Kishindo cha mwitikio wa wakazi wa Dar kwenye wito wa kupima afya bure

UPDATE: Septemba 26, 2016

WANANCHI waliojitokeza katika zoezi la kupima afya zao lililoanza Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wamelalamikia mpango mbovu wa huduma hiyo, anaandika Aisha Amran.

Wamesema, huduma hiyo imekuwa ya kuchelewa na kwamba, wamechukua namba mapema lakini mpaka jana hawakuwa wamehudumiwa.

Zoezi hilo lililotarajiwa kumalizika jana, limeongezwa siku mbili na sasa litamalizika kesho kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza.

Upimaji afya huo ulidhaminiwa na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuwa na tabia ya kwenda kupima afya zao mara kwa mara.

Akizungumza na mwanahalisionline, Salumu Moshi, mwananchi aliyekwenda kupata huduma hiyo Mnazimmoja amelalamika kuwa, huduma hazikidhi mahitaji kwasababu watoa huduma ni wachache ukilinganisha na watu waliojitokeza.

“Huduma za hospitali ni gharama sana kwani mpaka umuone dakitari lazima utoa kwanza kiasi cha shilingi 30,000 ambapo kwa hali ya Mtanzania wa chini hawezi kumudu na ndio maana kukitokea huduma kama hizi ambazo hutolewa bure, watu tunakauwa wengi sana,” amesema Moshi.

Moses Michael amesema, endapo hospitali wangepunguza gharama za kupima afya ya mwili, watu wengi wasingejitokeza mpaka watoa huduma kuelemewa.

“Baadhi ya watu walioendelea kujitokeza walirudishwa nyumbani kwa kukosa huduma ya namba ambazo mwazo zilitolewa kwa zaidi ya watu 11,200,” amesema.

Joseph Masanzo, Famasia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema, lengo la huduma hiyo ni kuwahamasisha wananchi kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara.

Amesema, hawakutegemea kama watajitokeza kwa wingi kiasi hicho na kwamba, kutokana na ongezeko la idadi ya watu kinyume na matarajia yao, wameongeza siku mbili zaidi (Jumatatu na Jumanne).

“Mategemeo yetu ni kutoa huduma kwa jumla ya watu 3000 na tuwahudumie kwa siku mbili lakini imekuwa kinyume kwani wamejitokeza zaidi ya idadi tuliyotegemea, mpaka tukaamua kuongeza siku ili kila mtu apate huduma.”

Amesema, awali wananchi hawakuwa na uelewa mzuri hivyo walitoa huduma taratibu.

“Tunashukuru wananchi kujitokeza kwa wingi lakini mpaka leo tumeshahudumia zaidi ya watu 6000 ukilinganisha na idadi tuliyoandikisha na huduma ambazo tunazitoa hapa ni kupima presha, figo, kisukari, virusi vya Ukimwi, tezi dume na mwagonjwa mengine,” amesema Masanzo.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kushoto) akizungumza na wananchi walio fika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kupata vipimo na kupatiwa ushauri na Madaktari kutoka Hospitali Mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

Wananchi wakiwa na watoto wao katika viwanja vya Mnazi Mmoja

Wananchi wakiwa katika mistari ambao hawajapata namba

Mkuu wa Idara ya magonjwa ya Dharura na Ajali Hospitali ya Taifa Muhimbili Dk. Juma Mfinanga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa zoezi la kupima vipimo kwa wananchi bure lililoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kwa kushirikiana na madaktari kutoka hospitali mbalimbali za Dar es Salaam ikiwemo, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aga Khan Hospital, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ikiongonzwa na Rais wa Chama cha Madaktari Figo Tanzania na pia ni Daktari Bingwa wa Figo Dk. Onesmo Kisanga

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace (kushoto) Magembe akiwaonyesha jambo wananchi waliojitokeza kupata huduma ya vipimo kutoka kwa madaktari wa hospitali mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili mkoa wa Dar es Salaam, zoezi lililoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, lililofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini humo.

Kutokana na mwitikio wa wananchi, huenda siku zitaongezwa baada ya Mkuu huyo kujadiliana na madaktari hao.

Septemba 25 ilikuwa ndiyo siku ya kuhitimisha zoezi hilo.


Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja

Zuhura Shaba (54) akiwa amebebwa na baadhi ya Madaktari na wafanyakazi wa Afya baada ya kujikuta amepoteza fahamu mara baada ya kufika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

Baada ya muda na mpiga picha hizi alibahatika kuongea naye na kuanza kusema kwa utaratibu kinachomsumbua na kueleza mengi. Alisema yeye ni Mtoto wa 7 na baba yake enzi za uhai wake miaka ya nyuma alishika nyadhifa mbalimbali serikalini kama, Waziri wa Afya, Meneja Mkonge Tanga, Mbunge.

Alisema anamshukuru Mkuu wa Mkoa na "Mungu amuongoze kwa kila anachokifanya kwa Jamii ya Kitanzania," na kumshukuru Rais wa Tanzania, "kwa kumpa maono ya kumchagua kijana huyu, Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa," na kuishukuru timu nzima ya Madaktari kwa moyo wao kuona jamii ya Kitanzania bado ina hali duni na, "kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kutuletea zoezi hili, nashukuru baada ya kujikuta napoteza fahamu nimejikuta nipo katika chumba huduma ya haraka na kupata huduma na sasa najiona ninanafuu."


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi Sophia Mjema (kushoto) akishiriki zoezi la kugawa namba kwa wananchi walioitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Baadhi ya wananchi wakiwa wamenyoosha mikono wakitarajia kupata namba kwa ajili ya kupatiwa huduma ya vipimo


Askari Polisi akizungumza na baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Mnazi Mmoja
Joyce Mgeta akipatiwa vipimo na Dk. Daniel Chacha (kushoto) mara baada kujikuta anaishiwa nguvu ghafla akiwa katika foleni ya kusubiri kupata namba. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Juma Mfinanga


Picha zote na maelezo: KHAMISI MUSSA