Meli kubwa yatia nanga Dar; TPA yafungua milango zije na nyingine nyingi

MV Hammonia Grenada ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema kwamba sasa milango ipo wazi kwa meli kubwa zaidi kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam kwani teknolojia ya meli za kisasa inaruhusu.

Mbali na teknolojia iliyotumika kutengeneza meli hizo, Mamlaka imeboresha ujuzi wa manahodha wake baada ya kuwapeleka katika nchi za Afrika Kusini, Denmark na Ufaransa kupata mafunzo jinsi ya kuingiza meli za aina hiyo bandarini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, Mhandisi Deusdedit Kakoko ameyasema hayo mara baada ya manahodha wa Mamlaka kufanikiwa kuingiza meli kubwa zaidi katika historia ya Bandari ya Dar es Salaam yenye urefu wa mita 261.

Meli hiyo inayoitwa MV Hammonia Grenada ambayo ina uwezo wa kubeba makasha 4,256 imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ambapo imeshusha makasha 483 na kupakia makasha 656 kabla ya kuelekea nchini Thailand.

“Kuingia kwa meli hii katika Bandari yetu ni uthibitisho tosha kwamba bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa kwa kutumia miundombinu iliyopo na kwa ufanisi mkubwa,” alisema Mhandisi Kakoko.

Mhandisi Kakoko amesema kwamba Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa huo katika gati zake nne, ambazo ni gati namba 8,9,10 na 11 ambazo zina kina chenye urefu mita 11.

Mkurugeni Mkuu amesema kwamba ujio wa meli hiyo ni ushahidi tosha kwamba bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa za aina hiyo ambazo awali zilikuwa zikiishia bandari ya Mombasa tu.
Kakoko amesema kwamba wapo waliokuwa wakifikiri kwamba bandari yetu sasa haifanyi kazi lakini ukweli ni kwamba bandari yetu ipo sawa na inaendelea kupokea meli kama kawaida.

Na kuwathibitishia hilo, amesema kwamba hata Mhe. Rais John Pombe Magufuli wakati alipokuja kufanya ziara katika bandari ya Dar es Salaam kulikuwa na meli nyingine saba zimetia nanga.

“Napenda niwatoa hofu wateja wetu kwamba bandari yetu ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa bila shida yoyote na ujio wa meli hii umefungua milango ya meli nyingine kubwa kuja katika bandari yetu,” alisema Kakoko.

Naye Rubani Mkuu wa Mamlaka, Capt. Abdullah Mwingamno ambaye ndiye aliyeengiza meli hiyo amesema kwamba hii ndio meli kubwa kuliko zote ambazo zimewahi kuingia katika bandari ya Dar es Salaam.

Mwingamno amesema kwamba hapo mwanzo mlango wa bandari yetu ulitengenezwa kuweza kuhudumia meli zenye urefu wa mita 234 tu lakini kutokana na mabadiliko ya teknolojia na jinsi meli zenyewe zinavyojengwa imeweza kuingiza hata meli za urefu mkubwa zaidi.

Pamoja na suala la teknolojia, Capt Mwingamno amesema kwamba kwa sasa TPA ina wataalamu wa kutosha ambao wamepata mafunzo sehemu mbalimbali Duniani ili kuweza kuingiza meli kubwa za namna hiyo.

“Tumepeleka kundi la kwanza la vijana wetu nchini Afrika Kusini kupata mafunzo ya jinsi ya kuingiza meli kubwa katika bandari yenye lango kama la kwetu na kundi la pili la vijana hawa tumelipeleka Copenhagen, Denmark,” amesema.

Amesema kwamba kundi la tatu la vijana hao tulilipeleka Nantes nchini Ufaransa kupata mafunzo kama hayo, kwahiyo napenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba tunao wataalamu wa kutosha kuifanya kazi hii.

Hapo awali, TPA ilishawahi kuingiza meli nyingine kubwa yenye urefu wa mita 250 na baadae ikaingiza meli nyingine yeenye urefu wa mita 255.

Kwa mujibu wa Capt. Mwingamno, meli zenye urefu wa mita 261 mara nyingi huishia Bandari ya Mombasa kutokana na udogo wa lango letu lakini ujio wa meli hii umefungua rasmi milango ya kibiashara.

“Ujio wa meli hii umefungua rasmi njia kwa meli nyingine kubwa za aina hii ambazo zilidhani zisingiweza kuingia katika bandari ya Dar es Saam na hivyo kufungua rasmi ushindani na bandari nyingine,” amesema.


Mhandisi Deusdedit Kakoko, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka

MV Hammonia Grenada ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam