Majambazi yenye SMG yaua mwanamke na kupora fedha na simu dukani Mwanza

Tarehe 23.09.2016 majira ya saa 19:45 usiku katika mtaa wa Nyakato MECCO wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza, watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha inayodhniwa kuwa aina ya SMG / SAR walivamia duka la vifaa vya ujenzi mali ya Elikana Ngagaya [miaka 38] mkazi wa Kangae na kupora fedha pamoja na simu nne za aina mbalimbali, ambapo bado haijafahamika kiasi cha fedha kilichoibwa na thamani ya simu zote.

Inadaiwa wakati majambazi hao wanaondoka eneo la tukio walifyatua risasi tatu zilizompata Grace Maega [miaka 36] kwenye bega la mkono wa kushoto wakati akizima taa ndani ya duka lake lililopo jirani na duka tajwa hapo juu, kisha wakatokomea gizani, ndipo majeruhi alikimbizwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa matibabu lakini alifariki dunia saa machache baadae kwa kuvuja damu nyingi.

Jeshi la polisi bado lipo katika msako pamoja na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda wa polisi mkoa wa mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza akiwata watulie huku wakiendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi, lakini pia amesema majambazi hao watasakwa popote walipo hadi kutiwa nguvuni, hivyo wananchi wasiwe na mashaka.

Imetolewa na:

DCP: Ahmed Msangi
Kamanda wa polisi (M) Mwanza