hivyo wanufaika wengi wamebaki wakilia njaa na wengine kubadili aina za maisha yao.
“Kwa kweli tutaikumbuka awamu ya nne maana kama fedha zililiwa hasa, fursa zilikuwa nyingi sana maana hata vikao vya kawaida vya kikazi katika ofisi na idara mbalimbali wakubwa walikuwa wakilipana poshi nono bila kujali. Hali hiyo sasa haipo. Hakuna mwenye uwezo wa kuandika dokezo la posho maana kesho yake atatumbuliwa mara moja,” kilisema chanzo hicho.
Alitoa mfano kuwa semina nyingi za mafunzo na hata mikutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya ofisi yao ilikuwa ikifanyika kwenye kumbi za hoteli mbalimbali na wengi walikuwa wakipata upenyo wa kuvuna fedha kirahisi; lakini hivi sasa hivi ulaji huo haupo kwa sababui mikutano yote hufanyika ofisini tena bila posho.

Pia kuna waraka unaoelekeza kuwa vikao vyote vya kikazi visivyohusisha wajumbe wanaozidi mikoa minane vifanyike kwa njia ya video na siyo kusafiri.

Katika kudhihirisha kwamba serikali haitanii kuhusu kukata matumizi, Mwezi Juni mwaka huu, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alizungumza na Bodi mpya ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kupitia Teknolojia ya Video (Video Conference) akiwa mjini Dodoma na bodi ikiwa Makao Makuu ya TPA, jijini Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa kabla ya ujio wa awamu ya tano, wajumbe wa bodi hiyo wangewasha magari kwenda Dodoma kumfuata Waziri na kulipwa posho nono.

MSAJILI WA HAZINA

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, ambaye huhusika pia katika kuidhinisha maombi ya watumishi wa Serikali kwa safari za nje ya nchi aliiambia Nipashe kuwa sasa hakuna namna isipokuwa ni kutekeleza agizo la kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima na hivyo kila anyetaka kusafiri ni lazima ajieleze vya kutosha kabla ya kupata kibali cha kufanya hivyo.
“Unajua fedha za serikali ni zile zilizotengwa kwenye bajeti. Sasa kama una safari yako na haiko kwenye bajeti ya serikali, hela ya kukusafirisha na kukulipa posho inatoka wapi?” 
Alihoji Mafuru na kuongeza:
“Sisi hatuwezi kuruhusu mtu asafiri kiholela. Hivyo lazima tujiridhishe kama mkutano anaotaka kwenda mhusika fungu lake limo kwenye bajeti iliyopitishwa na serikali na kama sivyo tunamkatalia,” alisema Mafuru

UKATA UNAVYOTESA

Ukata huo utokanao na uamuzi wa serikali kubana matumizi umesababisha mabadiliko makubwa kwa baadhi ya vigogo waliokuwa wakitamba mitaani kutokana na ukwasi mkubwa waliokuwa nao.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa badhi ya athari hizo ni pamoja na kupungua kwa idadi ya vigogo kwenye maeneo ya starehe; baadhi kupungua miili kiasi cha kupoteza maumbile ya vitambi vyao; wengine kulazimika kuwahamisha watoto zao kutoka kwenye shule ghali walizokuwa wakisoma na kuwajumuisha kwenye shule nyingine za gharama nafuu na pia wapo ambao sasa wametulia kwenye ndoa zao baada ya kushindwa kugharimia matunzo ya utitiri wa ‘nyumba ndogo’

Uchunguzi wa Nipashe umebaini vilevile kuwa athari nyingine zitokanazo na maisha mapya ya badhi ya vigogo yatokanayo na ukata uliokithiri ni pamoja na kupunguza matumizi yao katika kulipa mishahara ya watumishi wa ndani kwa maarufu kama ‘hausigeli’ na ‘hausiboi’; kupungua kwa idadi ya magari binafsi ya kifahari yaliyokuwa yakiwagharimu fedha nyingi kuyaendesha kwa kuyanunulia mafuta na viupuri na pia baadhi yao wameanza kugeukia usafiri wa rahisi wa bodaboda kwa safari fupifupi – jambo ambalo kamwe hawakutarajiwa kuliufanya hapo kabla.
“Kuna watu walikuwa wanatumia fedha bwana. Wengine tulikuwa tunawaita wazee wa bandari...hawa walikuwa hawana cha wikiendi wala nini, wao ni matanuzi tu na walikuwa wana vijumba vidogo kila kona ya mji. Lakini sasa wengi wanataabika kwa sababu mambo hayo yanahitaji fedha ambazo zimekuwa zikiwakimbia kwa kasi,” 
chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kuongeza:
“Baadhi wamechoka hadi vitambi vikubwa walivyokuwa navyo vimeanza kupukutika… hawaumwi lakini walau na wao wanaisoma namba kwakweli,” mwingine aliongeza.
Alisema baadhi ya watu hao waliokuwa wakitumia fedha kwa fujo hivi sasa wanaishi kwa kubangaiza kwa sababu wengi ni wale waliokuwa wakitegemea dili za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari TPA ambako mizigo mingi ilikuwa ikipitishwa bila kulipiwa ushuru.
“Unajua hata vyuo vimeathirika sana maana wale vigogo waliokuwa wanawasomesha baadhi ya kina dada hawana hela...baadhi ya warembo wamelazimika kuhama nyumba walizokuwa wakilipiwa na vigogo baada ya kutelekezwa,” chanzo kingine kiliongeza.
Nipashe ilifanya uchunguzi kwenye baadhi ya kumbi za starehe (pub) zilizofunguliwa kwa wingi enzi za utawala wa awamu ya nne na kubaini kuwa hivi sasa baadhi zikiwa zimefungwa na nyingine nyingi hazijai kam zamani.

Mmoja wa wafanyakazi wa pub moja iliyoko Ubungo Riverside alikiri kuwa hivi sasa biashara imekuwa mbaya na wateja ni wa kugombania.

Hali hiyo ya ukata inadhihirishwa pia na hatua ya baadhi ya hoteli kuanza kuuzwa au kubadilishwa matumizi, ikiwamo hoteli marufu ya Land Mark ya Ubungo jijini Dar es Salaam iliyogeuzwa kuwa hosteli ya wanafunzi.

Mmiliki wa Hoteli hiyo, Saul Amom, alisema hivi karibuni kuwa kudorora kwa biashara ndiko kumewalazimu kufanya mabadiliko hayo katika uendeshaji wa biashara.
“Kwa kweli hali ni mbaya na ndiyo maana tumeamua kufanya haya mabadiliko. Hakuna namna,” mmiliki huyo alikaririwa akisema.
Aidha, hoteli mbili za kitalii mkoani Arusha zilitangazwa pia kuuzwa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji huku nyingine ikielezwa kushindwa kulipa mishahara wafanyakazi wake. --- NIPASHE