Kivutio cha utalii mkoani Ruvuma: Jiwe la Mbuji


JIWE la Mbuji lililopo wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, ni miongoni mwa vivutio adimu na vya kipekee vilivyopo katika Bonde la Ziwa Nyasa ambalo linajumuisha mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Njombe.

Tayari Wizara ya Maliasili na Utalii imeliingiza Jiwe la Mbuji kwenye orodha ya vivutio vya utalii vilivyoko mkoani Ruvuma ili hatimaye kazi ya kutangaza eneo hilo na vivutio vingine, iweze kufanyika kwa tija.

Neno Mbuji lina maana ya Kitu Kikubwa. Hivyo pengine, jiwe hilo kuitwa Mbuji, ilitokana na ukubwa wake usiokuwa wa kawaida. Jiwe hili lipo katika Kijiji cha Mbuji, Kata ya Mbuji. Kwa sasa limekuwa kivutio kwa wageni wa ndani na nje wanafika kutembelea wilaya ya Mbiga kwa shughuli zao mbalimbali, zikiwemo za kitalii.

Moja ya maajabu ya jiwe hili, ni ukubwa wake likilinganishwa na mawe yote yanayopatikana katika mkoa wa Ruvuma. Chini ya jiwe hili kuna vyanzo vingi vya maji. Ni vigumu kwa mtu yeyote kulipanda bila kwanza kuwaona wazee wa kimila wa eneo hili. Yeyote anayethubutu kulipanda bila kuwaona wazee hao, yanayomkuta anajua mwenyewe, lakini ukweli ni kwamba ni tayari juu yake. Ni vigumu kulizunguka jiwe hilo bila kufuata mila na desturi za Kabila la Wamatengo wanaoishi eneo hilo.

Kwa jamii ya Wamatengo, jiwe hili linaheshimika sana. Sehemu kubwa ya wananchi wanaoishi kuzunguka eneo lilipo jiwe hili hawajawahi kulipanda wala kulisogelea katika maisha yao yote kwa hofu ya kupoteza maisha.

Sixmund Ndunguru (90), ni mmoja wa wazee wa kimila wa Kabila la Wamatengo. Katika mazungumzo yake na FikraPevu anasema pamoja na mambo mengine kwamba ili kuweza kupanda jiwe hili, ni lazima mtu awe na mzee wa kimila wa kumwongoza, anayezifahamu vizuri mila na tamaduni za kabila hilo.

“Ninayafahamu maajabu ya jiwe la Mbuji tangu nikiwa na umri mdogo. Mandhari ya jiwe hili hayajabadilika wala kuharibiwa tangu nilipoanza kulifahamu,” Mzee Ndunguru anaanza masimulizi yake juu ya jiwe hili.

Anaendelea: “Mimea hii aina ya matete inayozunguka jiwe hili imekuwepo miaka mingi sana. Kwa mara ya kwanza, mimi mwenyewe nilipanda juu ya jiwe hili miaka ya 1940 nikiwa na baba yangu mzazi…kwa hiyo, mtu yeyote anaruhusiwa kupanda jiwe hili ilimradi azingatie maelekezo ya wazee wa kimila.”

Kwa kawaida, Wamatengo wanaamini kwamba katika jiwe hili lina viumbe vinavyoitwa Ibuuta ambavyo ni mfano wa binadamu. Viumbe hivyo vinaelezwa kuwa vifupi mno na vya ajabu. Inadaiwa kwamba wakati mwingine inapofika usiku viumbe hivyo huweza kuonekana. Hata hivyo, inaelezwa kwamba viumbe hivyo vifupi vinapatikana pia katika mataifa kadhaa duniani, lakini vikifahamika kwa majina tofauti.