Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Kamanda wa mkoa wa Njombe wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkaguzi Joseph Mwasabeja akitoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Njombe.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeundwa na kufanya kazi chini ya sheria namba 14 ya mwaka 2007 “FIRE AND RESCUE FORCE ACT”. Majukumu makubwa ya Jeshi ni kuzima moto na kuokoa maisha na mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani pamoja na majanga mengineyo.

HUDUMA YA ZIMAMOTO NA UOKOAJI INATOLEWA

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeundwa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Hivyo basi mtu yeyote anastahili kupata huduma hiyo kwa kupiga namba ya simu 114. Pia kuna huduma nyingine zitolewazo na Idara.

HUDUMA ZITOLEWAZO NA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linajukumu kubwa la kutoa huduma kwa jamii katika Nyanja mbalimbali zikiwemo Kuokoa maisha ya watu na mali zao, Kuzima moto, Kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga moto, Kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto, Kusoma ramani za majengo na kutoa ushauri, Kutoa huduma ya kwanza katika majanga na ajali barabarani, Kutoa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto, Kufanya uchunguzi kwenye majanga ya moto na Kutoa huduma za kibinadamu.

KUFIKA KWENYE TUKIO BILA YA VITENDEA KAZI (MAJI)
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakati wote huwa limejiandaa kwa magari yake kuwa na vitendea kazi vya kuzimia moto na kufanyia maokozi pia magari huwa yamejazwa maji wakati wote yanapokuwa vituoni yakisubiri matukio. Changamoto iliyopo ni wananchi wengi kuwa na dhana kuwa magari ya Zimamoto huenda kwenye matukio bila maji.

AINA YA GARI LA ZIMAMOTO, VIFAA, UWEZO WA KUBEBA MAJI (UJAZO), NA JINSI YA UFANYAJI KAZI 
 
Gari la Zimamoto linapofika kwenye tukio hufanya kazi kama mtambo wa kuzimamoto, magari hayo yanamatanki ya maji yenye ujazo kuanzia lita 1,500 hadi lita 7,000 (kuna moja linabeba lita 16,000) ili maji hayo yatoke kwa nguvu na kuweza kuzimamoto, magari ya Zimamoto yamefungwa pampu zenye uwezo wakusukuma lita 2,000 hadi lita 6,000 kwa dakika.

Kwa kawaida tunapofika kwenye tukio hutumia mipira yenye kipenyo cha milimeta 70 na kufunga kifaa cha kumwagia maji (branch pipe) chenye kipenyo cha milimeta 20 na pampu husukuma maji kwa nguvu ya bar 7, kwa vipimo hivyo huwa tunamwaga lita 1,000 kwa dakika kwa njia moja ya kutolea maji hivyo kwa gari lililobeba lita 7,000 maji yatakwisha ndani ya dakika saba, kwa kawaida tunatumia njia mbili za kutolea maji hivyo huwa tunamwaga lita 2,000 kwa dakika, na gari lililobeba lita 7,000 maji yatakwisha baada ya dakika 3½ nasisi hulazimika kuondoka eneo la tukio kwenda kutafuta maji.

Huku nyuma wanaweza kuja waandishi wa habari na kuwauliza wananchi mbona moto unawakana Zimamoto hawapo? Wananchi hujibu kuwa wamekuja lakini baada ya muda mfupi wameondoka na kusema kuwa wanakwenda kuchukua maji, hapo ndipo dhana ya Zimamoto wamekuja kuangalia kwanza ukubwa wa moto na sasa ndio wamekwenda kuchukua maji hujengeka. Ki uhalisia si kweli kuwa magari ya Zimamoto hufika kwenye tukio bila ya maji.

Maji yanayobebwa na magari ya Zimamoto husaidia kuanzia kazi, kabla maji ya kwenye gari kwisha gari la Zimamoto hutegemea kupata maji kutoka kwenye vituo maalum vya maji kwa ajili ya Zimamoto (Fire Hydrants) ambazo katika miji yetu mingi huwa hazifanyi kazi kutokana na sababu zifuatazo:-
  1. Kutokuwa na maji
  2. Kufukiwa na vifusi au mchanga au kufunikwa kutokana na ukarabati wa mitaa au barabara.
  3. Kung’olewa na kubadilishwa matumizi.
  4. Kung’olewa kwa alama za utambulisho (H sign)
  5. Kuibiwa kwa mifuniko kutokana na biashara ya chuma cha kavu.
  6. Miradi mingi ya maji katika miji kutoshirikisha ufungwaji wa vituo vya maji (Fire Hydrants).

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa Jeshi hilo wakikagua moja ya kisima (Fire Hydrant) kinachoweza kutoa msaada wa maji katika matukio pindi magari ya zimamoto yanapoishiwa maji.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa Jeshi hilo wakikagua moja ya kisima (Fire Hydrant) kinachoweza kutoa msaada wa maji katika matukio pindi magari ya zimamoto yanapoishiwa maji.

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakionyesha jinsi ya uzimaji moto na kiasi cha maji yanayotumika (Pressure) wakati wa matukio.
  • PICHA ZOTE NA FC GODFREY PETER