Itafika siku Watanzania wagongewe milango kwa kudaiwa deni la taifa?

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa inaendelea na mikakati ya makusudi katika kudhibiti ongezeko la deni la taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Saed Kubenea Mbunge wa Ubungo lililouulizwa kwa niaba yake na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai Freeman Mbowe lililohusu deni la taifa.

Naibu Waziri huyo aliitaja mikakati inayosaidia kupunguza deni la taifa ambayo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara ya miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa pato la taifa.

Mikakati mingine ni kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa wakandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mikataba inayoweza kusababisha mzigo wa madeni kwa Serikali.

Naibu Waziri Dkt. Ashatu alisema hadi kufikia Juni 2016 deni la taifa lilikuwa dola za kimarekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na dola bilioni 19.69 kwa mwezi Juni 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.

Dkt. Ashatu alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni dola za Kimarekani bilioni 20.5 na deni la sekta binafsi ni dola za Kimarekani bilioni 2.7 na kuongeza kuwa deni la Serikali linatokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.

Baadhi ya miradi ya maendeleo iliyoainishwa ambayo imetumia fedha za maendeleo ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja, mradi ya kimakakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kv 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga na mabasi yaendayo haraka.

Miradi mingine ni ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafisha gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es salaam na mradi wa maji wa Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Aidha, Dkt. Ashatu amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali ilipokea mikopo yenye masharti nafuu na ya biashara kiasi cha sh trilioni 1.3 na mwaka 2014/2015 Serikali ilipokea mikopo ya kiasi cha Sh. trilioni 2.3 mikopo ambayo haikufikia trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni 9 kabla ya mwaka 2015.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi alipokuwa akichangia hoja hiyo amewatoa hofu Watanzania na kusema kuwa haitatokea hata siku moja wagongewe milango kwa kudaiwa deni la taifa na kuongeza kuwa deni la taifa linapimwa kutokana na ukusanyaji wa mapato hatua ambayo Serikali inaendelea kuitekeleza kwa vitendo.

Waziri Mwigulu aliongeza kuwa Serikali haikopi kwa ajili ya miradi ya kawaida isipokuwa inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa lengo la kuwahudumia wananchi.
  • Imeandikwa na Eleuteri Mangi - Dodoma