Hospitali ya Somanda yapandishwa hadhi na kuwa hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa

Hatimaye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi (Somanda) imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali Teule ya Mkoa, baada ya makabidhiano yaliyofanyika jana baina ya uongozi wa Halmashauri hiyo na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu.

Toka mwaka 2013, madiwani katika halmashauri hiyo wamekuwa wakilalamika juu ya mzigo mkubwa unaoikabili hospitali hiyo, kutokana na kuhudumia jumla ya halmashauri tatu, Halmashauri ya mji Baraidi, halmashauri ya wilaya Bariadi, pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Itilima.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika ukumbi uliko hospitalini hapo, ambapo Katibu Tawala wa Mkoa Jumanne Sagini pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri Melkizedeck Humbe walikabidhiana nyaraka zenye makubaliano katika uendeshaji wa haopstali hiyo.

Aidha, hafla hiyo ilihudhuliwa na watumishi mbalimbali wa hosptali hiyo ikiwa pamoja na maofisa kutoka Ofisi ya Katibu Tawala, huku Mwenyekiti wa Hlmashauri hiyo, Robert Rweyo aliyehudhuria makabidhiano hayo pia akishukuru hatua hiyo.

Rweyo alisema kuwa amekuwa akipata wakati mgumu katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiikabili hospitali hiyo, huku akieleza kuwa tatizo kubwa lilikuwa ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba.
"Nashukuru kwa hatua hii kufikiwa, toka mwaka 2013 tunalilia suala hili mimi pamoja na Madiwani wangu, tulikuwa tukieleza hospitali inalemewa, kiasi kinachopokelewa ni kidogo sana hakilingani na idadi ya watu inaowahudumia, kwa hatua hii huduma zitaboreshwa kwa kiwango kikubwa sana," alisema Rweyo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika makubaliano ya Mkoa kuendesha hospitali hiyo, watumishi wamegawanywa katika mamlaka ya kuajiriwa, huku usimamizi ukibaki sehemu moja ambayo ni Katibu Tawala wa Mkoa.
"Baadhi ya wafanyakazi mamlaka zao za kinidhamu pamoja na mambo mengine ya huduma kwao yako kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, lakini wengine wamepelekwa kwa Katibu Tawala Mkoa kama msimamizi mpya na mwendeshaji wa hosptali hii, lakini watumishi wote watasimamiwa na Katibu Tawala," alisema Humbe
Aliwataka watumishi wote kubadilika katika utendaji kazi wao kutokana na hospitali hiyo kupandishwa hadhi, na kuwa hosptali teule ya rufaa ya Mkoa, kwa kuwataka kubadilika kitabia ili ziweze kuendana na hadhi ya hospitali.

Mbali na hilo, Humbe alisema mambo mengi yatabadlika katika utoaji wa huduma katika hospitali hiyo, lengo likiwa kuboresha kuwa katika kiwango kikubwa kinachoendana na sera na taratibu za hospitali za rufaa hapa nchini.

Naye katibu Tawala Mkoa alisema kuwa hatarijii kusikia au kuona uwepo wa watumishi wazembe na wenye lugha chafu kwa wagonjwa na wanachi kwa ujumla, ambapo alisema hatasita kuchukua hatua kali kwa mtumishi atakayebainika kwenda kinyume cha maadili ya kazi yake.
"Kuanzia sasa hivi hii ni hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, tunategemea kwa kiwango kikubwa huduma hapa zitabadilika sana na kuwa katika kiwango cha hali ya juu, kwa hali hiyo hata watumishi watabadilika na kuwa katika kiwango hicho cha hospitali.
Hata hivyo, Katibu Tawala huyo ametangaza rasmi kuwa amemteua Dk Frederick Mlekwa kuwa Mganga Mfawidhi wa hosptali hiyo, ambapo Dk Mlekwa ameeleza kuwa atahakikisha anatumia taaluma na uzoefu alionao katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wagonjwa katika hospitali hiyo.