Kauli ya Wizara ya Afya kuhusu nchi 'kukaukiwa' dawaTatizo la dawa nchini ni kubwa kuliko watu wanavyodhani. Na ni bahati mbaya sana Watanzania wengi wanasahau haraka juu ya namna Serikali ya CCM isivyojali kabisa juu ya Afya na Maisha yao.

Kuna wananchi wenzangu wengi wananilaumu kwamba kwa kuwajulisha kuwa Hospitalini hakuna Madawa huku Serikali ikinyamazia Ufisadi wa Mabilioni 850 wa "Akaunti ya Tegeta Escrow" (Zaidi ya mara 3 ya Bajeti ya Madawa yote Nchi nzima kwa Mwaka), nakuwa sitoi njia Mbadala. Jambo ambalo si kweli. Tuna Serikali isiyo sikivu na isiyowapenda Wananchi wake, na sisi Wananchi tunasahau haraka.

Wakati wa Bunge la Bajeti nilisema yafuatayo juu ya Bohari ya Madawa – MSD na suala la Madawa:

"Mheshimiwa Spika, chukulia mfano wa Madawa (essential medicines) ambapo Serikali imepanga kutumia Shilingi za Kitanzania 251 bilioni mwaka 2016/17 kwa Bohari ya Madawa (MSD) lakini katika fedha hizo Shilingi 131 bilioni ni za kulipa madeni ya miaka ya nyuma. Kimsingi Bajeti ya madawa ya mwaka huu ni Shilingi 120 bilioni tu".

Katika Hotuba husika nilishauri masuala yafuatayo:

– DENI: Deni la MSD (yaani Bilioni 131) lipelekwe Wizara ya Fedha Ili Fedha za Bajeti ya Madawa ziwe Nyingi. Hivyo badala ya Bajeti halisi kuwa Bilioni 120 ibaki kuwa bilioni 251.

– Azimio La Abuja: Serikali kuhakikisha Suala la Afya na Madawa kwa Watanzania Wanyonge linakuwa Kipaumble kikuu kwa kuhakikisha Bajeti ya Sekta Nzima ya Afya inafikia Hata nusu ya 15% ya Bajeti yote Kama linavyotaka "Azimio la Abuja". Kwa sasa Bajeti ya Sekta ya Afya ni 3% ya Bajeti Nzima ya Taifa.

– Ajira Afya: Kuna tatizo kubwa sana la uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya. Zahanati nchini zina uhaba wa Wataalam wa maabara Kwa 93%, wauguzi wa ngazi ya cheti Kwa 65% na maafisa tabibu Kwa 52%. Vituo vya Afya vina uhaba wa wauguzi wa ngazi ya cheti Kwa 65% na Hospitali za Wilaya zina uhaba wa wauguzi Kwa 77% na uhaba wa madaktari Kwa 74%.

– Wizara ya Afya ilikuwa na kibali cha kuajiri watumishi wa Afya na mpaka Mwezi Mei 2016 hakuna aliyeajiriwa na vibali vya ajira vilimalizika muda wake mwisho wa Mwezi Juni 2016. Na sote tunajua sasa Ajira bado zimesitishwa.

– Bima Ya Afya Kwa Wote: Hapa nilieleza Juu ya Miradi ya Majaribio ya Ruangwa na Ujiji (Oktoba 1, 2016 Halmashauri ya Kigoma Ujiji itaanza Skimu husika) na Pia Mpango wa "Universal Health Coverage" wa Serikali.

– Mapendekezo yangu yalikuwa ni Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii Nchini iwe inapeleka michango ya Wanachama wao NHIF ili kuwe na Mfuko mmoja tu wa kitaifa (wa Bima ya Afya). Kwa hiyo, kutokana na mahesabu ya kiakchurio (actuarial), % ya michango inayopaswa kuwa ya Afya kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe 'remitted' (itengwe kwenda) NHIF na hivyo kila Mtanzania ambaye anakuwa ni Mwanachama wa Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii anakuwa ,moja kwa moja ni mwanachama wa NHIF.

– Mpaka Sasa Mfumo wetu wa Bima ya Afya haujaratibiwa vizuri na matokeo yake kuna watu kimsingi wanalipia bima za Afya mara 2 kutokana na kukosekana kwa uratibu. Hivi sasa kwa mfano kuna skimu za bima ya Afya za kitaifa kama NHIF na CHF na vile vile fao la Afya kutoka NSSF. Siku za karibuni PSPF na PPF wameanzisha Fao la Afya pia kwa wachangiaji wao wa hiari. Hata hivyo, Shirika la ILO ambalo Tanzania ni mwanachama limeainisha mafao 9 kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na moja ya hilo ni Fao la Bima ya Afya. Kwa hiyo katika kila mchango wa Mfanyakazi kwa mfano, kuna asilimia ya mchango inakwenda kwenye huduma ya Afya. Hata hivyo, ukiachana na NSSF mifuko mingine haifanyi hivyo na matokeo yake Wafanyakazi, hasa Wafanyakazi wa Serikali wanajikuta wanakatwa 20% kwenda kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na pia wanakatwa 6% kwenda Mfuko wa Bima ya Afya. Hii si Sawa, Ni kuwaumiza Hawa Wafanyakazi Wanyonge

Serikali si Sikivu

Serikali haikuwa sikivu (Kama ambavyo si sikivu sasa Juu ya Ufisadi wa Escrow). Lakini pia kwa dhahiri imeonyesha kuwa Madawa kwa Watanzania wanyonge si kipaumbele chake kikuu. Ingetekeleza hayo Watanzania wanyonge msingekosa madawa Hospitalini.

Zitto Kabwe